Sunday, April 24, 2016

Serikali yahamasisha wawekezaji viwanda vya kuongeza thamani

Serikali imewataka wawekezaji wa ndani na nje kutumia fursa zilizopo Tanzania hasa katika eneo la kuongeza thamani ya malighafi mbalimbali.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dkt. Adelhelm Meru alipokuwa akiongea na maafisa kutoka kampuni ya nchini Ufaransa ya Endel Engie mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Maafisa wa kampuni hiyo walikuwa nchini na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali waandamizi wa serikali kueleza nia yao ya kuwekeza Tanzania na kujua fursa zilizopo nchini.

Endel moja ya makampuni ya Engie Group yenye mapato yanayofikia Euro milioni 700 kwa mwaka na waajiriwa 6,000 nchini Ufaransa.

Baadhi ya shughuli za kampuni hiyo ni katika maeneo ya sayansi za anga, viwanda vya vyakula, reli, gesi, ujenzi wa meli, nishati ya nyuklia na viwanda vya chuma miongoni mwa vingine.

Kwa bara la Afrika, kampuni hiyo inafanya kazi katika nchi za Afrika ya Kusini, Angola na Congo DRC.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo, Dkt. Meru alisema eneo la kuongeza thamani bado halijafanyiwa kazi na lina fursa kubwa kwa watu wanaotaka kuwekeza katika viwanda vya aina hiyo.

“Kama serikali tunaweka mazingira mazuri ya kuhakikisha kuwa watu wanawekeza kwa faida ya pande zote mbili,” alisema.

Aliwaambia maafisa wa kampuni hiyo kuwa utulivu wa kisiasa na amani iliyopo Tanzania vinaifanya kuwa eneo bora la kuwekeza katika ukanda huu wa Afrika.

Kampuni hiyo iko katika mchakato wa kutafuta fursa na vivutio vya kuwekeza katika nchi za Tanzania, Kenya na Msumbiji.

Aliyataja maeneo mengine yenye fursa za kuwekeza kama madini, Kilimo, utafutaji wa gesi na mafuta na uzalishaji nishati miongoni mwa nyingine.

Makamu wa Rais, Maendeleo ya Kimataifa, Endel Engie, Bw. Olivier Rousseau alisema wamevutiwa na hali ya amani, utulivu na raslimali katika eneo hili la Afrika na hasa Tanzania.

“Tuko katika ziara ya kujifunza,” alisema.

Kwa mujibu wa afisa huyo, mwezi wa Kumi mwaka huu, wawakilishi wa kampuni hiyo, watarudi Tanzania na mapendekezo rasmi ya maeneo watakayokuwa wanataka kuwekeza hapa nchini.

Mbunge mstaafu wa jimbo la Mbinga Magharibi ambaye aliambatana na wawekezaji hao, Bw. Gaudence Kayombo alisema huu ni wakati wa kuitikia kwa vitendo azma ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda.

Alisema uwekezaji katika maeneo hayo utasaidia kuleta teknolojia, mitaji na uzoefu Tanzania.

Serikali imedhamiria kuwa ifikapo mwaka 2020, asilimia 40 ya ajira zote  na asilimia 15 ya pato la Taifa vitokane na sekta ya viwanda.

No comments: