Tuesday, March 29, 2016

Serikali ya Tanzania kujenga bomba la mafuta kutoka Tanga hadi Uganda

Imeelezwa kuwa Tanzania ina vigezo mbalimbali ambavyo vinaifanya nchi ijiamini kwa asilimia 98 kuwa mradi wa bomba la kusafirishia mafuta kutoka Ziwa Albert nchini Uganda utapitia  Kaskazini mwa Tanzania hadi Bandari ya Tanga badala ya nchini Kenya.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa wakati wa kikao chake na wafanyabiashara wa mafuta nchini ambacho kililenga kujadiliana nao kuhusu fursa za uwekezaji zitakazotokana na mradi huo endapo utapita nchini.

Profesa Ntalikwa alivitaja vigezo hivyo kuwa ni uzoefu wa Tanzania katika ujenzi wa mabomba ya kusafirisha nishati mbalimbali ikiwemo Bomba la Mafuta la kutoka Tanzania hadi Zambia (TAZAMA), Bomba la kusafirisha gesi kutoka  SongoSongo hadi Dar es Salaam, Bomba la kusafirisha gesi kutoka eneo la Mnazi Bay hadi Mtwara, pamoja na Bomba kuu la gesi kutoka mkoani Mtwara hadi Dar es Salaam lenye kipenyo cha inchi 36 hivyo uzoefu huo utasaidia katika kupunguza muda wa ujenzi wa bomba la mafuta ambalo kipenyo chake ni inchi 24.

“Tumewaeleza wenzetu kuwa Serikali ya Tanzania pia ilishajenga uwezo mkubwa katika masuala ya kutwaa, kumiliki na kulipa madai ya wananchi wanaopisha miradi ya mabomba na shughuli hizi zimekuwa zikifanywa kwa wepesi na umakini mkubwa ikiwemo umakini katika kufuata kanuni na sheria za mazingira, hivyo haitatuwia ngumu katika kutekeleza mradi huu,” alisema Profesa Ntalikwa.
Alitaja kigezo kingine kuwa ni ubora wa bandari ya Tanga ambayo imeonekana kuwa ni bora zaidi ukilinganisha na Bandari nyingine Afrika Mashariki kwa kuwa ina kingo za asili (naturally sheltered) na kina kirefu hivyo kupunguza muda na gharama za ujenzi kwa kuwa uchimbaji wa kuongeza kina hauhitajiki na itakuwa na uwezo wa kupakia mafuta katika kipindi cha mwaka mwaka mzima.
Profesa Ntalikwa aliongeza kuwa njia ya kupitia Tanzania hadi Bandari ya Tanga ni bora zaidi kwa upande wa ujenzi wa bomba hilo kwa kuwa haipiti sehemu yenye makazi ya watu wengi, sehemu za hifadhi na haina miinuko mikali hivyo kupunguza muda wa ujenzi na gharama za ujenzi.
“ Hivyo ndugu zangu tumewaita wafanyabiashara hawa wa mafuta nchini ili waweze kutumia fursa mbalimbali zitakazotokana na mradi huo na kuzichangamkia na wao wamepokea vizuri suala hili na wameahidi kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kwamba Tanzania inapata mradi huu muhimu,” alisema Profesa Ntalikwa.
Awali akizungumza kuhusu mradi huo, Mkurugenzi wa Mkondo wa Chini kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. Wellington Hudson alieleza kuwa Uwekezaji wa mradi  bomba hilo unakadiriwa kugharimu Dola za Marekani bilioni 4 na kwamba Bomba lote litakuwa na urefu wa kilomita  1403 na kipenyo cha inchi 24.
Alisema kuwa hatua zilizofikiwa hadi sasa ni kuwa Serikali za Tanzania na Uganda zilishatiliana sahihi Mkataba wa Maelewano (MOU) tarehe 12 Oktoba 2015 ambao kwa sasa ndiyo mwongozo wa kukamilisha majadiliano ya mikataba mbalimbali ambayo inayohitajika kisheria.
“Kwa sasa lengo ni kukamilisha mazungumzo mapema na kusainiwa kwa Mikataba husika, ili kuruhusu shughuli za upatikanaji wa mkuza na ujenzi kuanza maramoja. Ujenzi unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu baada ya Mikataba yote muhimu kusainiwa,” alisema Dkt. Wellington.
Alitaja baadhi ya faida zitakazopatikana kutokana na mradi huo kujengwa Tanzania kuwa ni kuchochea shughuli za utafutaji mafuta nchini hususani katika maeneo linapopita bomba la mafuta, Kuimarisha matumizi ya Bandari ya Tanga na hivyo kuongeza mapato ya Serikali kutoka katika bandari hiyo pamoja na kupatikana mkuza utakaoweza kutumika siku za baadaye kwa shughuli nyingine za maendeleo ikiwemo kusafirisha gesi na mafuta katika mikoa ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa na nchi za jirani.
Faida nyingine zitakazotokana na mradi huo ni Ujenzi wa barabara mpya takriba kilometa 200 na uboreshaji wa barabara zilizopo takriban kilometa 150 na madaraja katika maeneo linapopita bomba,
Pia kuongezeka kwa fursa ya Shirika la Reli Tanzania kufanya biashara ya kusafirisha kiwango cha mabomba yanayokadiriwa kufikia 123,000 kupitia miundombinu ya reli iliyopo, Fursa za ajira kwa takribani watu 15,000 wakati wa ujenzi na watu wapatao 1,000 wakati wa kuendesha mradi.
Dkt. Wellington pia aliwaasa Watanzania kuchangamkia fursa zitakazojitokeza endapo bomba hilo litapita nchini na kuzitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni kazi za kuunganisha mabomba (welding),  huduma za afya, huduma za mabenki, huduma za usafi na kudhibiti taka, Kandarasi za kujenga na za umeme, huduma za Bima, Huduma za mawasiliano na mtandao, kandarasi za ujenzi wa Mabarabara na Huduma za uuzaji mafuta.
Alitaja fursa nyingine zitakazopatikana kuwa ni Karakana za ukarabati wa mashine mbali mbali na magari, Huduma za sheria, Huduma za Mawasiliano na Kandarasi za kusamba vifaa vya ujenzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara, Dkt. Gideon Kaunda akiongea kwa niaba ya wafanyabiasahara hao aliishuukuru Serikali kwa kuamua kuwashirikisha katika suala hilo muhimu kwa manufaa ya nchi na kuahidi kushirikiana nayo ili kuhakikisha kuwa lengo la Serikali la kuhakikisha bomba hilo la Mafuta linapita Tanzania linafanikiwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justin Ntalikwa akiongea na baadhi waandishi wa habari mara baada mkutano ya wafanyabiashara wa sekta ya mafuta nchini leo jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Sekta ya Mafuta nchini Dkt. Gideon Kaunda akiongea na baadhi waandishi wa habari mara baada mkutano ya wafanyabiashara wa sekta ya mafuta nchini leo jijini Dar es salaam.Picha na Ally Daud- Maelezo
 

No comments: