Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Profesa Makame Mbarawa (katikati)
akizungumza na Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Vietnam Bw. Nguyen Bac Son
(kushoto) kuhusu ushirikiano baina ya Tanzania na Vietnam na (kulia) ni Naibu Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwini Ngonyani.
Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Vietnam Bw. Nguyen Bac Son (kulia) akimuaga
mwenyeji wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Profesa Makame
Mbarawa wa pili (kushoto) baada ya kufanya mazungumzo ya ushirikiano katika sekta
ya Mawasiliano, (kushoto) ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng.
Edwini Ngonyani.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (Mb) amekutana na
Waziri wa Habari na Mawasiliano wa nchi ya Vietnam Bwana Nguyen Bac Son ofisini
kwake kwa lengo la kupanua wigo wa uwekezaji kwenye Sekta ya Mawasiliano nchini
Tanzania na kushirikiana kwa pamoja kuendeleza Sekta hizo baina ya Tanzania na
Vietnman. Kikao hicho ni muendelezo wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti wa
Vietnam, Mhe. Truong Tan Sang na ujumbe wake nchini Tanzania.
Prof. Mbarawa alisema kuwa Tanzania imekuwa na ushirikiano na Vietnam kupitia
Kampuni ya Viettel kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya kufikisha huduma za
mawasiliano vijiini kwa kutiliana saini Mkataba. Mkataba huo ni wa miaka mitatu
kuanzia mwezi Oktoba mwaka 2014 hadi Novemba, 2017 ikijumuisha ujenzi wa
miundombinu ya Mkongo wenye urefu wa kilomita 20,000 kwenye wilaya zote nchini;
kujenga miundombinu ya mawasiliano kwenye vijiji 4,000; kuunganisha Ofisi za Wakuu
wa Wilaya; hospitali za Wilaya; Ofisi zote za Posta za Wilaya; na kupeleka na kutoa
huduma za intaneti bila malipo kwenye shule 3 za Sekondari za Serikali katika kila
Wilaya nchini kwa kipindi cha miaka mitatu.
Aidha, Prof. Mbarawa aliongeza kuwa tangu Kampuni ya Viettel yenye jina la biashara la
Halotel ilipoanza kufanya kazi rasmi mwezi Oktoba mwaka 2015, imeweza kupeleka
huduma ya mawasiliano maeneo ya vijijini na hadi hivi sasa ina watumiaji wa simu za
mkononi wapatao milioni 1.2 na wananchi walio wengi wanafurahia huduma hiyo tofauti
na hali ilivyo kuwa hapo awali kipindi cha miezi sita iliyopita na ikizingatiwa kuwa
sehemu nyingine za vijijini hapakuwa na mawasiliano.
Pia alisema kuwa, “Serikali ya
Tanzania itaendelea kujenga na kuwekeza kwenye Sekta ya Mawasiliano ili kuwavutia
wawekezaji na kampuni za simu za mkononi ambapo Serikali ya Tanzania ilitoa ruzuku
kiasi cha dola za marekani milioni 30 ili kuziwezesha kampuni hizo kupeleka
mawasiliano vijijini na maeneo yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara”.
Hadi kufikia mwezi
Machi, 2016 Halotel imejenga Mkongo wenye urefu wa kilomita 18,000 kati ya kilimota
20,000; na kujenga miundombinu ya mawasiliano kwenye vijijini 1,605 kati ya vijiji
4,000 visivyokuwa na mawasiliano.
Katika mazungumzo hayo ya kuendeleza sekta ya Mawasiliano Tanzania, Prof. Mbarawa
aliwaalika wawekezaji kutoka Vietnam wa Sekta ya Mawasiliano na kampuni ya Halotel
kujiandaa na kuja Tanzania kushiriki mnada wa kununua masafa ya 700MHz ambayo
yamepatikana baada ya kuhama kutoka Teknolojia ya Utangazaji ya Analojia na
kuhamia Teknolojia ya Utangazaji ya Dijitali. Pia alisema kuwa Kampuni za Vietnam
zinakaribishwa kuanzisha na kuendeleza huduma za mawasiliano za mfumo wa
kumpatia mteja huduma tatu kwa pamoja ya sauti; intaneti; na kuangalia televisheni
ikijulikana kwa jina la triple player ili Tanzania iweze kwenda sambamba na kasi ya
ukuaji wan a maendeleo ya TEHAMA yanayotokea dunia nzima.
Katika kikao hicho, Prof. Mbarawa alimweleza Mhe. Ngoyen Bac Son kuwa Tanzania iko
tayari kusaini Mkataba wa Makubaliano ya ushirikiano na Serikali ya Vietnam wa
kubadilishana wataalamu kwenye Sekta ya Mawasiliano na kuwapatia mafunzo ili
kujenga uwezo wa wataalamu wetu wa Tanzania; na kuanzisha na kuendeleza viwanda
vidogo vidogo vya TEHAMA (ICT Small Scale Factories) nchini Tanzania ambapo
viwanda hivyo vitazalisha ajira; kurahisisha upatikanaji wa vifaa na huduma za TEHAMA
kuendana na mahitaji na mazingira yetu; kuongeza mapato; na kuwahudumia wateja
wa nchi za jirani na Tanzania.
Mhe. Ngoyen Bac Son alisema kuwa Serikali ya Vietnam iko tayari kuendeleza
ushirikiano baina ya Serikali yao na ya Tanzania ya kuendeleza Sekta ya Mawasiliano;
na sekta ya kukuza Uchumi na Maendeleo ya Tanzania kama alivyozungumza Rais wa
Vietnam. Pia aliongeza kuwa, “Serikali ya Vietnam iko tayari kuleta kampuni za
kuwekeza Tanzania kwa kuanzisha Kiwanda cha vifaa vya mawasiliano kwa ajili ya
kuwapatia watanzania huduma za mawasliano na ni matarajio yetu kuhakikisha kuwa ni
kiwanda kikubwa ambacho kitahudumia na wateja wa nchi za jirani na Tanzania”.
Aidha, Mhe. Ngoyen Bac Son aliongeza kuwa Serikali ya Vietnam inaridhia kusaini
Mktaba wa Ushirikiano baina ya nchi hizo na amewakaribisha wafanyabiashara na
kampuni za Tanzania kwenda kuwekeza nchini Vietnam.
No comments:
Post a Comment