Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. James Jesse akitoa mada mbele ya
waandishi wa habari kuhusu Mpango wa Kimataifa wa Kujitathmini juu ya
Masuala ya Haki za Binadamu (UPR) wakati wa warsha ya siku moja 29
Aprili 2016 Mkoani Morogoro.
Afisa
Utetezi na Haki za Binadamu wa Shirika la Under The Same Sun (UTSS) Bi.
Perpetua Senkoro akitoa mada kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu
kupewa haki zao wakati warsha ya siku moja kuhusu Mpango
wa Kimataifa wa Kujitathmini juu ya Masuala ya Haki za Binadamu (UPR)
wakati wa warsha ya siku moja 29 Aprili 2016 Mkoani Morogoro.
Wadau
wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wakiwa katika picha ya
pamoja na Waaandishi wa Habari waliohudhuria mafunzo ya siku moja ya
warsha kuhusu Mpango
wa Kimataifa wa Kujitathmini juu ya Masuala ya Haki za Binadamu (UPR)
wakati wa warsha ya siku moja 29 Aprili 2016 Mkoani Morogoro.
(Picha zote na Benedict Liwenga)
Na Benedict Liwenga.
Asasi za Kiraia
pamoja na Taasisi za kutetea haki za binadamu nchini zimewaasa Waandishi wa
Habari nchini kujikita katika kuhabarisha umma kuhusiana na masuala ya haki za
binadamu ikiwemo mauaji ya watu wenye ualbino, mauaji ya vikongwe, ukatili dhidi
ya watoto, pamoja na adhabu ya vifo.
Rai hiyo imetolewa
leo na Kamishna wa Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bi. Salma Ally Hassan
wakati wa Warsha ya siku moja iliyofanyika mkoani Morogoro yenye lengo la kuwajengea
uelewa Wanahabri kuhusu Mpango wa Kimataifa wa kujitathmini juu ya Masuala ya
Haki za Binadamu (UPR).
Bi. Salma ameeleza
kuwa kutokana na tathmini ya masuala ya haki za binadamu nchini, vyombo vya
habari havinabudi kuwa na uelewa mkubwa kuhusu umuhimu wa kuziongelea haki za
binadamu kwani jamii imekuwa haizitambui baadhi ya haki hizo na kumekuwepo na kukithiri
kwa vitendo vya uvunjifu wa amani yakiwemo matukio ya mauaji ya watu wenye
ualbino, vikongwe pamoja na ukatili kwa watoto.
Ameongeza kuwa,
baadhi ya watu nchini wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi kwa kuua watu ambapo
watu wenye kuyasemea hayo ni Vyombo vya Habari lengo likiwa ni kukemea
kuendelea kwa vitendo hivyo.
“Uvunjaji wa haki za
binadamu unafanywa na watu katika jamii, kwa mfano, mauaji ya Watu wenye Ualbino,
mauaji ya vikongwe, pale sio Serikali inakua imevunja haki za binadamu, bali ni
watu katika jamii”, alisema Bi. Salma.
Kwa upande wake
Mshauri wa masuala ya haki za binadamu kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini
Tanzania, Bi. Chitralekha Massey ameeleza kuwa, ni vema Tanzania ikakubalina na
mapendekezo yanayohusiana na masuala ya haki za binadamu yanayoendana na Dunia
kwa ajili ya ulinzi wa haki hizo.
“Sisi kama Umoja wa
Mataifa tunapenda kuona Tanzania inafanya uamuzi utakaosaidia kuboreshwa kwa haki
za binadamu nchini kwani ni wakati sasa wa jamii kusema kwa uwazi kuwa
mapendekezo hayo yatakuwa yenye manufaa kwao”, alisema Massey.
Aidha, katika warsha
hiyo, vyombo vya habari, jamii pamoja na Serikali wanajukumu la kulinda haki za
binadamu na kuendelea kukemea matukio yanayovunja amani katika jamii.
Tarehe 9 Mei, 2016 Tanzania
inatarajiwa kufanyiwa tathmini ya pili juu ya hali ya haki za binadamu nchini
na Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa ambapo tayari Asasi za Kiraia na Watetezi
wa haki za binadamu wamekwisha wasilisha mapendekezo yao kwa Wawakilishi wa nchi
wanachama wa umoja huo.
|
No comments:
Post a Comment