Je, Falsafa ya Kuanzishwa kwa Mbio za Mwenge wakati wa Uhuru wa Tanganyika tarehe 9/12/1961 imepitwa na wakati??? Je, kuna wakati utafika misingi ambayo taifa hili lilijengwa kwahiyo, itapitwa na wakati? Je, tuachane na mbio za Mwenge kwa sababu za gharama kuwa kubwa - wengine wanasema mwenge ni Jipu na Rais Magufuli alitumbue? Au Mbio za Mwenge zina umuhimu na ni sehemu ya msingi ambao taifa hili lilianzishwa na ni kumbukumbu ya mapambano ya kumletea mabadiliko na maaendeleo Mtanzania? Yote haya nitayatolea ufafanuzi kwenye Penyenye Fupi Fupi.
Falsafa ya Mwalimu Julis Kambarage Nyerere kuhusu mwenge wa Uhuru ilikuwa ni: “Sisi Watanganyika, tunataka kuuwasha Mwenge na kuuweka juu ya mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo pale ambapo pana chuki, heshima ambapo pamejaa dharau”.
Je, Falsafa ya Kuanzishwa kwa Mbio za Mwenge wakati wa Uhuru wa Tanganyika tarehe 9/12/1961 imepitwa na wakati??? Ikumbukwe kwamba falsafa hii ni sehemu ya misingi ya Taifa letu..tangu ilipoanzishwa na waasisi wetu. Mataifa yaliyoendelea yameendelea kuenzi misingi iliyojenga Mataifa hayo kwa gharama zozote zile. Tutakubaliana sote kuwa Watanzania bado tunahitaji kujikwamua kutoka kwenye ujinga, maradhi, na umaskini. Tunahitaji kujikwamua kutoka kwenye dhuruma na chuki ambazo, ukizingatia dhana ya mazingira na wakati, zimekuwa ni tofauti zaidi ukilinganisha na wakati wa Uhuru. Japokuwa wakati wa Uhuru kulikuwa na dhuruma, ufisadi, chuki nakadharika, bado hata sasa hivi tuna ufisadi, dhuruma na chuki tena zilizoenda mbali sana. Katika dhama hizi za Magufuli, zilizotofauti kabisa na nyakati za Kikwete, Mkapa, Mwinyi na zile za wakati wa Baba wa Taifa. Tumejionea uozo wa hali ya juu kuliko ambavyo tumewahi kushuhudia. Neno hili siyo geni tena kwetu – “Tanzania ilikuwa ni shamba la bibi”. Mwenge wa Uhuru unapaswa kutukumbusha kila mara kuwa vita dhidi ya ubadhirifu, chuki, na dharau bado inaendelea. Tena falsafa ya Mwalimu ilikuwa inataka huu Mwenge umulike hadi nje ya mipaka yetu. Hii inanipeleka kwenye penyenye yangu inayofuata – Kuingiliwa kwa Uhuru wa Taifa letu na Mataifa ya Magharibi.
Tutakumbuka kuwa hivi karibuni sakata la MCC 2 lilishika kurasa nyingi sana. Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Marudio wa Zanzibar na kuhusiana na ile sharia ya makosa ya Kimtandao. Taasisi ya MCC ni kibaraka wa umagharibi, pia ina kila lengo la kuingilia mambo ya ndani ya nchi yetu. Maitaifa ya Magharibi kuingilia mambo ya ndani ya nchi za kiafrika limekuwa ni jambo la kawaida sana. Tumekuwa ni nchi ya amani isiyokiuka haki za binadamu, sasa kuiingiliwa kwenye mambo ya ndani ya nchi ni jambo linakiuka hadhi yetu ya kuwa Sovereign State. Mwenge wa Uhuru unatukumbusha maneno ya Mwalimu Julius Nyerere kuwa “… tunataka kuuwasha Mwenge na kuuweka juu yam lima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu...” Je msingi huu wa kuanzishwa kwa Taifa letu umepitwa na wakati, hasha.. msingi huu bado uko na unaendelea. Na kama taifa lazima tusimame kidete. Mwenge huu inabidi tuumulike ili sisi kama Watanzania tujikumbushe, na hayo mataifa ya nje yaliyo karibu nasi na yaliyo Magharibi au Mashariki. Pia ninaungana na kauli ya Mh. Rais Dk. John Joseph Magufuli kuwa ni bora kuishi kwa kula mihogo kuliko kula mkate ya masimango.
Je, kuna wakati utafika misingi ambayo taifa hili lilijengwa kwayo, itapitwa na wakati?
Mwalimu Julius Nyerere, alipohutubia Watanganyika kwa mara ya kwanza kama Waziri Mkuu wa Tanganyika, alielekeza kuwa Tanganyika iko vitani dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini. Ni nukuu baadhi ya maneno yake: “…matatizo haya, hayanitishi mimi, hayawatishi wenzangu, na wala hatuombi kwamba yawatisheni ninyi. Tunayaona kwamba ni jaribio tu…Mara nyingi sana, nimesema nayi juu ya umaskini, ujinga, na maradhi, lakini kwa kweli adui yetu mkubwa ni umaskini. Tukiweza kumshinda adui huyu, tutakuwa tumeweza kupata silaha itakayotuwezesha kuushinda ujinga na maradhi. …tunaweza kupigana vita vya umaskini. Namuomba kila raia wa Tanganyika, aape kiapo cha kuwa adui wa umaskini. Amshambulie adui huyo mahali popote atakapoonekana.”
Japokuwa Tanganyika ilipata Uhuru wake bila mapambano dhidi ya mkoloni yaliyohusisha kumwaga damu. Msingi tuliachiwa na Baba wa Taifa ni kuwa nchi iko kwenye mapambano dhidi ya umaskini. Kila Mtanzania anapaswa kuwa vitani wakati wowote. Nikiiweka hoja hii kwenye muktadha wa Mwenge wa Uhuru ambao unajengwa kwenye msingi wa kumulika ubadhirifu na dhuruma. Tumeshuhudia ambavyo viongozi au watumishi wetu katika kada mbalimbali wakiwa mstari wa mbele kwenye ubadhirifu wa mali za umma. Kuingia mikataba isiyokuwa na tija wala maslahi ya Taifa. Watu hawa wamekuwa wakiturudisha nyuma sana kwenye vita dhidi ya umaskini ambao mwalimu alitutaka kila Mtanzania kuapa kupambana nao kila sehemu atakapoukuta. Ila katika juhudi za Mtanzania maskini kujitafutia njia za kutoka kwenye umaskini na wengine kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi, wachumia tumbo wamekuwa na mtindo wa kujinufaisha wao na vizazi vyao. Kinyume kabisa na misingi ya Taifa letu. Kila Mtanzania akiwa vitani dhidi ya umaskini inamaanisha kuwa atafanya kazi kwa bidii ili kujipatia kipato na serikali itatimiza wajibu wake kuwaletea wananchi bidhaa za umma. Ndiyo maana katika dhama hizi za Magufuli utumbuaji wa majipu unaturudisha kwenye ile vita dhidi ya dhuruma, ufisadi, na uonevu. Mwenge lazima uendelee kumulika, falsafa na itikadi ya kuwa tuko katika mapambano lazima iendelee kumulikwa.
Je, tuachane na mbio za Mwenge kwa sababu za gharama kuwa kubwa - wengine wanasema mwenge ni Jipu na Rais Magufuli alitumbue? Au Mbio za Mwenge zina umumhimu na ni sehemu ya msingi ambao taifa hili lilianzishwa kwayo na ni kumbukumbu ya mapambano ya kumletea mabadiliko na maaendeleo Mtanzania?
Kama nilivyelezea hapo juu nia, falsafa na matokeo ya kuwepo kwa mbio za Mwenge wa Uhuru bado hazijabadilika. Changamoto ambazo zilikuwepo wakati wa Uhuru wa Tanganyika, bado zipo katika kipindi cha Tanzania ya karne ya 21, na inawezekana Tanzania ya vizazi vijavyo itakutana na changamoto zinazofanana na hizi lakini kadika mazingira na wakati wa vizazi vya wakati huo.
Kama Taifa misingi ya kuanzishwa kwa Taifa lazima iendelezwe, kwani wanaosema kuachana na misingi hiyo huwezi fahamu ajenda yao iliyojificha ni mimi. Taifa lisilo na misingi ya kuanzilishwa kwake ni dhaifu. Taifa linaloweza kutupilia mbali misingi ya kuanzilishwa kwake, linaweza kuwa katika hatari kubwa sana ya siku moja kutoweka, au kuingia katika virugu na matatizo ambayo ni vigumu kuweza kurudi katika hali ya awali. Bado tunaihitaji misingi ya Taifa letu. Bado tunaipenda misingi ya Taifa letu. Gharama ya mbio za Mwenge siyo hoja, maana misingi ya kuanzishwa kwa Taifa lazima ilindwe kwa gharama zozote zile. Ufisadi uliokuwa unaendana na kukimbiza mbio za Mwenge wa Uhuru ndiyo unaotakiwa kupigwa vita kwa juhudi zote. Mwenge kwa sababu unamulika na kuangaza palipo na ufisadi, udharimu, dharau, na chuki. Mbio za Mwenge wa Uhuru zitumike kutumbulia kila linapokuwa limemulikwa jipu, kwenye miradi ambayo imekuwa ni utamaduni kutumika kuizindua nchi nzima yaani mikoa 31 na Halimashauri 173.
Kumbukumbu ya kumletea Mtanzania mabadiliko ya kiuongozi na uundwaji wa mfumo wa utawala bora utakao ridhishwa kizazi hadi kizazi, ni jambo linalopaswa kuwa sehemu ya ujivuni wa kuwa na Mwenge wa Uhuru. Mwenge ni alama ya Uhuru wetu kuona mapungufu yetu. Mwenge ni alama ya kutuunganisha Watanzania na kupambana na uovu, udharimu, wizi, na ufisadi. Mwengi ni alama ya Uzalendo na kila Mtanzania nia akiuona anapaswa kuukumbuka wakati wa uhai wake wote, na kuwafundisha watoto na watoto wa watoto wake kuwa hiyo ndiyo ishara ya Uzalendo wa Mtanzania. Ndiyo ishara la tumaini la Mtanzania lilioanza tangu na kabla baada ya kupata Uhuru na lilikuwepo kabla ya kupata Uhuru. Wanaoupiga vita Mwenge wa Uhuru wamepoteza tumaini na wanataka Watanzania nia pia wapoteze tumaini pamoja nao. Ninachoamini mimi ni kuwa mtu aliyepoteza tumaini safari yake inapaswa kuishia kaburini. Tena kwa sisi tuliona tumaini la kizazi hiki na kutambua ukuu wa Mungu, tunaamini hata baada ya Kaburi tunatumaini kuwa siku moja tunauna uso wake. Sasa iweze sisi Watanzania tukubali mawazo haya finyu kuwa Mwenge ni Jipu, ninadhani kupoteza Tumaini ni Jipu, na dawa ya jipu ni kulitumbua na Mwenge unamwangaza kwa kutosha kumulika wakati wa Utumbuaji wa Jipu hilo.
Mnyela Jonathan N.
1 comment:
Yaa hiyo ni kweli kabisa mwenge utumike kutumbulia majipu kwani uzunguka nchinzima na kabla haujatoka katika mkoa mwenge uhakikishe kama kunajipu lazima litumbuliwe awe mkuu wa mkoa awe waziri na viongozi wengine wanaofuata ili tuweze kushinda vita zidi ya umasikini the itakuwa raisi kuondoa umasikini na maradhi kama alivyosema Mwl jk Nyerere (Baba wa Taifa) wakati wa kuwashwa Mwenge wa Uhuru!!!; mdau kutoka Canada
Post a Comment