1. Mheshimiwa Spika, awali
ya yote, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mwingi wa Rehma kwa
kuendelea kuweka nchi yetu hii katika hali ya amani, utulivu, umoja na
mshikamano mkubwa. Hali ambayo imeiwezesha Serikali na wananchi kuendelea na
shughuli zao za kila siku bila ya mtafaruku wa aina yeyote. Aidha, tunaendelea
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufanya uchaguzi katika hali ya amani
na utulivu, jambo ambalo sote tuliomo humu Barazani pamoja na wananchi wote ni
mashahidi wa hilo. Ninawaomba wananchi waendelee kuitunza na kuithamini amani
iliopo nchini.
2. Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena, napenda
kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha hapa tukiwa
katika hali ya uzima na afya njema na kutuwezesha kufanikisha vizuri Mkutano wa
Kwanza wa Baraza hili Tukufu la Tisa la Wawakilishi, ulioanza tarehe 30 Machi,
2016. Nimefarijika kuwa kazi zote zilizopangwa katika ratiba yetu
tumezikamilisha kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.
3. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kwa
niaba yangu na Waheshimiwa Wawakilishi kutoa pongezi za dhati kwako wewe Mhe.
Spika pamoja na Naibu Spika, Mhe. Mgeni Hassan Juma kwa kuchaguliwa kwa kura
nyingi kuliongoza Baraza letu hili Tukufu. Vile vile, nampongeza Mhe. Riziki
Pembe Juma, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Viti Maalum na Mhe. Shehe Hamad
Mattar, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Mgogoni, Pemba kwa kuchaguliwa
kuwa Wenyeviti wa Baraza letu hili. Hii inaonesha imani kubwa waliyonayo
Waheshimiwa Wajumbe juu yao. Ni mategemeo ya Waheshimiwa Wajumbe kwamba
mtaliongoza Baraza hili Tukufu kwa hekima, busara, uadilifu na umakini mkubwa
ili kuliwezesha Baraza kutekeleza majukumu yake yakiwemo ya kuisimamia Serikali
kwa ufanisi na kupeleka maendeleo endelevu kwa wananchi wetu na nchi yetu kwa
ujumla.
Aidha, nachukua fursa hii kuwapongeza
Waheshimiwa Hamza Hassan Juma, Salha Mohamed Mwinjuma, Rashid Ali Juma, Lulu
Msham Abdulla na Hamad Abdulla Rashid kwa kuchaguliwa kwao kuwa Wajumbe wa
Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi.
Kuchaguliwa kwao kunadhihirisha imani kubwa ambayo Waheshimiwa Wajumbe
aliyonayo juu yao, kwani Kamati hii ni muhimu sana kwa maendelezo ya Baraza
letu.
Aidha, napenda kuwapongeza wenzetu saba
walioteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na hivi
karibuni tu uliwaapisha. Wajumbe hao
wakiwa Mhe. Mohamed Aboud Mohamed, Mhe. Amina Salum Ali, Mhe. Maudline Castico,
Mhe. Ali Abeid Karume, Mhe. Hamad Rashid, Mhe. Juma Ali Khatib na Mhe. Said
Soud Said. Kuteuliwa kwao kunaonyesha
imani kubwa ambayo Mheshimiwa Rais anayo juu yao na kwamba michango yao
italisaidia sana Baraza lako Tukufu.
4. Mheshimiwa Spika, napenda kutoa pongezi
maalum kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kuchaguliwa kwa ushindi wa kishindo wa zaidi ya
asilimia 91 kushika wadhifa huo katika muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya
Saba kupitia uchaguzi wa marejeo uliofanyika tarehe 20 Machi, 2016. Aidha, pamoja na pongezi hizo, napenda kutoa shukrani zangu
za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa imani kubwa aliyoionesha
kwangu kwa kuniteua kuwa Makamu wa Pili wa Rais kwa mara nyengine tena. Namuomba Mwenyezi Mungu atubariki na
kutujaalia afya njema na nguvu ya kuwatumikia wananchi wote hapa Zanzibar bila
kujali rangi, jinsia, dini au itikadi zao za kisiasa.
5. Mheshimiwa Spika, aidha, kwa niaba ya Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar, napenda kutoa pongezi za dhati kwa Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu
Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuchaguliwa kwa
kura nyingi sana. Hii imeonyesha imani
na upendo kwa wananchi wa Tanzania walioayo juu yao. Pia nampongeza Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo. Hii inaonyesha imani ambayo Mhe. Rais
Magufuli aliyonayo juu yake.
Ni matumaini yetu kwamba viongozi wetu hao
watalitumikia Taifa letu kwa hekima na busara ili kuwapatia wananchi wetu
maendeleo ya dhati. Tunampongeza Rais
Magufuli kwa kasi aliyoanza nayo.
6. Mheshimiwa Spika, Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein tarehe 05
Aprili, 2016 alilituhutubia Baraza hili Tukufu kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo
Kikatiba. Pamoja na mambo mengine, katika hotuba yake amefafanua kwa kina
kuhusu wajibu wetu kama Wajumbe wa Baraza hili, na ameeleza masuala muhimu
katika kuijenga Zanzibar yetu.
7. Mheshimiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais
itakuwa dira na mwongozo wetu katika kutekeleza majukumu yetu ndani na nje ya
Baraza hili kwani hotuba hiyo iligusa kila Sekta ya maendeleo yetu. Wajumbe mlipata nafasi ya kuijadili hotuba
hiyo kuanzia tarehe 6 Aprili, 2016 hadi leo hii.
Michango ya
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako tukufu ilijikita zaidi juu ya uwepo wa amani
na utulivu, kuboresha na kuimarisha maeneo huru hasa ya Fumba na Micheweni,
vita dhidi ya rushwa na udhalilishaji wa kijinsia, wanawake na watoto,
uendelezaji wa elimu na Vyuo vya Amali, mazingira, ajira kwa vijana, ukusanyaji
wa mapato na ulipaji wa kodi kwa kutaja machache. Naliahidi Baraza lako tukufu kuwa Serikali
itachukua hatua ya kuyashughulikia mapendekezo yote yaliyotolewa. Kama Mwanasheria Mkuu alivyosema, michango
yote hiyo itawekwa kwenye jeduali maalum (Bango Kitita) na kusambazwa kwa Mawaziri
wote watakaohusika.
8. Mheshimiwa Spika, Baraza hili Tukufu la
Wawakilishi lina jukumu muhimu na kubwa la kutunga Sheria. Napenda kuwakumbusha
Waheshimiwa Wawakilishi kwamba hiyo itakuwa ndiyo kazi yetu ya msingi,
inayotakiwa kufanywa kwa busara, hekima na umakini mkubwa. Pia, tunalo jukumu la kuisimamia na kuishauri
Serikali ili kuhakikisha kuwa matatizo na kero mbali mbali za wananchi
zinatatuliwa kwa ufanisi na mafanikio makubwa.
Tunapaswa kuhakikisha kuwa Serikali inatoa mchango wake kikamilifu
katika kuyafanya maisha ya wananchi wetu kuwa bora zaidi kwa kutumia nguvu kazi
na rasilimali tulizonazo. Ni matarajio ya Serikali kuwa itapata taarifa na
ushauri kutoka kwa Waheshimiwa Wawakilishi juu ya maeneo yanayohitaji kupewa
msukumo ili kuongeza kasi ya maendeleo ya Zanzibar. Kwa upande wake, Serikali
itaifanyia kazi taarifa na ushauri utakaotolewa na Baraza hili Tukufu.
9. Mheshimiwa Spika, sambamba na majukumu hayo,
naomba kuwashauri Waheshimiwa Wawakilishi tuwe karibu na wananchi
waliotuchagua. Sisi ndio macho na masikio ya wananchi hao. Tumepewa heshima
kubwa na wananchi hao kwa kutuchagua kuwa Wajumbe wa Baraza hili. Wananchi hao wana mategemeo makubwa kwamba
tutawasaidia kutatua changamoto zao mbali mbali za maendeleo zinazowakabili. Ni
wajibu wetu kufikisha mawazo ya wananchi hao Serikalini kwa kupitia mikutano na
vikao vya Baraza hili pamoja na njia nyengine zinazofaa. Aidha, tunapaswa
kuwaeleza wananchi wetu kile ambacho Serikali imepanga kukifanya na jinsi ya
kutumia fursa, rasilimali, mipango na taratibu zilizopo za Serikali ili kuweza
kuboresha maisha yao.
10. Mheshimiwa Spika, napenda kuwaomba kwa mara
nyingine tena, wananchi wote kuendelea kudumisha amani na utulivu katika visiwa
vyetu na nchi yetu ya Tanzania kwa ujumla. Bila ya kuwepo Amani na Utulivu, hakuna
maendeleo. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kusimamia suala la
amani na utulivu kwa nguvu zake zote ili kutekeleza mipango yetu ya kujiletea
maendeleo zaidi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Hakuna haja tena ya kukumbusha mambo
yaliyopita, ila Serikali inatambua wapo baadhi ya wananchi wakorofi
wanaojihusisha na vitendo vya kuvuruga amani na utulivu uliopo.
Kwa mfano, wakati tukielekea katika uchaguzi wa
marejeo uliomalizika hivi karibuni, wakorofi hao walijihusisha kutega miripuko
inayosadikiwa kuwa mabomu na kuchoma moto mashamba ya mikarafuu, nyumba na
makaazi na maskani za CCM. Vyombo vya Dola vinaendelea na hatua za uchunguzi wa
matukio hayo na baadae kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria. Hakuna mtu atakayepona kuchukuliwa hatua kali
za kisheria ikiwa atabainika kutishia amani na utulivu tulionao.
11. Mheshimiwa Spika, tunasikitishwa na mambo
yanayotokea huko Pemba ambapo baadhi ya wafanya biashara kuwanyima wananchi
wenzao huduma za kibiashara kama vile kuwauzia bidhaa au kuwapa huduma za
usafiri kwa sababu za kiitikadi za kisiasa.
Jambo hili siyo zuri na ingefaa liachwe mara moja. Serikali inalifuatilia kwa karibu sana suala
hili na haitasita kumchukulia hatua mfanya biashara yoyote atakaye liendeleza
jambo hili ikiwa ni pamoja na kumfutia leseni yake.
12. Mheshimiwa Spika, kuhusu uchaguzi wa marejeo
uliofanyika tarehe 20 Machi, 2016, nachukua fursa hii kuipongeza Tume ya
Uchaguzi Zanzibar kwa kazi nzuri ya kusimamia na kufanikisha uchaguzi huo kwa
mafanikio makubwa. Uchaguzi huo ulikuwa huru na haki, na ulipelekea ushindi
mkubwa kwa Chama cha Mapinduzi kupitia kwa aliyekuwa mgombea wake, Dkt. Ali
Mohamed Shein, ambaye kwa sasa anaendelea kuiongoza nchi yetu akiwa ni Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kipindi cha pili cha miaka
mitano (2015 – 2020).
13. Mheshimiwa Spika, kwa vile uchaguzi umekwisha,
tunapaswa tuzidishe ushirikiano, mshikamano na umoja wetu katika kuijenga nchi
yetu. Kwa upande wetu Waheshimiwa Wawakilishi turudi Majimboni mwetu ili
tukashirikiane na wananchi kusukuma gurudumu hili la maendeleo. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwaomba
watumishi na watendaji wote wa Serikali watakaoteuliwa hapo baadae, kuwatumikia
wananchi wote bila ya kujali itikadi zao za kisiasa. Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inahimiza uwajibikaji zaidi na usimamizi mzuri wa fedha na rasilimali
nyengine za umma katika ngazi zote.
Wafanyakazi kujituma na siyo kufanya kazi kwa mazoea jambo ambalo Rais
wetu alilipigia kelele sana katika kipindi kizima cha kwanza. Na hata hotuba yake aliyoitoa wakati
akilizindua Baraza hili alisisitiza jambo hilo.
Nikimnukuu alisema:
“wapo baadhi ya watumishi
wenye tabia ya kutoroka kazini, kuchelewa na hawazijali kanuni ziliopo za
utumishi wa umma. Wao hujifanya wababe
mbele ya viongozi wao. Wafanyakazi wenye
sifa mbaya nilizozielezea katika kipindi hiki tutawachukulia hatua
watakapobainika na kama hapana budi tutawafukuza kazini. Hatuwezi kuwa na wafanyakazi waliokuwa hawana
nidhamu. Sasa basi, imetosha.
Waliopewa dhamana ya kuziongoza
Idara mbali mbali za Serikali watapaswa watekeleze wajibu kwa kuwasimamia
wafanyakazi walio chini yao. Pindi kama
hawatawawajibisha wafanyakazi wao, basi watawajibishwa wao. Lengo letu liwe kutoa huduma kwa wananchi,
kwani sote tunawajibika kwao; kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.”
14.
Mheshimiwa Spika, mimi najua ziko Idara na
Mashirika ya Umma ambayo hayako vizuri kiutendaji na ambayo yanalalamikiwa sana
na wananchi kwa sababu ya kutowajibika kwa watendaji wao. Nawaomba Watendaji watakaoteuliwa pamoja na
kazi zao za Maofisini, watenge muda kuzitembelea Taasisi zilizo chini yao ili waone
uwajibikaji wa viongozi wanaozisimamia Taasisi hizo. Naahidi kumsaidia Mheshimiwa Rais katika
kuyatumbua majipu yatakayojitokeza.
Nitamuomba Mhe. Rais aniunge mkono kwa uamuzi wowote nitakao uchukua
dhidi ya mtendaji yeyote ambaye ataonekana hawajibiki vipasavyo, kwa sababu ya
ama uvivu, uzembe, dharau au ubadhirifu.
Wako watendaji, Mhe. Spika, wanakatazia jambo la maendeleo kwa sababu ya
ubinafsi. Watendaji hawa nao hatutawavumilia.
15.
Mheshimiwa Spika, naamini siyo baada ya muda
mrefu Mheshimiwa Rais atateua Baraza lake la Mawaziri. Ni imani yangu kwamba tutashirikiana pamoja
na Watendaji watakao teuliwa ili kulisukuma gurudumu la maendeleo kwa manufaa
ya wananchi wetu. Natoa wito kwa
watakaoteuliwa kuwa Mawaziri nao wasikae maofisini tu, wakipepewa na mafeni na
viyoyozi, bali watenge siku waende vijijini wakaangalie wananchi wenye matatizo
na waone namna gani wataweza kuwasaidia.
Kila Waziri kwa eneo linalomhusu.
16.
Mheshimiwa Spika, migogoro ya ardhi imekuwa
changamoto kubwa kwa Serikali yetu katika kipindi kilichopita. Migogoro mingi imekuwa ikisababishwa na
baadhi yetu viongozi kwa sababu za kitamaa.
Kama hiyo haitoshi, baadhi ya wananchi wanaendesha ujenzi wa nyumba
kiholela bila ya vibali vya kujengea na wakati mwingine katika maeneo yasiyo
ruhusiwa kama vile kwenye maeneo ya vianzio vya maji na maeneo yaliyotengwa kwa
ajili ya ujenzi wa miji ya kisasa.
Tunawatahadharisha waliojenga katika maeneo hayo. Katika hotuba yake aliyoitoa wakati
akilizindua Baraza hili, Mheshimiwa Rais alilizungumzia sana suala hili. Niwakumbushe aliyosema, namnukuu:
“Napenda nitoe indhari kuwa
Serikali haitomvumilia kiongozi wa ngazi yoyote ambae atajijengea tamaa na
akajiingiza katika migogoro ya ardhi au akashindwa kutatua migogoro iliyopo
katika dhamana yake. Si siri kwani wapo
baadhi ya viongozi waliojiingiza katika matatizo ya ardhi na kusababisha mzozo
mkubwa kwenye jamii. Migogoro ya ardhi
ni kadhia ambayo tunataka tuimalize katika kipindi hiki cha miaka mitano
ijayo. Kwa hivyo, nawatahadharisha
viongozi watakaopewa dhamana ya kushughulikia masuala ya ardhi wayazingatie
maelezo yangu haya.”
17.
Mheshimiwa Spika, mnamo siku za hivi karibuni
kumekuwepo na upandaji wa bei za bidhaa bila ya sababu za msingi. Serikali inalifuatilia suala hili kwa karibu
sana, na atakaye gundulika kupandisha bei kiholela atafungiwa leseni yake ya
kuendeshea biashara mara moja.
18. Mheshimiwa Spika, ninachukua nafasi hii kutoa
wito maalum kwa Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kushirikiana na
wananchi katika kuendeleza usafi wa mazingira na kutekeleza maelekezo yote ya
Wataalamu wa afya ili kujikinga na maradhi ya miripuko kikiwemo Kipindupindu
kwani ugonjwa huo bado upo, na namna moja ya kuuepuka ni kuweka mazingira yetu
katika hali ya usafi.
Pia, ninaomba niwakumbushe Waheshimiwa
Wawakilishi na wananchi tuzitumie vizuri mvua zinazoendelea nchini kwa
kuendeleza shughuli za kilimo cha mazao ya chakula na biashara kwa lengo la
kupata mavuno mengi zaidi na kujiongezea kipato. Sambamba na hayo, Serikali
inaendelea kuwataka wananchi wanaoishi sehemu za mabondeni waendelee kuchukua
hadhari wakati huu wa mvua zinazoendelea ili tuweze kuepuka athari na majanga
yasiyo ya lazima. Tunawasihi wananchi
hao wahame kutoka mabondeni humo na kuhamia sehemu za juu ili kuepuka uharibifu
wa mali zao na hata upotevu wa maisha yao.
19. Mheshimiwa Spika, mwisho, ingawa si kwa
umuhimu, napenda kumshukuru sana Spika wetu Mstaafu, Mhe. Pandu Ameir Kificho
kwa kuliongoza Baraza hili kwa umahiri mkubwa kwa mudakwa miaka 20
mfululizo. Mhe. Kificho aliliongoza
Baraza hili kwa hekima, busara na uvumilivu mkubwa. Ninamtakia kila la kheri na mafanikio mema
katika shughuli zake za baadae.
Lakini pia niwashukuru Mhe. Ali Abdulla Ali,
Naibu Spika Mstaafu, Waheshimiwa Mgeni Hassan Juma na Mahmoud Mohamed Mussa
ambao walikuwa Wenyeviti wa Baraza hili.
Ni dhahiri kuwa wote walituongoza vizuri katika kipindi chote cha miaka
5 iliyopita. Nao nawatakia kila la kheri
na mafanikio mema.
20. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru wote
waliotuwezesha kukamilisha shughuli zilizopangwa kwenye Mkutano huu wa Kwanza
wa Baraza la Tisa la Wawakilishi kwa ufanisi mkubwa. Pongezi hizo zaidi
ziwafikie watendaji wote wa Baraza hili la Wawakilishi wakiongozwa na Katibu,
Dkt. Yahya Khamis Hamad. Ni ukweli
usiofichika kwamba tumeanza vizuri na ninaamini tutaendelea vizuri. Mungu libariki Baraza hili, Zanzibar na
Tanzania kwa ujumla. Lakini pia
niwapongeze wakalimani wetu wa lugha ya alama ambao wamewawezesha Waheshimiwa
Wawakilishi wenye ulemavu wa kusikia kufuatilia yote yaliyokuwa yakiendelea
ndani ya Baraza. Pia nawashukuru
wanahabari kwa kufanya kazi ya kuwahabarisha wananchi wetu yale yaliyokuwa
yakiendelea Barazani hapa.
21. Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila
kama sitawashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Mahonda kwa imani kubwa walionipa
kwa kunichagua kuwa Mwakilishi wao.
Nawaahidi kuwa nitawapa utumishi ulio bora na kutekeleza ahadi zote
nilizozitoa wakati wa Kampeni. Nawaomba
wanipe ushirikiano wao ili tuweze kuendeleza Jimbo letu na kujiletea maendeleo.
22. Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia niwatakie
Waheshimiwa Wawakilishi kila la kheri na mafanikio mema katika kuwatumikia
wananchi wao Majimboni mwao. Aidha,
nawatakia safari njema na ya salama ya kurudi Majimboni mwao, na hasa
Wawakilishi wenzetu kutoka Pemba kwa sababu wao wana safari ndefu zaidi kuliko
wenzao wa Unguja.
23. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo,
naomba sasa kutoa hoja kwamba Baraza lako Tukufu liahirishwe hadi siku ya
Jumatano tarehe 18 Mei, 2016, saa 3.00 barabara za asubuhi.
24. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment