Katibu wa kamati maalum ya NEC, idara ya itikadi na uenezi CCM Zanzibar Bi, Waride Bakar Jabu akimkabidhi misaada Katibu mkuu wa ofisi ya makamo wa pili wa rais, Joseph Abdallah Meza kwa ajili ya kuwasaidia wahanga wa mafuriko waliopo kambi ya mwanakwere "C" Unguja.
Katibu wa kamati maalum ya NEC, idara ya itikadi na uenezi CCM Zanzibar Bi, Waride Bakar Jabu akikagua wahanga wa mafuriko katika kambi ya mwanakwere zanzibar.
Kambi ya kipindupindu iliyopo chumbuni Zanzibar.
CHAMA chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka wananchi kuendelea kufuata kanuni na taratibu zinazotolewa na wataalamu wa kiafya ili kujikinga na maambukizi ya maradhi ya kipindupindu yaliyopo nchini.
Wito huo umetolewa na Katibu wa Kamati Maalum NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Waride Bakar Jabu katika ziara ya kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa wa Kipindupindu wa kambi iliyopo Chumbuni Zanzibar, alisema endapo wananchi watafuata kanuni za kiafya itasaidia kutoweka ugonjwa huo kwa haraka.
Waride alisema CCM itaendelea kutoa misaada ya hali na mali kwa wagonjwa wa kipindupindu ili kusaidia serikali huduma za uendeshaji kwa wagonjwa hao.
“ Tunawaomba wananchi waendelee kuweka mazingira yao katika hali ya usafi sambamba na kutumia maji salama, vyoo kuwa visafi na wagonjwa wenye dalili za maradhi hayo kupelekwa haraka katika kambi za kipindupindu.
Pia CCM inawapa pole wananchi wote waliopata maradhi ya kipindupindu na kuwasihi waendelee kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha matibabu yao.”, alisema Bi, Waride na kuzisihi taasisi zingine za serikali na binafsi kutoa misaada kwa wagonjwa hao kwani maradhi ya Kipindupindu hayana itikadi za kisiasa bali yanawapata wananchi wote.
Aliwashauri wanawake nchini ambao ni walezi wa watoto na mama wa nyumbani kuacha tabia ya kutupa ovyo pempasi za kuwafungia watoto kwani nazo ni miongoni mwa vitu vinavyopelekea kuenea kwa maradhi ya kipindupindu nchini.
“ Wanawake tukumbuke kuwa kila janga lolote sisi pamoja na watoto ndiyo waathirika wa mwanzo hivyo lazima tuwe makini katika kuweka mazingira yetu katika hali ya usafi pia tusitupe pempasi ovyo bali tuziweke katika sehemu zinazostahiki.” Alisisitiza Waride.
Naye Daktari dhamana wa Wilaya ya Magharibi Unguja ambaye pia ni Mkuu wa Kambi ya Kipindupindu Chumbuni Zanzibar, Ramadhan Mickdad Suleiman ameshukru msaada uliotolewa na CCM na kuahidi kuutumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Akitoa takwimu za hali ya maambukizo ya ugonjwa huo kwa sasa, Mickdad alisema ya hali ya maambukizo kwa sasa imepungua kutoka wagonjwa 40 kwa siku hadi 21 wanaolazwa katika kambi hiyo.
Alisema hali hiyo imetokana na utekelezaji wa agizo la Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein alipowaagiza wananchi wanaofanya biashara za vyakula na vinywaji kuacha kuuza kwa muda ili kudhibiti kupunguza kasi ya maambukizi ya kipindupindu.
Alifafanua kuwa mpaka sasa kambi hiyo tayari imeshapokea wagonjwa 2026 waliopatiwa matibabu na kupona na wakaondoka na kati ya hao wamefariki wagonjwa 43 mpaka sasa.
“ Tunaishauri jamii kudumisha usafi wa vyoo na kula vyakula na maji vilivyokuwa salama kwani ugonjwa huu unaambukizwa kwa kasi katika maji ya kunywa yenye bakteria wa kipindupindu ama kumgusa maiti yaliyekufa kwa ugonjwa au kugusana na mtu aliyeambukizwa kipindupindu.”, alisema Bi, Micjdad.
Aliwaomba wananchi wenye uwezo pamoja taasisi binafsi na serikali kutoa misaada kujitokeza kutoa misaada mbali mbali ya kuwasaidia wagonjwa wa maradhi hayo waliopo katika kambi hiyo.
Mapema Waride alitembelea na kuwafariji Wahanga wa mafuriko waliopo katika kambi ya Shule ya Mwanakwerekwe “ C” Unguja, aliwapa pole kwa matatizo yaliyowafika na kuwaomba waendelee kuwa wavumilivu katika kambi hili huku serikali ikiendelea kutafuta mbinu za kuwasaidia ili wapate makaazi katika sehemu salama.
Alitoa wito kwa wananchi wanaoishi katika sehemu za mabonde na sinazojaa maji wakati wa msimu wa mvua za maska kuhama haraka kabla hawajapata athari za kukumbwa na mafuriko hayo.
Kwa upande wake Katibu mkuu wa Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar, Joseph Abdallah Meza alitoa shukrani kwa uongozi wa CCM kwa msaada wao wa kuisaidia kambi hiyo yenye wananchi zaidi 400.
Alisema serikali bado inaendelea kuwahudumia wananchi hao ambao wamepata maafa ya mafuriko na kupoteza makaazi yao hivyo bado panahitajika misaada mbali mbali ya maji na vyakula pamoja na huduma za kibinadamu.
Misaada iliyotolewa na CCM katika ziara hiyo ina thamani zaidi ya shilingi milioni tano (5) kwa upande wa kambi ya kipindupindu Chumbuni ni pamoja na Maji ya kunywa, Dawa za Chroline, Sabuni za kufulia na kuogea, viatu vya mvua, dawa ya choo na mashine za kufukizia dawa Sprayers.
Vingine vilivyotolewa katika kambi ya wahanga wa mafuriko iliyopo Mwanakwere “C” ni pamoja na Pempasi za watoto, maji ya kunywa, sabuni za kuogea na kufulia, sabuni za chooni na madaftari ya wanafunzi.
No comments:
Post a Comment