Monday, April 18, 2016

Balozi Seif atembelea maeneo yaliyoathirika na mvua katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar

Mhandisi wa Baraza la Manispaa Mzee Juma Khamis wa kwanza kutoka kulia akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyefanya ziara kuangalia baadhi ya Mitaro iliyosababisha mafuriko kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hapa nchini. Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed na Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Nd. Said Juma Ahmada.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili a Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Abdoud Mohammed akimueleza Balozi Seif hatua zilizokwisha chukuliwa na watendaji wa Kamati ya Maafa katika kunusuru maafa yaliyojitokeza ndani ya kipindi cha mvua zilizoleta athari kubwa.
Balozi Seif akiwafariji Baadhi ya Wananchi wa Mitaa ya Kwahani, Kwawazee na Sebleni ambao nyumba zao zimeathirika kwa mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia Jumapili.
Skuli ya Nyerere Sekondari ni miongoni mwa skuli zinazotoa huduma ya muda ya kuwahifadhi watu walioathirika na mvua kubwa za juzi ambapo Balozi Seif alipata wasaa wa kuwatembelea kwa kuwapa pole. Picha na – OMPR – ZNZ.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshajiandaa rasmi kutoa viwanja vya ujenzi wa nyumba za kudumu kwa Wananchi wanaoendelea kukumbwa na maafa ya mafuriko wakati wa kipindi cha msimu wa mvua za masika hapa Nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara katika maeneo mbali mbali yaliyoathirika na mvua kubwa zilizofurika usiku wa kuamkia Jumapili na kuleta athari kubwa kwa Wananchi hasa katika Mkoa wa Mjini Magharibi.

Balozi Seif ambae aliambatana na Viongozi wa Kamati ya Taifa ya kukabiliana na Maafa Zanzibar kwa kuangalia mitaro wa uwanja wa Mnazi Mmoja, Kwa Binti Hamrani Mpendae pamoja na Bwawa na Sebleni Kwawazee hata hivyo alisema baadhi ya wananchi wanaopewa viwanja huamua kuviuza na baadae kurejea katika maeneo wanayohamishwa bila ya kuzingatia usalama wao.

Alisema kutokana na athari za mara kwa mara zinazoendelea kuwakumba wananchi katika maeneo mbali mbali nchini kutokana na majanga ya mafuriko ya mvua wakati umefika kwa wanaopewa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kudumu kuzingatia mipango miji ili kujikinga na athari zinazoweza kuepukika.

Balozi Seif alitanabahisha kwamba ujenzi usiozingatia mipango miji matokeo yake huleta adha, hasara na mashaka, na si vyema tabia hiyo ikaendelezwa wakati jamii inatambua athari inayoweza kujitokeza.

Mapema Mhandisi wa Baraza la Manispaa Zanzibar Nd. Mzee Juma Khamis alimueleza Balozi Seif kwamba maji yaliyotuwama katika mtaro wa Uwanja wa Mnazi Mmoja yataondoshwa mara baada ya kupunguwa kwa kina cha maji ya bahari.

Mhandisi Mzee alisema maji ya bahari hivi sasa yako juu hali iliyopelekea kufungwa kwa mlango wa kutolewa maji ya mvua yaliopo kwenye Uwanja huo kuelekezwa pwani jambao ambalo limekwamisha utoaji wa maji hayo.

Akizungumzia mtaro wa Kwa binti Hamrani Mhandisi huyo wa Baraza la Manispaa alimueleza Balozi Seif kwamba kazi za uendelezaji wa mtaro huo zimesimama kutokana na tatizo la baadhi ya nyumba zilizopo kwenye eneo linalokusudiwa kupitishwa mtaro huo.

Alisema kazi hiyo inaweza kuendelea tena baada ya wananchi wanaomiliki nyumba hizo kufanyiwa tathmini ya nyumba zao ili walipwe fidia na baadae kupisha ujenzi huo.

Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipata wasaa wa kuwafariji Wananchi wa Mitaa ya Kwahani, Kwawazee na Nyerere ambao wamehifadhiwa kwa muda katika skuli ya Sekondari ya Nyerere kwa Wazee.

Akiwapa pole wahanga hao Balozi Seif aliwaomba wananchi hao kuzingatia usafi wa mazingira kwa kulinda afya zao na hasa watoto wao wadogo ili kujiepusha na maambukizo ya maradhi kama kipindi pindu.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed alisema taratibu za kuwahifadhi wananchi walioathirika na mvua hizo zimeshakamilishwa na Serikali Kuu.

Mh. Aboud alisema Kamati ya Kukabiliana na Maafa tayari imeanza kupokea wananchi waliopata maafa ya mvua kwa kuwahifadhi katika skuli ya Sekondari ya Mwanakwerekwe “C ” ambapo eneo hilo liko salama kwa maazingira na afya zao.

Mwakilishi wa Timu ya Msalaba mwekundu { Action Team }inayotoa huduma kwa wahanga waliopo katika skuli hiyo ya Nyerere Shaaban Ali Iddi alisema timu yao inaendelea kutoa elimu ili kuwasaidia wananchi hao kujiepusha na maradhi ya matumbo.

Wakati huo huo Balozi Seif alikabidhi msaada wa vyakula mbali mbali ili kuwasaidia wahanga wa mafuriko hao wanaopata hifadhi ya muda katika skuli ya Sekondari Nyerere.

Msaada huo wa maji, maharage, mchele, sukari, sembe pamoja na mafuta ya kupikia umetolewa kwa pamoja na Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo la Amani Mwalimu Mussa Hassan Mussa na Mh. Rashid Ali Juma.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
18/4/2016.

No comments: