Tuesday, May 3, 2016

Wanahabari shirikianeni na Wadau wa Afya kuelimisha Jamii kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

 
 Msimamizi wa Mradi wa Mabadiliko ya Tabia Nchi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Geofrey Mchau akitoa mada mbele ya Waandishi wa Habari kuhusu mabadiliko ya tabianchi nchini wakati wa Semina Maalum kwa Waandishi hao leo 3 Mei, 2016 Jijini Dar es Salaam. 
 Afisa Habari toka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Bwana Saidi Makola akichangia mada mbele ya Waandishi wa Habari kuhusu mabadiliko ya tabianchi nchini wakati wa Semina Maalum kwa Waandishi hao leo 3 Mei, 2016 Jijini Dar es Salaam.
 Dkt. Azma Simba wa Kitengo cha Epidemolojia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambaye alimwakilisha mgeni rasmi katika ufunguzi wa Semina kwa Waandishi wa Habari kuhusu mabadiliko ya tabianchi akisoma taarifa ya Mkurugenzi toka Wizarani leo 3 Mei, 2016 Jijini Dar es Salaam. 
Afisa Habari toka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Catherine Sungura akichangia mada mbele ya Waandishi wa Habari kuhusu mabadiliko ya tabianchi nchini wakati wa Semina Maalum kwa Waandishi hao leo 3 Mei, 2016 Jijini Dar es Salaam.

Na Benedict Liwenga-MAELEZO.

Wanahabari nchini wametakiwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusiana na mabadiliko ya hali ya hewa na afya.

Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Bi. Neema Rusibamayila wa Wizara hiyo, Dkt. Azma Simba wa Kitengo cha Epidemolojia amesema kuwa suala la kuielimisha jamii lina umuhimu ndo maana kuna haja ya Wizara kushirikiana kwa pamoja katika kutekeleza suala hilo.

Ameeleza kuwa Shughuli za kibinadamu zinachangia kwa kiasi cha asilimia 95 katika kuzalisha na kuongeza kiasi cha gesi joto katika kwenye anga hewa ambapo amezitaja baadhi ya shughuli hizo zikiwemo za uzalishaji viwandani, uzalishaji nishati, kilimo,ufugaji, ukataji miti, uchomaji misitu, usafirishaji, pamoja taka. 

Akitaja athari za mabadiliko ya tabianchi, Dkt. Azma ameeleza kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa joto juu ya wastani, ukame, mafuriko, vimbunga, kubadilika kwa mgawanyo na muda mvua kunyesha pamoja na kuongezeka kwa kina cha bahari.

‘’Sisi sote ni mashahidi wa mabadiliko ya hali hewa yalivyokuwa tishio katika afya ya binadamu. Mabadiliko hayo yameendelea kuleta athari mbalimbali kwa jamii, mazingira na afya ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, hewa safi, uhakika wa upatikanaji wa chakula na makazi salama’’, alisema Dkt. Azma.

Ameongeza kuwa athari hizo zimepeleke uwepo wa magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambikiza ikiwemo malaria, kuhara, kipindupindu, homa ya bonde la Ufa, denge, utapiamlo, magonjwa ya mfumo wa upumaji na magonjwa ya mfumo wa fahamu.

‘’Jamii ina fursa ya kuboresha afya yake na vizazi vijavyo endapo itaamua kubadilisha mfumo wa maisha unaochangia uzalishaji na ongezeko wa jotogesi unaoharibu (ozone) yaani tabaka hewa’’, aliongeza Dkt. Azma.

Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi wa Global Framework For Climate Services toka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Geofrey Mchau amesema kuwa halli ya hewa na tabianchi vinaweza kubadilika kiuhalisia (Naturally) au binadamu wenyewe ambapo amefafanua kuwa lengo la semina hiyo ni kuoingeza wigo wa matumizi wa taarifa ya hali ya hewa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya pamoja kuwajengea uwezo Wataalam katika ngazi ya Wizara kimkoa pamoja na Wilaya.

‘’Tupatapo taarifa zinazohusiana na masuala ya hali ya hewa toka Mamlaka ya Hali ya Hewa tunazitafsiri na tunazitumia kwa manufaa ya jamii’’, alisema Dkt. Mchau.

Naye Afisa Habari toka Hospitali ya Taifa Muhimbili Bwana Saidi Makola ameeleza kuwa tafiti zinazoendelea zinaonyesha kuwa kuna ongezeko la magonjwa yatonayo na mfumo wa hewa na hayo yanatokana na mabailiko ya tabianchi, hivyo uwepo wa semina hiyo kwa Wanahabari utasaadia kutambua masuala mbalimbali na kuwajengea uwezo katika kuelimisha jamii.

Aidha, Afisa Habari toka Wizarani hapo, Bi. Catherine Sungura amewaasa Wanahabari kuzingatia katika kutafuta taarifa mbalimbali ili kuweza kuelimisha jamii kuhusiana na masuala mbalimbali yanayohusu afya.

Semina hiyo imehusisha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

No comments: