WANANCHI wa Jimbo la
Kikwajuni Zanzibar, wametakiwa kujenga tabia ya kufanya usafi wa mazingira
katika maeneo yao ili kuepuka maradhi ya kipindupindu yanayoathiri maeneo mbali
mbali nchini.
Wito huo umetolewa kwa
nyakati tofauti na Mbunge wa jimbo la Kikwajuni, Muandisi Hamad Yussuf Masauni
alipokuwa akifanya usafi wa mazingira katika maeneo mbali mbali ya jimbo hilo
Mjini hapa.
Alisema maeneo mengi ya
jimbo hilo hasa katika Majumba ya Maendeleo ya Michenzani ni machafu sana hali inayoweza kusababisha maradhi ya miripuko
yakiwemo kipindupindu na kichocho.
Masauni ambaye pia ni
Naibu Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, alieleza kuwa wananchi wa maeneo hayo
wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira na kupelekea
uharibifu wa miundombinu ya kusafirisha maji taka ikiwemo mitaro kuziba.
“ Nachukua fursa hii
kuwakumbusha wananchi wa kikwajuni kuwa suala la usafi wa mazingira halina
itikadi za kisiasa ni lazima wananchi sote tuungane bila ya kujali tofauti za
kisiasa.
Pia nakuombeni wananchi
hasa mnaoishi katika majumba ya michenzani mbadilike kwa kujali mazingira yenu
kwani mjue kuwa endapo eneo hili litapata maradhi ya mripuko kuna hatari ya
wananchi wengi kupoteza maisha kwa maradhi ambayo tuna uwezo wa kuyazuia.”,
alisema Masauni huku akisisitiza umuhimu wa kufanya usafi wa mara kwa mara katika
maeneo hayo.
Alisema viongozi wa
jimbo hilo kwa sasa wanapanga kuanzisha kikundi maalum cha vijana wa kufanya
usafi katika maeneo ya jimbo hilo, ambapo kila kaya(nyumba) watakuwa
wanachangia kiasi cha shilingi 200 kila siku ili fedha hizo ziweze kuwasaidia
watu wanaofanya usafi huo.
“Aibu kubwa kuona ndani ya jimbo la kikwajuni
panaanza kupatikana wagonjwa wa maradhi ya kipindupindu kwani ni jimbo lenye
sifa ya usafi na ukaribmu toka enzi na enzi tena lipo mjini, lazima
tushirikiane kufanya usafi katika maeneo yetu.” Alisema Masauni.
Aidha aliishauri
Manispaa ya Zanzibar kuanza mara moja utafti wa kubaini mifumo ya maji machafu
na masafi inayoingiliana katika maeneo hayo ili kuifanyia matengenezo kwa
haraka kabla hapajatokea maafa ya maradhi ya miripuko na kusababisha athari kwa
wananchi wa maeneo hayo.
Kwa upande wake
Mwakilishi wa Jimbo hilo, Nassor Salum Ali(Jazeera) aliwapongeza wananchi wa
jimbo hilo waliojitokeza kufanya usafi wa mazingira kwa lengo la kuweka maeneo
yako katika hali ya usafi.
Jazeera alisema kwamba
kinga ya maradhi ya mripuko hasa kipindupindu ni usafi wa mazingira hivyo kila
mwananchi anatakiwa kutekeleza wajibu wake bila ya kulazishwa na mtu.
Naye Mkurugenzi wa
Manispaa ya Zanzibar, Aboud Hassan Serenge alisema kila mwananchi ana jukumu la
kufanya usafi wa mazingira katika maeneo anayoishi kwa lengo la kuweka mji wa Zanzibar
katika hali ya usafi.
Serenge alifafanua kwamba
kuna baadhi ya wananchi wamekuwa wakichafua mazingira ya mji kwa makusudi huku
wakidai kuwa Manispaa ipo na ndiyo yenye dhamana ya kufanya usafi jambo ambalo
sio sahihi kwani kila mtu suala la usafi linamuhusu.
Mkurugenzi huyo
alieleza kuwa endapo wananchi wa manispaa ya Zanzibar wataendelea kushirikiana
vizuri na mamlaka hayo katika kuweka mjini wa Zanzibar katika hali ya usafi, basin
chi itarudi katika historia ya haiba na usafi uliotukuka kama ilivyokuwa miaka
ya nyuma.
Alisema Manispaa ina
mpago wa kufanya marekebisho katika maeneo mbali mbali ya mji wa Zanzibar yanayoonekana
kuwa na tatizo la kuziba kwa mitaro na mifereji ya maji machafu inayopita chini
kwa chini ili kuzuia uchafu unaosambaa katika maeneo mbali mvali ya mji huo.
No comments:
Post a Comment