Saturday, March 19, 2016

UTEUZI WA MKAPA UNATIA MATUMAINI - BAN KI MOON

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akiwasilisha mbele ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, taarifa yake kuhusu ziara yake aliyoifanya hivi karibuni nchi Burundi. Katika taarifa yake ameelezea kutiwa matumaini na uteuzi wa Rais Mstaafu Mhe. Benjamin Mkapa kuwa Mwezeshaji wa majadiliano ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa Burundi.
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akizungumza kwa niaba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mkutano wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana Ijumaa uliojadili kuhusu Burundi. Aliyeketi nyuma ya Balozi, ni Bw. Khamis Abdallah Afisa wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Burundi, Bw. Alain Amic Nyamitwe naye akielezea hali ya mambo na jitihada mbalimbali ambazo serikali ya Burudi imekuwa ikichukua katika kurejesha hali ya amani na utulivu.
Wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, katika mkutano wao wa Ijumaa ambapo baada ya kupokea taarifa kuhusu Burundi, waliendelea na kikao chao cha ndani.

Na Mwandishi Maalum, New York

Wakati Mwezeshaji wa majadiliano kuhusu mgogoro wa kisiasa nchini Burundi, Rais Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Benjamin William Mkapa akiwa ameanza mchakato wa kukutana na viongozi na wadau mbalimbali. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amesema, uteuzi wa Benjamin Mkapa unatia matumaini.

Ban Ki Moon ametoa kauli hiyo jana Ijumaa, wakati alipokuwa akiwasilisha mbele ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, taarifa kuhusu ziara yake aliyoifanya nchini Burundi mwezi uliopitia.

“ Uteuzi uliofanywa na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa kumteua Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa kuwa mwezeshaji wa majadiliano kuhusu Burundi ni maendeleo yanayotia moyo”. Amesema Ban Ki Moon.

Na Kuongeza, ni lazima Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Afrika, Jumuiya na Umoja wa Mataifa kusaidia utalamu wa hali ya juu wa usuluhishi ambao Burundi unahitaji. Akielezea zaidi kuhusu ziara aliyoifanya nchi Burundi ziara iliyomwezesha kukutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Kisiasa akiwamo Rais wa Nchi hiyo Bw. Piere NKurunzia. Ban Ki Moon, amesema hakuna njia mbadala zaidi ya mazungumzo ya kisiasa ambapo pande zinazopingana zitakaa katika meza ya mazungumzo.

Akasema, wakati wa ziara hiyo iliyofuatia baada ya wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama kufaya ziara yao, alitoa wito kwa wadau wa pande zote kutorejea kule walikotoka akimaanisha vita vilivyosababisha vifo vya wananchi wengi wa nchi hiyo kabla ya kupatika kwa Mkataba wa Amani wa Arusha ( The Arusha Agreement).

“ Nilitoa wito kwa pande zinazopinga na wananchi wa Burudi kutorejea kule walikotoka na waonyeshe dhamira ya dhati ya kukaa katika meza ya mazugumzo yatakayokuwa jumuishi na umoja wa kisiasa kwa kuwa hiyo ndiyo njia sahihi na pekee ya kutatua mgogoro wao “. Akasisitiza Ban Ki Moon.

Ban Ki Moon ameeleza zaidi kuwa aliwaeleza viongozi wa Burundi kwamba kusainiwa kwa Mkataba wa Arusha Agosti 2000 uliotokana mahasimu kukaa meza moja na kukaa katika meza na kukubaliana kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe pia ulifungua ukurasa mpya wa maridhiano na kushirikiano wa kuijenga nchi yao.

Akabanisha kuwa Rais wa Burundi wakati wa mazungumzo yao aliahidi kutekeleza mambao kadhaa yakiwako ya kuwaachia huru wafungwa wakiwamo viongozi wa upinzani, kutoa uhuru kwa vyombo vya habari pamoja na kusitisha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na mauaji ya holela.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akizugumza kwa niaba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ameliambia Baraza Kuu la Usalama kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli, kama Mwenyekiti wa EAC, anaamini kwa dhati kabisa kwamba hali ya kisiasa nchini Burundi inaishughulisha siyo tu Ukanda wa Afrika ya Mshariki, bali pia Jumuiya ya Kimataifa.

“ Hali ya Kisiasa inaishughulisha EAC na Jumuiya ya Kimataifa, siyo kwa sababu Burundi ni mwanachama wa EAC, lakini ni kutokana na ukweli kwamba athari za mgogoro wa Burundi zinaweza kutuathiri sisi sote ”. Akasema Balozi Manongi kwa niaba ya EAC.

Na kuongeza ni kwa kulitambua hilo ndiyo maana EAC inaendelea na juhudi zake za kutafuta suluhu ya kudumu nchini Burundi, na kwamba inakaribisha juhudi zinazofanywa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa za kushirikiana na Burundi na Kanda ya Afrika Mashariki.

“Sisi kama Jumuiya ya Afrika Mashariki tunaomba juhudi hizi tunazozikaribisha ziende sawia na hatua za kuboresha na kusaidia mahitaji ya kijamii na kiuchumi ya watu wa Burundi, ikiwani pamoja na kuisaidia kuimarisha mifumo na Taasisi zake za kiutawala.” Amesisitiza Balozi Manongi.

Msemaji huyo wa EAC akabinisha kwa kusema , hapana shaka pana mambo mengi yanayochangia uwepo wa hali tete ya kisiasa nchini Burundi. Mambo anayosema yanapashwa kujadiliwa wa uwazi na katika ujumla wake. Na kwamba EAC inawashukuru wale wote ambao wamekuwa wakiunga mkono jitihada zinazofanywa na EAC.

Akizungumzai kuhusu utezi wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kuwa mwezeshaji wa mazungumzo ya Burundi akimsaidia Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, Balozi Manongi amesema, EAC imetiwa na inashukuru kwa kauli za kutia moyo za kuukubali uteuzi wa Rais mstaafu Mkapa.

Akasema katika juhudi zake za kuisaidia Burundi na watu wake alizofanya wakati wa mchakato wa Amani wa Arusha. Mkapa alisema yafuatayo “ Suluhu endelevu kuhusu mgogoro wa Burundi unatakiwa kutoka ndani ya majadiliano ambayo wadau wote wenye dhamana kuhusu Burundi watashiriki kwa uhuru. Suluhu endelevu inatakiwa kumilikiwa na kuheshimiwa na washiriki wote wa mchakato wa kutafuta amani. Shinikizo kutoka nje haiwezi kuleta suluhu ya kudumu”

Balozi Manongi akabanisha kwamba maneno hayo aliyoyasema Rais Mstaafu wakati huo bado yana matinki na uzito katika mazingira na hali ya sasa ya Burundi.

Na kuongeza , inatia moyo kuwa Rais Mstaafu Mkapa amekwisha anza ziara za awali za kuwatembelea viongozi na wadau mbalimbali ndani ya EAC kwa lengo la kuhakikisha kwamba viongozi na wahusika wote wanakuwa na uelewa wa pamoja kuhusu dhamana mpya aliyokabidhiwa. Na amewahakikishia viongozi wa EAC dhamira yake, kujituma kwake, uwazi na ujumuishi katika utekelezaji wa dhamana hiyo.

“Rais Mstaafu Mkapa anahitaji uungwaji mkono wa dhati na ushirikiano kutoka pande zote nchini Burundi, katika EAC na katika Jumuiya ya Kimataifa” akasisitiza Balozi Manongi.

Wengine waliotoa taarifa zao kuhusu hali ya Burundi alikuwa ni Kamishna wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu Prince Zeid Raad Hussein, Mwenyekiti wa Burundi Configuration Balozi Jurg Lauber na Bw. Alain Amic Nyamitwe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Burundi.

No comments: