Na
Veronica Simba
Serikali imesema
ushindani kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika sekta ya nishati, ndiyo njia
bora zaidi itakayowezesha kuwapata wawekezaji wenye vigezo vinavyotakiwa.
Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliyasema hayo jana, Mei 10, alipokutana na
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya KOYO kutoka Japan, Norio Shoji na Ujumbe wake, ambayo
imeonesha nia ya kuwekeza katika uzalishaji na usafirishaji wa umeme nchini,
kwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwemo gesi asilia na jua.
“Kampuni nyingi
zimeonesha nia ya kuwekeza kwenye sekta ya nishati. Serikali inao uhitaji
mkubwa wa wawekezaji walio makini, hivyo tunahitaji kuwapata wawekezaji wenye
vigezo kwa kutumia ushindani unaozingatia uwazi,” alisisitiza Profesa Muhongo.
Aliongeza kuwa, ili
kuwarahisishia wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya nishati nchini,
Wizara inaandaa taarifa maalum itakayobainisha maeneo yanayohitaji uwekezaji
pamoja na vipaumbele vyake.
Alisema, taarifa hiyo
itakuwa tayari na kutolewa mwishoni mwa mwezi huu (Mei 31, 2016) na kwamba
itasambazwa kwa wadau wote wa ndani na nje ya nchi kupitia njia mbalimbali za
mawasiliano, ikiwamo tovuti ya wizara.
Profesa Muhongo
alieleza kuwa, taarifa hiyo pamoja na mambo mengine, itawapa fursa wawekezaji
wenye nia, kuchagua aina ya uwekezaji wanaohitaji kufanya na katika maeneo
ambayo wanadhani watakuwa na uwezo wa kumudu ushindani kutoka kwa wawekezaji
wenzao kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Akifafanua zaidi,
Profesa Muhongo alisema kuwa, zoezi la kuwashindanisha wawekezaji walioonesha
nia, litakuwa ni endelevu na litakuwa likifanyika kila baada ya muda fulani,
ambao utabainishwa katika taarifa husika inayotarajiwa kutolewa.
Akitoa mfano, alisema
kuwa, siyo lazima kumpata mwekezaji katika zoezi la ushindanishaji, hivyo ni
muhimu zoezi liwe endelevu ili kuweza kutoa fursa kwa wawekezaji wengi zaidi
kushiriki na hivyo kumpata mwekezaji mwenye vigezo vyote ambavyo Serikali
inavihitaji.
“Endapo tutaendesha
zoezi la ushindanishaji wawekezaji na wote walioshindanishwa wasipotimiza
vigezo vinavyotakiwa, hatulazimiki kumchukua yeyote tu. Tutakachofanya ni
kutokumchukua yeyote kati yao na hivyo kuendelea na zoezi hilo baada ya muda
tutakaoubainisha, hadi pale tutakapowapata wawekezaji wenye vigezo
tunavyovitaka.”
Profesa Muhongo
alibainisha kuwa, mchanganyiko wa nishati ambao Serikali imekusudia kuutumia
kama vyanzo vya kuzalisha umeme nchini kwa sasa ni pamoja na gesi asilia, maji,
upepo, jua, makaa ya mawe, mvuke (maji moto) na tungamotaka.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kushoto), akiagana na
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya KOYO kutoka Japan, Norio Shoji (Kulia)
pamoja na Ujumbe wake, baada ya kikao baina yao. Kushoto kwa Waziri ni
baadhi ya Viongozi na Maofisa wa Wizara na Taasisi zake walioshiriki
kikao hicho kilichofanyika Mei 10, mwaka huu Makao Makuu ya Wizara
jijini Dar es Salaam. KOYO imeonesha nia kuwekeza katika sekta ya
nishati nchini.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati,
Dkt Mhandisi Juliana Pallangyo (Kulia), akisalimiana na Mtendaji Mkuu wa
Kampuni ya KOYO kutoka Japan, Norio Shoji, baada ya kikao baina ya
Waziri wa Nishati wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na
Kampuni husika, kilichofanyika Mei 10 mwaka huu Makao Makuu ya Wizara
jijini Dar es Salaam. Kampuni ya KOYO imeonesha nia kuwekeza katika
sekta ya nishati nchini.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Katikati), akiwa katika
kikao na Ujumbe kutoka Kampuni ya KOYO ya Japan (Kushoto). Kulia ni
baadhi ya Viongozi na Maofisa wa Wizara na Taasisi zake walioshiriki
kikao hicho kilichofanyika Mei 10 mwaka huu, Makao Makuu ya Wizara
jijini Dar es Salaam. Kampuni hiyo imeonesha nia kuwekeza katika sekta
ya nishati nchini.
No comments:
Post a Comment