Monday, April 18, 2016

WAKUFUNZI 53 WA JKT WAFUZU MAFUNZO YA UJASIRIAMALI YA NEEC.

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama akimkabidhi cheti mmoja wa wakufunzi wa mafunzo ya vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Athuman Libanda baada ya kuhitimu mafunzo ya siku 12 ya ujasiriamali yaliyoendeshwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na kumalizika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kwenda kuwafundisha vijana wanaojiunga na jeshi hilo. Kushoto ni Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT, Bregedia Jenerali, Michael Isamuhayo, Katibu Mtendaji wa NEEC, Bi. Beng’i Issa (nguo nyekundu) na viongozi wengine wa jeshi hilo. 
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, .Jenista Mhagama akimkabidhi cheti mmoja wa wakufunzi wa mafunzo ya vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Bi. Joyce Shauza baada ya kuhitimu mafunzo ya ujasiriamali ya siku 12 yaliyoendeshwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na kumalizika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kwenda kuwafundisha vijana wanaojiunga na jeshi hilo. Kushoto ni Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT, Bregedia Jenerali, Michael Isamuhayo, Katibu Mtendaji wa NEEC,  Beng’i Issa (nguo nyekundu) na viongozi wengine wa jeshi hilo. 
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama (katikati) akiondoka katika ukumbi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mara baada ya kufunga mafunzo ya siku 12 ya wakufunzi wa somo la ujasiriamali mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.  Kulia ni  Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bi. Beng’i Issa na kushoto ni Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali, Michael Isamuhayo. Mafunzo hayo yaliendeshwa na NEEC.

Na Mwandishi wetu.
Jumla ya wakufunzi 53 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wamehitimu mafunzo ya ujasiriamali na kutunukiwa vyeti.

Mafunzo hayo yaliendeshwa kwa muda wa siku 12 na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Mafunzo hayo yalifanyika katika kambi ya Mgulani na kuhusisha mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Pwani. 

Akikabidhi vyeti hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Kazi, Ajira Vijana na Walemavu,Bi.Jenista Mhagama alisema wakufunzi hao wana wajibu wa kuwafundisha somo la ujasirimali vijana wanaojiunga na jeshi hilo ili kupambana na tatizo la ajira nchini.

“Mafunzo mliyopata yalilenga kuwawezesha mkawafundishe vijana ili baada ya hapo waweze kujiajiri au kuajiri wengine,” alisema,Bi. Mhagama mwishoni mwa wiki.

Alifafanua kwamba kuwafundisha somo la ujasiriamali itasaidia kwenda sambamba na soko la ajira katika sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo, utalii, hoteli na kwamba nguvu kazi kubwa ya vijana itakuwa inafanya kazi badala ya kukaa tu na kupenda starehe.

Alisema serikali ya awamu ya tano imejielekeza katika kuwezesha wananchi na jeshi hilo lina nafasi kubwa ya kutumia fursa iliyonayo kusaidia kukuza vijana ili kwa pamoja kufikia uchumi wa kati mwaka 2025.

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT, Brigedia Jenerali, Michael Isamuhayo alisema jeshi limejipanga kuwafundisha vijana wanaopitia mafunzo hayo ipasavyo ili wawe chachu ya kukuza vipato vyao na uchumi wa nchi.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bi. Beng’i Issa alisema utoaji wa mafunzo hayo kwa wakufunzi wa vijana kwa jeshi hilo ni utekelezaji wa sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.

“Kupitia mafunzo haya wakufunzi watapata fursa ya kwenda kuwafundisha vijana kupata stadi na kushiri katika uzalishaji mali na kuendesha maisha yao,”alisema,Bi. Issa.

Aliwahimiza vijana wanaohitimu masomo wajiunge na mafunzo ya JKT kwa wingi na huko watakutana na mafunzo hayo yanayolenga kuwajenga kujitegemea.

Kwa mujibu wa program hiyo, kanda itakayofuata itakuwa ya Kati na Magharibi itakayojumuisha mikoa ya Dodoma, Kigoma, Tabora na Mwanza,”alisema.

Mafunzo yatafanyika katika kambi ya Makutopora, Dodoma, Mafunzo hayo katika kanda ya Kusni yatafanyika Mafinga ambapo mikoa itakayohusika itakuwa Ruvuma, Mbeya, Songwe, Rukwa, Iringa na Njombe.

Mafunzo katika kanda ya Kaskazini yatafanyika katika kambi ya Mgambo mkoani Tanga na kuhusisha mikoa ya Tanga, Arusha na Kilimanjaro.

Tangu kurejeshwa kwa utaratibu wa mafunzo ya vijana wa kujitolea mwaka 2001 idadi ya vijana wanaojiunga na JKT imeendelea kuongezeka kila mwaka.

Vijana waliopita JKT hadi mwaka 2014 ni 104,594.  Kati ya idadi hii, vijana 34,291 waliingia kwa mpango wa kujitolea ambapo asilimia 70 waliajiriwa na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama.

Asilimia 30 inayobaki, sawa na vijana 2,000 wanarudi nyumbani kila mwaka, Mafunzo hayo yanaendeshwa na wakufunzi wanaotambuliwa kimataifa. 

No comments: