Serikali
imeliagiza Shirika la Reli Tanzania (TRL), kupitia upya mikataba ya ununuzi wa
vichwa vya treni na mabehewa ili kubaini kasoro zilizojitokeza na kuchukua
hatua stahiki kabla ya maboresho ya reli ya Tanga-Moshi-Arusha.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa agizo hilo mkoani
Kigoma wakati akikagua miundombinu ya reli na kusissitiza nia ya serikali
kufufua reli ya kanda ya kaskazini ili kuimarisha huduma ya uchukuzi katika
mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
“Kama Serikali tumewekeza vya kutosha katika
TRL, hivyo tunawataka mfanye biashara itakayolipa nasi tutahakikisha popote
reli ilipo inatoa huduma iliyokusudiwa na kuchangia kukuza uchumi wa nchi”,
amesema Prof. Mbarawa.Prof. Mbarawa amewataka
wafanyakazi wa TRL kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kupata bidhaa na
abiria wengi wa kuwasafirisha nchini kote.
Amesema
Serikali imedhamiria kuliongezea nguvu TRL ambapo baadhi ya mitambo kutoka
Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) itakabidhiwa kwa shirika hilo hivyo
kulitaka kuwa na mpango madhubuti wa kufanya biashara na kurudisha hadhi ya
usafiri wa reli hapa nchini.
“Fanyeni bidii ili mpate mzigo wa kusafirisha
kutoka Tanga kwenda Moshi na Arusha ili kufikia lengo la kubeba mzigo wa tani
milioni moja kwa mwaka”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Amezungumzia
umuhimu wa TRL kuafanya kazi kwa karibu na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
nchini (TPA), ili kuongeza kasi ya huduma za uchukuzi nchini, kuongeza fursa za
ajira na kukuza pato la shirika na taifa.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mkuu wa TRL, Bw. Masanja Kadogosa amesema TRL imejipanga kutafuta
masoko ndani na nje ya nchi ili kuboresha huduma za uchukuzi na kukuza pato lake.
Katika hatua
nyingine Prof. Mbarawa amekagua Meli ya MV Liemba na kuitaka Mamlaka ya
Usimamizi wa usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), kuhakikisha meli za MV
Liemba na MV Mwongozo zinakaguliwa na kufanya kazi inavyostahili katika Ziwa la
Tanganyika.
“Tumieni fursa
ya kuwa karibu na nchi za maziwa makuu kufanya biashara ili meli zetu zipate
mzigo wa kutosha na kuongeza mapato kwa taifa”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa
ambaye yupo katika ziara mkoani Kigoma amewataka viongozi na wafanyakazi wa
taasisi zilizo chini ya wizara yake kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuibua
fursa za kiuchumi katika ukanda wa magharibi na hivyo kufufua miundombinu
itakayochochea uchumi wa mikoa ya magharibi mwa Tanzania yenye fursa nyingi za
kibiashara.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati) akimsikiliza
mmoja wa abiria anayetumia usafiri wa reli ya kati mkoani Kigoma. Kushoto ni
Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Zitto Kabwe na Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kigoma
Saveli Maketta.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na
wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), mkoani Kigoma.
Muonekano wa
mabehewa ya treni yakiwa mwisho wa reli ya kati, mkoani Kigoma.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kushoto)
akipata maelezo kutoka kwa Kapteni wa Meli ya MV Liemba ya namna
inavyoendeshwa, mkoani Kigoma.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kulia), akipata
ufafanuzi wa namna ya injini za Meli ya MV Liemba zinavyofanya kazi wakati
alipotembelea Meli hiyo mkoani Kigoma.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (mwenye kizibao cha
njano), akimsikiliza Kapteni Winton Mwassa (wa kwanza kulia), kutoka Kampuni ya
huduma za meli mkoani Kigoma mara baada ya kutembelea na kuona hali ya MV
Liemba.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment