Wednesday, March 2, 2016

WAZIRI MKUU AAGIZA WATUMISHI WOTE WAHAMIE BUSEGA

 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi na watendaji wote wa Serikali wahamie yalipo makao makuu ya wilaya ya Busega kuanzia sasa ili kuleta kasi ya utendaji kazi kwenye wilaya hiyo ambayo ni mpya.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Machi 2, 2016) wakati akizungumza na wananchi waliofika kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi kwenye jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Busega mkoani Simiyu. Waziri Mkuu ambaye ameanza ziara ya siku sita ya mkoa huo atakagua shughuli za maendeleo na kusalimia na wananchi katika wilaya zote za mkoa huo.

"Leo nimeagiza watumishi wote wa umma katika wilaya hii wahame kutoka Magu ambako wanaishi hivi sasa na wahamie hapa Busega ili wafanye kazi kutokea hapahapa. najua kuna changamoto ya nyumba za watumishi lakini waje waishi kwenye nyumba za kupanga wakati Serikali ikiendelea kushawishi NHC, NSSF na Mwananchi Housing Corporation waje wajenge nyumba za watumishi kwenye halmashauri mpya," alisema.

Waziri Mkuu alisema kitendo cha watumishi kuhamia yalipo makao makuu ya wilaya kitasaidia kuongeza kasi ya kuleta maendeleo kwani watakuwa wanaziona changamoto zilizopo mahali wanapoishi. Alisema Serikali inao wajibu wa kujenga ofisi na nyumba za watumishi na kuwahakikishia kuwa azma hiyo itatimia kutokana na makusanyo ambayo Serikali imekuwa ikiyafanya hivi sasa ikilinganisha na siku chache zilizopita.

Jengo hilo la Halmashauri lililoanza kujengwa Julai 20, 2015 litagharimu sh. bilioni 4.66/- na linatarajiwa kukamilika Januari 20, 2017.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Busega, Bibi Gaudensia Bamugileki alisema changamoto kubwa inayowakabili ni kutopatiwa fedha kwa wakati hali ambayo alisema kama itaendelea itaathiri ukamilishaji wa jengo hilo kwa wakati.

"Hadi sasa mkandarasi ameshalipwa sh. milioni 600. Fedha ambazo zinahitajika kukamilisha ujenzi ni sh. 4,064,580,238/-. Tunaendelea kukumbushia fedha za ujenzi kutoka Serikali kuu ili tupunguze gharama ya kodi inayolipwa kwa jengo la kukodi ambalo pia halitoshelezi mahitaji ya vyumba vya ofisi kwa watendaji na watumishi wa Halmashauri," alisema.

Katika mkutano mwingine, mara baada ya kukagua wodi ya akinamama, Waziri Mkuu alizungumza na wakazi wa Nyashimo ambako wodi hiyo inajengwa na kuwahakikishia nia ya Serikali kufikisha huduma bora kwa wananchi.

Alitoa shukrani kwa ubalozi wa Japan kwa kuchangia ujenzi wa wodi kwa gharama ya dola za marekani 80,000 pamoja na nyongeza ya sh. milioni 312.1. Pia aliishukuru taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation ambayo tayari imejenga nyumba 10 za watumishi kwa ajili ya hospitali ya wilaya ya Busega.

Pia alisisitiza elimu kwa watoto wa kike na kumtaka Mkuu wa wilaya hiyo, Bw. Paul Mzindakaya afanye msako wa kubaini wale wote ambao hawajaanza kidato cha kwanza hadi sasa. "Serikali inataka watoto wote waliofaulu kwenda kidato cha kwanza wawe wameripoti shuleni. DC wewe ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hii. Fuatilia na kuwachukulia hatua wote waaliozuia watoto hawa wasiende shule," alisema.

"Suala la ulinzi kwa watoto wa kike hivi sasa ni la lazima. Ni lazima tuhakikishe mtoto akianza shule ya awali anaingia darasa la kwanza lazima amalize darasa la saba. Akiingia kidato cha kwanza, ni lazima amalize kidato cha nne, akiingia kidato cha tano ni lazima amalize kidato cha sita," alisisitiza huku akishangiliwa.

Mapema, akitoa taarifa ya mkoa huo, Mkuu wa Simiyu, Bw. Elaston aliomba kuongezewa ukomo wa bajeti ya mkoa kwa mwaka kwa sababu mkoa huo ni mpya na una changamoto nyingi ikilinganishwa na mikoa ya zamani ambayo haina mahitaji ya miundombinu.

"Mkoa wa Simiyu umetengewa ukomo wa bajeti sh. 1,117,133,000.00 wakati mikoa ya zamani kama Morogoro imetengewa sh. 2,836,225,000.00, Arusha (2,595,571,000.00), Kilimanjaro (2,543,463,000.00) Mbeya (2,141,239,000.00) na Tanga (2,318,545,000.00). Tunaomba tufikiriwa ili tuweze kuimarisha miundombinu ya ofisi, barabara, na huduma za jamii katika mkoa huu," alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, MACHI 2, 2016.

No comments: