Meneja wa Habari, Elimu
na Mawasiliano wa Wakala ya Serikali Mtandao Bi. Suzan Mshakangoto akitoa ufafanuzi
kwa waandishi wa Habari kuhusu taratibu zinazotakiwa kuzingatiwa na taasisi za
Serikali katika kuimarisha matumizi sahihi na salama ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano katika kuendesha mifumo ya Tehama Serikalini. Kushoto ni Mkurugenzi
wa Usimizi wa Huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Wakala hiyo.
Waandishi wa Habari
wakifuatilia mkutano huo.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma
za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Wakala hiyo Bw. Benedict Ndomba akifafanua
kuhusu mpango wa Serikali wa kuimarisha mawasiliano katika mifumo ya TEHAMA Serikalini.
Na Beatrice Lyimo - Dar es Salaam
Wakala ya Serikali mtandao (e-Government
Agency) imezishauri Taasisi zote za Umma ,Wizara, Idara zinazojitegemea, Sekreterieti
za Mikoa, Wakala na Mamlaka za Serikali ,Bodi, Tume, Mabaraza, Mifuko,
Mashirika ya umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa kufuata miongozo na viwango
vilivyotolewa Wakala hiyo katika uanzishaji na usimamizi wa mifumo ya Tehama
Serikalini.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na
Meneja wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala ya Serikali Mtandao Bi. Suzan
Mshakangoto alipokuwa akitoa maelekezo na ufafanuzi wa taratibu zinazotakiwa
kuzingatiwa na taasisi hizo kwa lengo la kuimarisha matumizi sahihi na salama
ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika kuendesha mifumo ya Tehama
Serikalini.
Bi. Mshakangoto amesema kuwa miongozo na
viwango hivyo vinalenga kuziwezesha taasisi za umma kujenga mifumo inayoendana
na mahitaji halisi ya taasisi husika na kuepuka mifumo inayojengwa kwa
shinikizo la wafanyabiashara, wafadhili au kwa matakwa ya mtu binafsi.
“ Taasisi zote zikitumia miongozo ya
viwango tuliyoweka, Serikali itakuwa na uwezo wa kuepuka urudufu wa mifumo na
kupunguza gharama kubwa za uendeshaji kwa kuwa na mifumo endelevu yenye gharama
halisi inayofuata viwango vya Usalama katika kulinda taarifa na data za
Serikali” Alifafanua Meneja huyo.
Amezishauri taasisi hizo kuwasilisha
maandiko ya mifumo mipya ya TEHAMA na kujaza taarifa za mifumo au miradi ya
TEHAMA iliyopo katika mfumo wa kukusanya na kutunza taarifa za miradi ya TEHAMA
Serikali ili iweze kuthibitishwa iwapo imefuata miongozo na viwango
vilivyowekwa kabla ya kujengwa na kusakinishwa.
Akitoa ufafanuzi kuhusu wafanyabiashara
wanaojihusisha na miradi au utengenezaji wa mifumo ya TEHAMA Serikalini amesema
kuwa wanashauriwa kufuata miongozo na viwango hivi ili kujua mahitaji halisi ya
Serikali na kuweza kujenga mifumo ya TEHAMA endelevu na inayoleta tija kwa
umma.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usimizi wa
Huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Wakala hiyo Bw. Benedict
Ndomba ameeleza kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa mifumo yote ya
TEHAMA ya Serikali inakuwa na mawasiliano na kubadilishana taarifa mbalimbali.
Amesema kuwa Serikali imekuwa ikiweka msisitizo
wa matumizi ya TEHAMA kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji kwa
kuwawezesha wananchi na wadau mbalimbali kupata huduma za Serikali kwa gharama
nafuu kwa njia ya Mtandao.
Wakala ya Serikali
Mtandao (e-Government Agency) ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2012
kwa sheria ya Wakala za Serikali Na. 30, Sura ya 245 ya mwaka 1997. Wakala hii
ina majukumu na mamlaka ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali
Mtandao nchini Tanzania.
No comments:
Post a Comment