Sunday, March 20, 2016

TPA yaipiga tafu Hospital ya Kisarawe

Meneja Mawasiliano wa TPA, Bibi Janeth Ruzangi (kulia) akikabidhi vitanda 20, magorodo 20 na mashuka 100, vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 13 kwa hospitali ya Wilaya ya Kisarawe mwishoni mwa wiki. Anayekabidhiwa vifaa hivyo ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Bwana Hamis Likupotile (kushoto) na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dkt Elizabeth Oming'o. Makabidhiano hayo yaliyafanyika hospitali hapo.
Meneja Mawasiliano wa TPA, Bibi Janeth Ruzangi (kulia) akikabidhi vitanda 20, magorodo 20 na mashuka 100, vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 13 kwa hospitali ya Wilaya ya Kisarawe mwishoni mwa wiki. Anayekabidhiwa vifaa hivyo ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Bwana Hamis Likupotile (kushoto) na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dkt Elizabeth Oming'o. Makabidhiano hayo yaliyafanyika hospitali hapo.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetoa msaada wa Vitanda 20, Magodoro 20 na Shuka 100 kwa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani.

Vitanda hivyo vya kisasa aina ya ‘Cardiac’, mashuka pamoja na magodoro yake vilivyokabidhiwa katika hospitali hiyo ya wilaya vina thamani ya shilingi za kitanzania milioni 13.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Meneja Mawasiliano wa TPA, Bibi Janeth Ruzangi alisema msaada huo ni sehemu ya wajibu wa Mamlaka kuisaidia jamii ya Watanzania.

“Pamoja na shughuli zake za kupakua na kupakia mizigo, Mamlaka pia ina wajibu wa kurudisha kile inachokipata kutokana na huduma zake kwa kuisaidia jamii na ndio maana leo hii tumekuja kutekeleza wajibu huo,” alisema Ruzangi.

Bibi Ruzangi alisema pamoja na kwamba msaada huo ni mdogo lakini wana imani utasaidia kupunguza changamoto za uhaba wa vitanda katika hospitali hiyo ya wilaya. Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dkt Elizabeth Oming’o hospitali hiyo ina uhaba wa vitanda 94 na mashuka 1,200.

“Hiki kilicholetwa na Mamlaka ya Bandari ni zaidi ya msaada kwani vitanda hivi ni vya kisasa na ni vya gharama sana,” alisema Dkt Oming’o.

Dkt Oming’o alisema kwamba wanashukuru sababu msaada huo utaenda kupunguza pengo la uhaba wa vitanda na mashuka walilonalo hospitalini hapo. Alisema kwamba mbali ya vitanda na mashuka hayo, pia wana changamoto ya vitanda vya upasuaji. Vilivyopo sasa katika hospitali hiyo vimechakaa na hivyo havikidhi mahitaji yao.

Akizungumzia vitanda walivyokabidhiwa na TPA, Dkt Oming’o alisema ‘Cardiac bed’ ni vitanda vya kisasa kabisa ambavyo hospitali hiyo ilikuwa haina.

“Vitanda hivi ni gharama sana kiasi kwamba kama tungeamua kwenda kuvinunua kwa pesa yetu, hakika tusingeweza,” alisema.

Alisema wamefarijika na ujio wa vitanda hivyo kwani vitarahisisha kazi zao kwa kiasi kikubwa.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bw. Hamis Likupotile alisema wanaishukuru Mamlaka kwa msaada huo kwani hospitali yao ina upungufu mkubwa wa vitanda.

Vitanda hivi 20 na magodoro yake pamoja na mashuka ni msaada mkubwa kwetu kwani umesaidia kutatua tatizo sugu la uhaba wa vitanda katika hospitali hiyo. Alisema kwamba changamoto walizo nazo ni nyingi na walishapeleka maombi sehemu mbalimbali ili wasaidiwe lakini kote bado hawajibiwa.

“Kwa kweli tunawashukuru sana TPA kwani katika mashirika yote tuliyoomba, bandari ndio wamekuwa wa kwanza kutujibu na kutusaidia kwa wakati,” alisema. Hospital hiyo kwa sasa imekuwa chombo muhimu si kwa Kisarawe tu bali hata kwa wananchi wa mikoa jirani kwani kwasasa wanahudumia watu wengi sana kutoka Gongo la Mboto, Pugu na Mbagala.

Kwahiyo alisema msaada huo umesaidia jamii kubwa ya watanzania na si Kisarawe pekee, hivyo kuiomba Mamlaka iendelee kuwasaidia vifaa tiba vingine, kwani ujio wa wagonjwa wengi pia huleta changamoto nyingi.

No comments: