Friday, April 29, 2016

BOMBA LA MAFUTA KUTOKA UGANDA HADI TANGA KUKAMILIKA 2020 - PROF. MUHONGO

Chalila Kibuda, Globu ya Jamii

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga  litakuwa limekamilka kufikia 2020 hivyo kilichobaki ni kuanza utekelezaji wa kuanza kujenga bomba hilo.

Profesa Muhongo ameyasema hayo  leo jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na waandishi wa habari  juu ya mikakati walioweka katika kutekeleza ujenzi wa bomba hilo, amesema kuwa wataalam katika sekta mbalimbali kutoka Uganda na Tanzania wamekutana leo jijini Dar es Salaam kuweza kuweka mikakati hiyo ya kuanza kutekeleza bomba hilo.

Muhongo amesema kuwa  kutokana na maagizo  ya Rais Dk.John Pombe Magufuli na Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Mseveni  ya  mradi wa bomba la mafuta watendaji kazi yao ni kuanza kufanya utekelezaji na wataweza kumaliza kabla ya mwaka huo baada ya kupata muongozo wa wataalam wataowasilisha Mei 26  Oima nchini Uganda.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akielezea uzoefu wa Tanzania kwenye ujenzi wa miradi ya mabomba ya gesi na mafuta katika mkutano huo. Kushoto ni Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini Nchini Uganda, Mhandisi Irene Muloni na kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa.

Waziri huyo amesema kuwa Uganda imetoa asilimia 40 kwa nchi Jumuiya ya Afrika Mashariki kuweza kununua hisa hizo ili kuwa na sehemu ya kunufaika na bomba hilo ikiwa hisa hizo zinauzwa kwa Dola za Kimarekani Bilioni 4.7.

 Amesema kuwa kwa nchi makini haiwezi kuacha kununua hisa hizo kutokana na faida ya mradi huo na  nchi itakayoacha kununua hisa hizo sio makini.

Amesema bomba hilo lina umuhimu kwa kujengwa nchini ambapo Tanzania itaweza katika kujenga bomba la gesi kwenda uganda kutokana na uhitaji wa Waganda wa gesi inayozalishwa nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia madini Profesa James Mdoe ( wa kwanza kushoto, waliokaa mbele); Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia nishati Dk. Mhandisi Juliana Pallangyo ( wa pili kushoto waliokaa mbele) pamoja na wataalam wengine wa Wizara ya Nishati na Madini wakifuatilia kwa makini hotuba iliyokuwa inatolewa na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini Nchini Uganda, Mhandisi Irene Muloni (hayupo pichani) katika mkutano kati ya nchi ya Tanzania na Uganda lengo likiwa ni kujadili mpango wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi katika bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Naye Waziri wa Maendeleo ya Nishati na Madini wa Uganda, Mhandisi Irene Muloni amesema kuwa bomba hilo likijengwa litanufaisha nchi mbili ambazo ziko katika huo mradi huo na unafanywa na wataalam katika nchi mbili.

Mhandisi Irene amesema kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi hivyo Uganda inahitaji gesi ambayo wataipata Tanzania kutokana na mahitaji ya viwanda nchini humo.

Amesema vyombo vya habari ni wadau muhimu katika kuhabarisha wananchi wa Uganda na Tanzania kwa kila kitu kinachoendelea kwa masilahi ya mapana ya kwa nchi ambazo  mradi zinatekeleza.
Wataalam kutoka Wizara, taasisi na makampuni ya mafuta kutoka Tanzania na Uganda wakifuatilia kwa makini mada iliyokuwa inawasilishwa na mwakilishi kutoka kampuni ya Total katika mkutano huo.

 Aidha ameipongeza Tanzania katika kuwa sehemu ya watekelezaji wa mradi huo na kuahidi kuendelea na ushirikiano katika miradi mingine.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini Nchini Uganda, Dk. Fred Kaliisa (kushoto) akifafanua jambo katika kikao hicho. Kulia ni Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini Nchini Uganda, Mhandisi Irene Muloni.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika bandari ya Tanga nchini Tanzania. Kulia ni Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini Nchini Uganda, Mhandisi Irene Muloni.
Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini Nchini Uganda, Mhandisi Irene Muloni (kulia) akifafanua jambo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilika kwa mkutano huo. Kushoto ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Balozi wa Uganda Nchini Tanzania, Dorothy Hyuha akifafanua jambo katika mkutano huo.

No comments: