Sunday, April 17, 2016

Cybercrimes Act: Hoja au vioja vya Wamarekani?

Na Mwandishi Wetu, Addis Ababa

“KAMA kuna jambo ambalo katika maisha yangu lilinishangaza, basi ni kufanyakazi na Wamarekani. Katika ile MCC ya awamu ya kwanza kila siku walikuwa ‘wakihamisha goli’ tusipate fedha ambazo wao wenyewe walishaziidhinisha. Kwa kweli fedha zile zilikuwa na siasa nyingine kabisa,”
Hiyo ni kauli ya rafiki yangu mmoja kutoka moja ya nchi zilizowahi kupata kufaidika na fedha za awali za MCC akionesha machungu na jakamoyo alilonalo dhidi ya siasa za vioja za Wamarekani.
Kwa hakika kutokana na majukumu ya hapa na pale sikupata fursa ya kushiriki katika mjadala huu kwa wakati. Lakini wiki iliyopita baada ya majadiliano marefu na rafiki yangu huyu nimeshawishika kufanya utafiti kidogo kujiridhisha hasa pale anaposema fedha za MCC ni “siasa nyingine kabisa.”
Katika kuyaandika haya nimelazimika kutumia muda mrefu kusoma na kutafakari wachambuzi wengi walivyolichambua suala la Tanzania kukosa misaada ya awamu ya pili chini ya ufadhili wa MCC baada ya kufuzu ile awamu ya awali.
Nimeona wapo walioendekeza kile ambacho mara kadhaa humu nimekieleza kama tabia ya Watanzania kupenda kulialia. Kundi hili limejumuisha wachambuzi wanaoamini kuwa Tanzania haiwezi kwenda bila misaada ya nje.
Wapo wachambuzi wengine walioona changamoto ya kunyimwa misaada iwe chachu ya sisi kujitegemea kwa sababu hakuna nchi duniani iliyopata kusonga mbele kwa kupewa misaada na mataifa mengine.
Hawa waliukubali ukweli kwamba kwanza katika MCC hatukuomba: waliweka vigezo, wakatupima na tukaikubali misaada yao tulipofuzu na ni kweli kwamba tunahitaji misaada lakini isiwe sababu ya kupangiwa mambo yetu ya ndani.
Nimetafakari pande zote hizo mbili: nimeamua kupita katikati yao. Swali langu kuu la kitafiti ni Je, sababu zilizoainishwa na  Wamarekani katika kuiondoa Tanzania katika MCC-2 zina hoja au ni vihoja tu?
Zimetajwa sababu kuu mbili: suala la mgogoro wa Zanzibar na Sheria ya Makosa ya Uhalifu Mtandaoni (Cybercrimes Act). Hizi ndizo sababu kuu mbili kadiri ya taarifa yao rasmi.
Nimeamua kujadili zaidi hilo la pili kwa sababu kwangu mimi suala la changamoto za kisiasa visiwani Zanzibar ninamtazamo tofauti kabisa na Wamarekani hasa ninapochunguza mwenendo wao katika kuua demokrasia duniani na kuchochea vurugu-hivyo tuliweke hili kiporo kwa kuwa wao wenyewe hawana “moral authority.”
Juu ya Wamarekani kuitaja Sheria ya Uhalifu Mitandaoni kuwa moja ya sababu za kuzuia msaada wao niseme tu binafsi nilistushwa sana na hili lakini juzi ndipo nimelielewa kuwa ni mwendelezo ule ule wa “kuhamisha goli.” Zipo hoja nyingi.Tupitie chache tu kwa leo.
                                         Tanzania haikukurupuka
Kutungwa kwa Cybercrimes Act, Serikali ya Tanzania haikukurupuka. Nijuavyo na kwa uzoefu wangu, ni watanzania wenyewe ambao kutokana na mwingiliano  katika matumizi ya teknolojia za mawasiliano katika mtandao walijikuta wakipata madhila mbalimbali.
Wapo ambao wamedhalilishwa mitandaoni, wapo ambao wametishiwa maisha mitandaoni, wapo ambao wametapeliwa mitandaoni na kipo kizazi ambacho kimekuwa kikioneshwa picha mbaya za utupu mitandaoni. Wamarekani walitaka  haya yaendelee?
Hali ya makosa na uhalifu wa mitandaoni nchini Tanzania ilifikia kiwango kibaya sana ambapo takwimu zinaonesha kuwa kufikia mwaka 2013 zaidi ya kesi 400 za uhalifu mbalimbali wa mitandaoni zilikuwa zimeripotiwa katika kitengo cha polisi.
Ni ajabu kwamba Taifa linalopenda kuwalinda raia wake kama Marekani halioni hoja wala haja ya Tanzania kuwalinda watu wake dhidi ya uhalifu huu na badala yake kugeuka kabisa na kuifanya sheria inayolenga kusaidia raia kuwa ni kama vile ni kitu kibaya sana kisichopaswa hata kutajwa jina.
  
                                          Mbona wao ni yale yale?
Kama nilivyosema awali katika mijadala kuhusu uamuzi wa Marekani kupitia MCC kuamua kuondoa msaada wao sijaona wachambuzi wetu wakizama zaidi kuzitazama kwa kina sababu zilizotolewa.
Binafsi nimeisoma na kuisoma sheria hii. Nimesoma pia maoni ya wachambuzi wengi wakiwemo wataalam wa taasisi ya ‘Article 19’ yenye makazi yake jijini London, Uingereza.
Niseme wazi nimefika hatua ya kutoshangazwa na uamuzi huo wa Wamarekani. Kama nilivyoainisha hapo awali kutungwa kwa sheria hii kumekuja wakati ambapo Watanzania wengi wakiwa wameshaumizwa sana na uhalifu wa mitandaoni na kulikuwa hakuna namna ya kupata haki au kuzuia vitendo hivyo.
Ukiisoma sheria ya Cybercrimes utaona inavyowabana wanaojaribu kutumia majina ya watu wengine kufanya uhalifu, inazuia watu kuiba taarifa za watu wengine kimtandao, inazuia mtu kuingia kwa jinai katika mawasiliano ya mtu mwingine kimtandao, inazuia na kukinga jamii dhidi ya picha za ngono.
Sheria hiyo inakwenda mbali zaidi kwa kiwango cha kuzuia watu kuingiliwa faragha yao au watu kueneza uongozo na uzushi mitandaoni unaolenga kuingilia faragha (privacy), kushusha heshima (defamation) au kuchonganisha watu na kuibua uhasama (hatred). Haya yote Wamarekani hawataki!
Kama kuna kitu nitamshukuru rafiki yangu niliyemnukuu hapo juu ni ile kauli yake ya kwamba jambo hili lina “siasa nyingine kabisa,” kwa sababu sasa nimeelewa.
Nasema hivi kwa sababu sheria hiyo inaweza kuwa na mapungufu yake kama ilivyo kwa sheria nyingine na mahitaji yakiongezeka inaweza kubadilishwa kukidhi matakwa ya wakati huo ya kijamii.
Lakini kukurupuka tu na kila mtu kwa sababu zake akajiona anaweza akasimama kudai inakwaza au kuzuia haki za watu kwa kiwango cha Tanzania kunyimwa msaada ni hila iliyo wazi.
Kwa wasiofahamu na wanaounga mkono tu kwa kufuata mkumbo huu msimamo tata wa Wamarekani, wajue kupitia ukurasa huu ya kwamba sehemu kubwa ya makosa yaliyoainishwa katika Cybercrimes Act ya Tanzania yapo pia katika sheria kama hizo katika nchi mbalimbali ikiwemo Marekani yenyewe.
Ukifungua hii anuani ya mtandao hapa https://www.oas.org/juridico/spanish/us_cyb_laws.pdf utapata fursa ya kuona muhtasari wa sheria ya makosa ya mtandaoni ya Marekani ambayo kwa sehemu kubwa mambo iliyoyakataza ni kama yale ya Tanzania.
Pia sehemu ya sheria hiyo utaisoma katika http://www.cybercrimelaw.net/US.html ikiainisha makosa mengine mbalimbali ya katika mtandao na kompyuta.
Marekani pia mwaka 1996 ilitunga sheria iitwayo Communication Decency Act inayoainisha namna mawakala au wasambazaji mbalimbali wa taarifa za kimtandao (Internet Service Providers) wanavyolindwa au kuwajibikaji yanapokuja makosa ya kimtandao.
Katika tasnifu yake kwa ajili ya shahada ya uzamivu (PhD) msomi mmoja aitwaye Park (2015) ameichambua sheri hiyo ya Marekani akilinganisha na ile ya Uingereza ambapo amebaini Wamarekani wamewalinda zaidi wananchi wao kuliko ambavyo Waingereza wamefanya kuhusu uhalifu wa mitandaoni.
Kwa kifupi Marekani imewalinda raia wake sana tu kutokana na makosa ya kimtandao kuliko mtu anavyoweza kudhani. Haishangazi Marekani hiyo hiyo “inapopanic” kuona Tanzania inalinda raia wake kwa sababu sasa ni dhahiri katika haya mambo kuna “siasa nyingine kabisa.”
Ni kwa sababu hii basi naungana na wale wanaodhani njia pekee ya kuepukana na hizi siasa na vioja katika hoja ni kuenenda njia ya kujitegemea. Hii ni njia ngumu lakini ambayo hatuna budi kuipita ili tufike kuleee tunakokuwaza kila uchao.
Kwa leo alamsiki.  
*Mwandishi wa makala haya ni Mtanzania anayeishi jijini Addis Ababa, Ethiopia na ni mtaalamu katika masuala mbalimbali ya maendeleo.  






No comments: