Tuesday, March 15, 2016

MWANAMKE WA AFRIKA BADO ANAKABILIWA NA CHANGAMOTO - WAZIRI UMMY MWALIMU

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Ally Mwalimu ( Mb) akitoa hutuba kwa niaba ya Kundi la Nchi za Afrika wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 60 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Wanawake ( CSW).Mkutano huu wa wiki mbili unawakusanya wawakilishi kutoka serikali mbalimbali duniani na Asasi za Kiraia ambapo hujadiliana na kubalishana uzoefu na kuelimishana kuhusu hatua mbalimbali ambazo serikali zao zinachukua katika kuboresha maisha ya mwanamke na mtoto wa kike.
Waziri wa Malawi akimpongeza Waziri Ummy Mwalimu mara baada ya hotuba yake aliyoitoa kwa niaba ya Kundi la Nchi za Afrika.
Mhe. Waziri Mwalimu akichangia majadiliano ya Mawaziri yaliyofanyika mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa 60 wa Kamisheni kuhusu hali ya Wanawake. Majadiliano hayo ya Mawaziri yalihusu uimarishaji wa mfumo ya kisheria na kisera kwaajili na utekelezaji wa usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake.
Sehemu ya Washiriki wa Mkutano huo.

Na Mwandishi  Maalum, New York
Wakati mamia ya wanawake   kutoka serikalini na  Asasi za Kiraia  wakiwa wanakutana hapa Umoja wa Mataifa kwa mkutano wao  unaojadili hali yao katika  maeneo mbalimbali. Mamia mengine ya wanawake  hususani  wale  wa Afrika  wanaendelea kukumbana na changamoto lukuki zinazowarudisha nyuma kimaendeleo.

Ni wanawake hao wanaoishi katika  nchi zenye migogoro, vita visivyokwisha, wenye kukabiliwa  na uhaba na ukosefu  mkubwa wa chakula, maji safi na salama,  matatizo yatokanayo na  mabadiliko ya tabia nchi,  ndio ambao  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto,Mhe.  Ummy Ally Mwalimu(Mb) ameitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza kasi ya  ushirikiano ili   malengo mapya ya maendeleo endelevu (Agenda 2030)  yaweze kuwafikia.

Waziri  Mwalimu ametoa wito huo jana jumatatu,  wakati alipotoa hutuba kwa niaba ya nchi Afrika   katika  siku ya  kwanza ya Mkutano wa  60 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya wanawake (CSW) ambao umeanza  hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Changamoto hizo pamoja na nyinginezo nyingi zikiwamo  kutopata fursa ya  huduma za afya ya uzazi  salama, elimu na usawa wa kijinsia  zinamfanya mwanamke wa Afrika ashindwe kushindana na  wanawake wenzie hususani  wale walioko katika  mataifa yaliyoendelea.  

Waziri Mwalimu ambaye anaongoa ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu wa wiki mbili,  alitoa hotuba hiyo kwa  niaba ya nchi za Afrika  kutokana na kwamba Tanzania kupitia  Uwakilishi wake wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ni  Mwenyekiti wa Kundi  la Nchi za Afrika kwa mwezi huu wa March.

Amewaeleza washiriki wa mkutano huo waliofurika katika Ukumbi  Mkuu wa Mikutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kwamba.  Ingawa pamekuwamo na  makubaliano  na  mapendekezo mengi kuanzia yale yaliyofikiwa huko Beijing, bado mwanamke anayeishi katika nchi zenye migogoro na vita barani Afrika  ataendelea kuachwa nyuma na hivyo kukosa fursa ya kushinda na wenzie.

“ Ingawa  vita,   ukame wa kutisha,  ukosefu  wa chakula, ukosefu wa maji safi, ukichanganya na ukosefu wa  fursa za kiuchumi,  kijamii  na kisiasa ni matatizo yanayowakabili watu maskini lakini mwanamke ndiye anayeathirika zaidi” akaeleza Waziri Mwalimiu.

Na kuongeza kwamba Afrika inaendelea kutilia mkazo hoja   ya kuwashirikisha wanawake katika   majadiliano na utoaji wa maamuzi katika masuala yanayowagusa yakiwamo masuala yanayohusu mabadiliano ya tabia nchi na usuluhishi wa migogoro. 

Akaeleza kwamba,  nchi zinazoendelea na zilizoendelea   zinapashwa  kuongeza kasi ya ushirikiano  na ubia  baina yao ili kufanikisha utekelezaji  Agenda 2030), Makubaliano  juu  Mabadiliko ya  Tabia nchi yaliyofikiwa  huko Paris Ufaransa mwaka jana   na  makubaliano  yaliyofikiwa na waafrika wenye kupitia Ajenda 2063 , ili  katika umoja wake dunia basi iweze kumwondoa mwanamke na jamii nzima kutoka hapa ilipo na kufikia hali bora  zaidi ya maisha.

Kama  hiyo  haitoshi Waziri  amesema, Afrika inaamini pia katika uwezeshwaji wa Sekta binafsi,  kupanua wigo wa  ujasiliamali kama njia moja wapo ya kukuza uchumi endelevu , usawa wa kijamii,  usawa wa jinsia, ulinzi wa mazingira na uwezeshaji wa mwanamke. 

Mada kuu ya Mkutano wa 60 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Wanawake, ni “Uwezeshaji wa Wanawake na uhusiano wake na Ajenda 2030.

Awali akizungumza mwanzoni mwa mkutano huu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki   Moon amasema  tangu alipoingia madarakani mwaka 2006 amejjitadi kuongeza nafasi za viongozi wanawake katika Idara za Sekreatarieti ya Umoja wa Mataifa.

Akitilia msisitizo  hoja na haja ya kupanua wigo  wa wanawake kushika nafasi katika ngazi za juu za maamumizi, Ban Ki Moon amesema, ingawa  nchi nyingi  zimejitahidi sana kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za juu za uongozi bado kuna  Nchi Tano ambazo hazina wanawake katika  Mabunge  yao    ili hali Nchi nyingine 7 hazina mawaziri wanawake katika serikali zao.

Naye  Rais wa Baraza Kuu la 70 la  Umoja wa Mataifa  Bw Monges Lykketoft, akizungumza wakati wa mkutano huo,  pamoja na kusisitiza umuhimu wa utekelezaji wa Agenda 2030 ambayo ameitaja  kuwa ni jumuishi ameendelea kupigia  chapuo la kutaka   Katibu Mkuu  ajaye wa Umoja wa Mataifa awe  Mwanamke.

No comments: