Wednesday, March 9, 2016

Prof. Muhongo aagiza Malipo ya Ushuru wa Huduma yafanyike hadharani

 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kutoka kulia) akikata utepe kuashiria ufunguzi wa mgodi. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Zelothe Stephen.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akiwasili katika mgodi wa dhahabu wa Cata Mining. Kulia ni Mkurugenzi wa mgodi huo, Mahuza Nyakirang’ani.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akikagua shughuli zinazoendelea mgodini hapo. Kushoto kwake ni Meneja wa mgodi huo, Peter Bourhill na kulia kwake ni Mkurugenzi wa mgodi,  Mahuza Nyakirang’ani.

 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akisalimiana na baadhi ya wananchi kutoka vijiji vya jirani na mgodi wa Cata Mining waliohudhuria mkutano wake wa hadhara ili kujadili masuala mbalimbali.
 Meneja wa mgodi wa Cata Mining, Peter Bourhill akimweleza jambo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokua akikagua mgodi huo. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa mgodi,  Mahuza Nyakirang’ani.

Prof. Muhongo aagiza Malipo ya Ushuru wa Huduma yafanyike hadharani
Serikali imeagiza ulipaji wa ushuru wa huduma unayofanywa na migodi mbalimbali nchini ufanyike hadharani ili kila mwananchi aelewe kiasi kilicholipwa.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alitoa agizo hilo hivi karibuni alipofanya ziara kwenye mgodi wa dhahabu wa Cata Mining uliopo katika kijiji cha Kataryo, mkoani Mara ambapo vilevile alikagua shughuli za mgodi huo na kuweka jiwe la msingi.Profesa Muhongo alisema ili kuondoa hali ya sintofahamu pamoja na kuongeza uwazi na utekelezaji sahihi wa miradi kutokana na fedha zitokanazo na malipo ya ushuru wa huduma, ni lazima ulipaji huo wa ushuru husika ukashuhudiwa na kila mwananchi.

Aliongeza kwamba wananchi wanapaswa kushirikishwa katika kuibua miradi itakayotekelezwa kwa kutumia fedha hizo za ushuru wa huduma.“Wananchi wanapaswa kuelewa ni kiasi gani kimelipwa; na hiyo haitoshi inatakiwa washirikishwe kwenye matumizi ya fedha hiyo.”

Waziri Muhongo alimuagiza Kamishna wa Madini kuandika barua kuikumbusha migodi yote nchini pamoja na Halmashauri ambazo kuna migodi kufuata utaratibu uliowekwa. “Migodi itaandaa mfano wa hundi ya malipo husika na italipa hadharani kwenye mikutano ya hadhara ili kila mwananchi wa eneo husika ashuhudie, na aelewe kiasi halisi kilicholipwa”.

Alisema baada ya kupokea malipo hayo, wananchi wapewe fursa ya kueleza wanataka fedha hiyo iliyolipwa itumike vipi, ndipo madiwani wajadili utekelezaji wake. “Asilimia 0.3 inayolipwa kama ushuru wa huduma ni lazima iende kwenye miradi ya maendeleo ya maeneo husika na sio vinginevyo” alisisitiza.

Akiuzungumzia mgodi wa Cata Mining, Mahuza Nyakirang’ani ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa mgodi huo alisema unamilikiwa na wamiliki watatu ambapo wawili ni kutoka nchini Tanzania na mmoja kutoka nchini Canada.Alisema gharama zilizotumika katika uwekezaji huo ni kiasi cha Dola za Marekani milioni 54 ambapo baadhi ya fedha ni mikopo kutoka Benki ya CRDB na TIB na fedha zingine zimetolewa na mbia wao wa Canada.

Nyakirang’ani alieleza kuwa mgodi huo ni wa kati na utaanza uzalishaji kwa kutumia marudio ya mchanga wa dhahabu uliochimbwa kipindi cha nyuma na wachimbaji waliokuwepo hapo kipindi cha nyuma na kwa baadaye ndipo wataanza kuchimba rasmi.

Akizungumzia suala la uwajibikaji kwa jamii (CSR), Nyakirang’ani alisema mbali na kwamba mgodi huo haujaanza uzalishaji, lakini umeanza taratibu za kuboresha ujirani mwema kwa kuhakikisha wanachangia katika shughuli za kimaendeleo kwa jamii zinazozunguka mgodi huo.Alisema mgodi huo umejenga madaraja ya kudumu matatu, umeshiriki katika ujenzi wa barabara, shule na zahanati. “Hapo awali ilikuwa mvua zikinyesha watoto wanashindwa kuvuka kuja upande ilipo shule maana hakukuwa na daraja na hivyo maji yalikuwa yakijaa lakini sasa watoto wanakwenda shule bila wasiwasi,” alisema.

Aidha, Profesa Muhongo alifanya mkutano wa hadhara na kuzungumza na wananchi wa vijiji vya maeneo ya jirani na mgodi huo ambapo aliagiza wamiliki wa mgodi huo kutoa ajira bila upendeleo kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo hususan zile ambazo hazihitaji utaalamu.Katika hatua nyingine, waziri Muhongo alipongeza uanzishwaji wa mgodi huo na kuahidi kwamba Serikali itatoa ushirikiano katika hatua mbalimbali na vilevile aliwaasa wamiliki wa mgodi huo pamoja na wananchi wanaoishi maeneo hayo kujenga mahusiano mazuri.

No comments: