JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
Ndugu
Wanahabari, tukiwa tunaelekea sikukuu ya pasaka, Serikali ya Mkoa wa Dodoma
imeona ni vyema ikakutana na wawakilishi wa vyombo vya habari hapa Mkoani
Dodoma, ili kupitia vyombo vya habari, tupate fursa ya kuweka wazi kwa wananchi
wa Dodoma na watanzania kwa ujumla masuala ya msingi ambayo yamejiri hapa
Mkoani Dodoma.
Awali, usiku
wa kuamkia jana kuna tukio tunaloweza kuita la ujambazi lilitokea kama majira
ya saa 8 usiku ambapo kundi la watu takribani saba (7) ambao bado
hawajafahamika walivamia ofisi za Halotel Mkoani Dodoma kwa lengo la kutaka
kufanya uhalifu ambapo waliwavamia askari wawili waliokuwa wakilinda Ofisi
hiyo, ambapo pamoja na athari nyingine zilizojitokeza; walipora silaha aina ya
SMG na kumjeruhi askari mmoja ambaye alilazwa kwa matibabu kwenye Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kuruhusiwa jana hiyohiyo.
Hadi hivi sasa
Jeshi la polisi Mkoa wa Dodoma linaendelea kulifanyia kazi suala hilo ambapo
hadi tunavyozungumza sasa tayari silaha hiyo iliyoporwa imeshapatikana,
uchunguzi zaidi wa suala hilo unaendelea kubaini watu wote waliohusika.
Kufuatia suala hilo, Serikali ya Mkoa wa Dodoma, kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa
Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana anapenda kutoa tamko lifuatalo:
·
Kwanza
kabisa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana analaani vikali tukio hilo
la uhalifu na kuwa halivumiliki na halikubaliki katika Mkoa wa Dodoma na Mikoa
mingine hapa nchini na amewataka wananchi wema kutoa ushirikiano kwa vyombo vya
Dola ili kuwabaini wahusika na kukomesha matukio kama hayo.
·
Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana analiagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa
Dodoma kuhakikisha wanafanya uchunguzi na kuwabaini wale wote waliohusika
katika tukio hilo la uhalifu,ili kuwatia mbaroni na kuwachukulia hatua kali za
kisheria. Aidha amelitaka jeshi la polisi kujipanga vizuri na kuhakikisha kuwa
tukio hili ni la mwisho na halijitokezi tukio jingine la aina hii.
·
Aidha,
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa
Dodoma kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama kuna dalili
zozote za kuwepo kwa uzembe wa aina yoyote kwa askari hao waliokuwa wanalinda
Ofisi hiyo, na endapo itabainika kulikuwa na uzembe basi Jeshi la polisi
lichukue hatua kali kwa askari hao waliohusika.
Katika hatua nyingine, Mnamo mwezi
Februari kulitokea tukio la mgogoro baina ya jamii za kifugaji za wamaasai na
wabarbaig/Mang’ati eneo la mpakani mwa wilaya ya Kondoa kwa upande wa Mkoa
wa Dodoma na Wilaya ya Simanjiro kwa
Upande wa Mkoa wa Manyara, ambapo Mama mmoja mja mzito jamii ya Kibarbaig akiwa
anachunga mifugo aliuwawa na watu inaosemekana ni jamii ya wamasai na kisha
mifugo aliyokuwa akichunga (ngombe 25) kuibwa.
Katika kile kinachoonekana kama
kulipiza kisasi au kujibu mapigo, wabarbaig nao walivamia kwa wamasai na kuiba
ng’ombe 112 ambao baadae walirudishwa
kwa wamasai huku Ngombe 25 wakiwashikilia kwa lengo la kutaka kulipwa ng’ombe
zao 25 zilizoibiwa wakati zikichungwa na mama wa kibarbaig aliyeuwawa na baada
ya wamasai kurudisha ngombe hao 25 na kusaidia aliyehusika na mauaji kupatikana,
wabarbaig walirudisha ng’ombe hao 25 wa wamasai waliokuwa wamewashikiria.
Baada ya siku mbili au tatu Wamasai
waliibuka na madai kwamba ngombe wao 101wameibiwa na kijana mmoja wa kimasai
kukutwa amekufa wakiwashutumu wabarbaig kuhusika na matukio hayo na kudai
serikali isimamie ngombe zao hizo zirudishwe na kutaka mtu au watu waliyohusika na wizi na mauaji hayo
kupatikana na kukamatwa.
Baada ya uchunguzi ilibainika kuwa
kijana huyo wa kimaasai alikutwa amekufa vichakani siyo kwenye boma kama
walivyodai wamaasai hapo awali na ilionekana kuwepo kwa dalili kuwa amekufa
kabla ya mgogoro huo wa wamaasai na Barbaig kuanza.
Mgogoro huu ulikua na dalili za
kutishia amani na usalama wa maeneo yale na jamii zile husika. Kwa muda wote
serikali za mikoa miwili ya Dodoma na Manyara kupitia kwa viongozi wao na
kamati za ulizi na usalama zilihusika kwa karibu na kuhakikisha athari zaidi
hazitokei.
upande wa wafugaji jamii ya kimasai
walilalamika serikali kutoshughulikia suala hili ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
ng’ombe wao 112 waliokuwa wameibwa na wabarbaig wanarejeshwa, Kufuatia hali
hii, Wakuu wa Mikoa ya Dodoma na Manyara na kamati zao za Ulinzi na Usalama za
Mikoa yao na Wilaya husika walikubaliana na kutoa maagizo yafuatayo:
·
Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana kwanza kabisa amekemea na kulaani
vikali matukio hayo ya uhasama na wizi wa mifugo kati ya makundi hayo yenye
kuhatarisha usalama na amani ya makundi husika. Vilevile serikali haitavumilia
matukio kama hayo ya uvunjifu wa amani badala yake kila mtu/mwananchi anatakiwa
kufuata na kutii sheria za nchi bila shuruti.
·
Mhe.
Rugimbana ameliagiza Jeshi la polisi Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Polisi
Mkoa wa Manyara na viongozi wa kimila kutoka pande zote mbili kwenda nyumba
hadi nyumba kutambua wamaasai walioibiwa ng’ombe hao 112 pia na ng’ombe wenyewe
walioibiwa, alama zao kisha kufanya msako wa boma hadi boma kubaini ng’ombe hao
walioibiwa.
·
Wakati
wote huo zoezi hilo likiendelea ametaka wananchi kutii sheria za nchi bila
shuruti na kuhakikisha wana dumisha usalama na amani wakati wote na endapo baada
ya zoezi hilo itabainika shutuma hizi za kuibiwa ng’ombe sio za kweli basi waliotoa
shutuma hizi wachukuliwe hatua kali za kisheria.
·
Amezipongeza
kamati za ulinzi na usalama za Mikoa ya Dodoma na Manyara na viongozi wa Wilaya
za Kondoa na Simanjiro kwa kusimamia vizuri utatuzi wa Mgogoro huu na kutaka
wazidi kushirikiana na wananchi wao pia ili kulipatia ufumbuzi tatizo hili kwa hali ya amani.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma Mhe.Jordan Rugimbana amepongeza na ameunga Mkono hatua iliyochukuliwa na
Naibu waziri Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Suleiman
Jafo ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ghala la usindikaji ngozi za wanyama
lisilo Rasmi eneo la Mailimbili juzi tarehe 24 machi, 2016 ambapo alibaini ghala hilo halifuati taratibu
na kanuni za Afya na usafi wa mazingira na kuwa limekuwa kero kwa wakazi wa
eneo hilo na lina hatarisha Afya zao. Mhe. Naibu Waziri Jafo aliamua kulifunga
ghala hilo na kuwapa siku tano uongozi wa Manispaa ya Dodoma kuhakikisha ngozi
na vitu vyote kwenye ghala hilo vinaondolewa kutokana na kuendeshwa kinyume cha
taratibu za Afya.
Katika kuunga mkono hatua alizozifanya
Mheshimiwa Naibu Waziri Jafo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana amewaagiza Uongozi wa
Manispaa ya Dodoma na Wamiliki na waendeshaji wa ghala hilo wafike Ofisini
kwake mara moja kwa lengo la kuzungumzia tatizo hilo na kutafuta namna ya kulimaliza
mara moja ili kuhakikisha usalama wa Afya za wananchi waliopo eneo linalozunguka
ghala hilo unalindwa, vilevile kuzuia
magonjwa yanayoweza kusababishwa na hali hiyo lakini kikubwa ikiwa kutafuta
namna bora inayozingatia taratibu za Afya katiika kuanzisha maghala na viwanda
vya ngozi.
Mwisho kabisa, Serikali ya Mkoa wa
Dodoma inatumia fursa hii kuwataka wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma kusherehekea
sikukuu ya Pasaka kwa hali ya Amani, utulivu na Usalama. Na kuwa kila mwananchi
ahakikishe anakua balozi mwema kwa kufuata maelekezo haya ya serikali ya Mkoa,
pia wamiliki na wasimamizi wa kumbi zote za starehe na burudani wanatakiwa
kuzingatia agizo lililotolewa na baraza la sanaa hapa nchini na kuzingatia masharti
ya Leseni zao za biashara ikiwa ni pamoja na kutoruhusu madisco ya watoto
kwenye kumbi za burudani. vilevile, kumbi za burudani na starehe zifungwe kwa
wakati sahihi kwa mujibu wa leseni za biashara za kumbi hizo.
Amewataka maafisa utamaduni wilaya
zote kwa kushirikiana na Jeshi la polisi kuhakikisha maagizo haya ya serikali
yanatekelezwa ipasavyo.
Mwisho Mkuiu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.
Jordan Rugimbana anawatakia wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma sikukuu njema ya
Pasaka.
Imetolewa na
Idara
ya Mawasiliano ya Serikali
OFISI
YA MKUU WA MKOA WA DODOMA
MACHI
25, 2016
No comments:
Post a Comment