Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe Steven Kebwe, (katikati) pamoja na ujumbe wake wakifanya ukaguzi wa kushitukiza katika mgodi wa Kiwanda cha Tanzania Zhong Fa Construction Material Group Co Ltd , katika mgodi wa Kiwanda hicho uliopo eneo la Kitongoji cha Mazizi, Kijiji cha Maseyu, Kata ya Gwata, Tarafa ya Mikese, wilaya ya Morogoro, kiwanda hicho kinamilikiwa na wachina, uzalishaji wake ulizuiwa na Serikali kuu tangu mwaka 2010 hadi watakapokamilisha taratibu zote za kisheria zikiwemo na za kimazingira.
Mfanyakazi raia wa China, Wang Jun (33) ambaye ni mtunza stoo katika mgodi wa kutengeneza marumaru wa Kiwanda cha Tanzania Zhong Fa Construction Material Group Co Ltd ,kinachomilikiwa na Wachina akiwa chini ya ulinzi wa Polisi kufuatia ukaguzi wa ghafla wa mkuu wa mkoa wa Morogoro Dk Kebwe Steven Kebwe, Aprili 13,2016 akifuatana na ujumbe wa serikali ya mkoa na wilaya ya Morogoro katika mgodi wa Kiwanda hicho uliopo Kitongoji cha Mazizi, Kijiji cha Maseyu, Kata ya Gwata, Tarafa ya Mikese , ambapo walikutwa wakiendelea na uzalishaji licha kuzuiwa na Serikali kuu mwaka 2010 hadi watakapokuwa wamekamilisha taratibu zote za kisheria zikiwemo na za kimazingira.
Na John Nditi, Morogoro
RAIA wawili wa China wametiwa nguvuni mkoani Morogoro kutokana na kuendelea kusimamia shughuli za uzalishaji wa marumaru katika mgodi wa mawe wa Kiwanda cha Zhong Fa Construction Material Group Co Ltd ,kinachomilikiwa na Wachina licha ya kuzuiwa na Serikali kuu tangu mwaka 2010.
Mbali na kuendelea na uzalishaji katika kipindi chote hicho, kampuni hiyo imekuwa ikifanya udangayifu kuwa marumaru zinazouzwa katika maduka yake zinaingizwa kutoka nchini China , wakati bidhaa hiyo ikitengenezwa kutoka Morogoro.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Steven Kebwe, aliamuru kukamatwa kwa raia hao baada ya kufanya ukaguzi wa kushitukiza Aprili 13, 2016 akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa pamoja na viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Morogoro.
Kampuni hiyo ilizuiwa kuendelea na uzalishaji wa marumaru katika mgodi uliopo katika Kitongoji cha Mazizi, Kijiji cha Maseyu, Kata ya Gwata, Tarafa ya Mikese tangu Novemba 30, mwaka 2010 , lakini imeendelea na uzalishaji kwa kipindi chote hicho bila kuwa na vibali wala taratibu zote za kisheria zikiwemo za hifadhi ya kimazingira.
Hatua ya Mkuu kufanya ziara hiyo ni kwenda kujiridhisha kutokana na taarifa ya uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Morogoro iliyowasilisha vielelezo mbalimbali juu ya kampuni hiyo kushindwa kulipa tozo la kiasi cha Sh milioni sita kwa hesabu za wakati huo kabla ya kuzuiwa na Serikali.
Dk Kebwe alisema, licha ya kuzuiwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ,wakati wa Serikali ya awamu ya nne kabla ya mabadiriko ya wizara hiyo baada ya Waziri kutembelea mgodi huo na kukuta wakiendesha uzalishaji bila kuwa na leseni na vibari kutoka katika mamkala mbalimbali ikiwemo ya wizara hiyo .
“ Tangu wakati wa Waziri Profesa Muhongo awamu ya kwanza walipozuiwa kuendea na uchimbaji hadi watakapo kamilisha utaratibu wa kisheria zikiwemo na za hifadhi ya kimazingira, wameendelea kuzalisha katika mgodi bubu ...wamechimba eneo na kurivuruga kimazingira “ alisema Mkuu wa Mkoa Dk Kebwe.
Dk Kebwe alisema , uzalishaji wa marumaru katika mgodi huo umekuwa ikiendelea kwa njia zisizo halali ambapo bidhaa hiyo inatengezwa eneo hilo na kusafirishwa katika maduka ya Kampuni hiyo yaliyopo Jijini Arusha na Dar es Salaam kwa ajili ya kuuzwa ndani na nje ya nchi.
“ Ufuatiliaji umekuwa ukifanyika mara kwa mara eneo la mgodi na uzalishaji umekuwa ukifanyika kama tulivyowakuta hapa na marumaru hizi zikifikishwa katika maduka hayo zinajazwa kwenye makadha yaliyoandikwa kwa lugha ya kishina ya kampuni hii na kuonesha zimeingizwa kutoka China na kuuzwa ka bei ghali “ alisema Dk Kebwe.
“ Tumenunua marumaru zilizo kwenye maduka haya na kubaini hazitoki China bali ni Morogoro kwenye mgodi unaozalisha bidhaa hizi na kuwekwa nembo ya Kichina kwa jina hilo la kampuni ...huu ni wizi na kuikosesha serikali na halmashauri mapato yake” alisisitiza Mkuu wa mkoa , Dk Kebwe.
Mkuu wa mkoa , Dk Kebwe alisema , tangu mwaka 2010 walipozuiwa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, uzalishaji umeendelea kukua katika mgodi huo ambapo marumaru hizo kwa sasa zinasafirishwa kuuzwa katika nchi jirani za Afrika Mashariki na Kati zikiwa na lebo ya kutoka nchini China.
“ Kutokana na udanganyifu na wizi unaofanyika ndiyo maana kiwanda hiki hakijafungua Duka hapa Morogoro isipokuwa ni Dar es Salaam na Arusha ili watanzania wajue ni bidhaa kutoka China , na bei ya chini ya marumaru moja ndogo ni Sh 280,000 , jambo hilo lazima tulikomeshwe “ alisema Dk Kebwe.
Pia Dk Kebwe aliitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Morogoro kuanza mara moja kufanya tathimini ya mauzo ya marumaru zinazotokana na uzalishaji wa mgodi huo ili kupata mauzo halisi ya Kampuni ili kuiwezesha halmashauri kupata malipo ya halali .
Kutokana na kukaidi agizo la Serikali , mkuu wa mkoa Dk Kebwe aliamuru kukamatwa kwa wafanyakazi wawili wa China wa Kiwanda cha Zhong Fa Construction Material Group Co Ltd na msimamizi wa kitanzania kwa lengo la kuisaidia serikali ya mkoa katika uchunguzi wake juu ya kiwanda hicho.
Wachina waliokamatwa na Polisi eneo la mgodi ni Mtunza stoo Wang Jun (33) na mwezake Shiqing Liang (36) ,wakati mtanzania ni Hilary Paulo.
Naye Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro, Bertha Luzabiko, alimwezeza mkuu wa mkoa kuwa licha ya kuhamia mkoa huo mnamo Novemba mwaka 2014 , kazi yake ya kwanza ilikuwa ni kushughulikia maombi ya Kampuni hiyo , lakini iligundulika kuwa eneo hilo tayari lina leseni ya mwekezaji mwingine na si rahisi kutolewa nyingine.
Luzabiko alisema aliwaadikia barua wenye mgodi huo ya kuwasimamisha kuendelea na kutokana na eneo hilo lina leseni ya mtu mwingine wa uchimbaji wa dhahabu.
Hivyo alisema baada ya kuwandikia barua ya kusitisha shughuli zao , aliamua kufanya mara tatu kwa nyakati tofauti alikuta shughuli uchimbaji na utengenezaji wa marumaru ukiendelea , ndipo alipoamua kuripoti Polisi ili watu hao wakamatwe na kufunguliwa kesi mahakamani zoezi ambalo lilifanyika.
Lizabiko alisema, licha ya kukamatwa kwao, bado waliendelea na uzalaishaji ambapo pia aliamua kulifikisha suala hilo kwa Kamishina wa Madini Kanda ya Mashariki aliyemtaja kwa jina la Hamis Komba ili kuchukua hatua za kisheria na kiutawala.
Naye Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mkoa wa Morogoro Philip Kimune , aliyefuatana na Mkuu wa mkoa eneo la mgodi huo alisema taarifa zilizipo kwenye Mamkala ya Mapato zinaonesha kuwa , kampuni hiyo inatumia jina la Tanzania Zhong Fa Construction Material Group Co Ltd.
Alisema ,kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2011 hadi Machi 2016 kiwanda hicho kilionesha kuwa mauzo ya kiasi cha Sh bilioni 30.9 yaliyolipiwa Vat ya Sh bilioni 5.5.
Mbali na hayo alisema , mauzo hayo hayakuonesha iwapo yalitokana na bidhaa ya marumaru ama yalijumuishwa na bidhaa nyinginezo zinazozalishwa na kampuni hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Yona Maki alisema , kuchelewa kwa mchakato wa kukusanya ushuru katika kiwanda cha kuchoronga mawe cha wachina kinaikoseha mapato halmashauri kiasi cha zaidi ya Sh milioni 90 kwa kipindi cha miaka sita kuanzia mwaka 2010.
Sehemu ya Muonekano wa Kiwanda hicho.
Mfanyakazi wa Mgodi huo, Hilary Paulo (kulia) akimpatia maelezo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe Steven Kebwe.
No comments:
Post a Comment