Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akisalimiana na wananchi wa kijiji cha Seka na wafanyakazi wa mgodi wa dhahabu wa MMG Gold Mine Ltd mara baada ya kuwasili mgodini hapo
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kutoka kushoto) akimsikiliza Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya dhahabu ya MMG Gold Mine Ltd, Harrison Abraham (kulia).
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akikagua mgodi wa dhahabu wa MMG Gold Mine Ltd. Kushoto ni Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Harrison Abraham (kulia).
Baadhi ya mitambo ya kuchenjulia dhahabu iliyopo katika mgodi huo wa MMG Gold Mine Ltd uliopo katika kijiji cha Seka, wilaya ya Musoma.
Serikali imetoa miezi minne kwa mgodi wa dhahabu wa MMG Gold Ltd uliopo katika kijiji cha Seka wilaya ya Musoma kuanza uzalishaji vinginevyo itafutiwa leseni.
Agizo hilo limetolewa hivi karibuni na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipofanya ziara mgodini hapo kwa lengo la kujionea shughuli zinazoendelea katika mgodi huo.
Awali Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Viktoria Mashariki, Mhandisi Juma Sementa alisema leseni ya mwanzo kutolewa kwa mgodi huo ilikua mwaka 2002 ambapo Kampuni ya awali ilikuwa JMG Exploration Co. Limited ambayo ilifanya utafutaji wa madini kuanzia mwaka 2002 hadi 2005.
Mhandisi Sementa aliongeza kuwa baada ya hapo eneo hilo lilibaki chini ya maombi ya makampuni na watu binafsi mbalimbali bila kutolewa Leseni ya utafutaji wa madini hadi mwaka 2011 ambapo kampuni ya MMG ilipata leseni ya utafutaji wa madini na mwaka huo huo tarehe 8 Desemba ilipatiwa leseni ya uchimbaji wa madini namba ML.449/2011.
Akizungumzia muda huo tangu kutolewa kwa leseni husika, Profesa Muhongo alisema ni mrefu na ilipasa kampuni hiyo iwe imeanza uzalishaji. "Haiwezekani muda wote huo tangu leseni imetolewa mgodi upo tu na hakuna kinachozalishwa."
Aliagiza hadi kufikia tarehe 15 Julai mwaka huu mgodi huo uwe umeanza uzalishaji vinginevyo kampuni hiyo itapewa notisi ya kusimamisha shughuli zake na kuondoka mgodini hapo.
Mbali na hilo, waziri Muhongo aliiagiza kampuni hiyo kuhakikisha inalipa kodi na tozo mbalimbali za Serikali kama sheria inavyoagiza.
Akitetea hali hiyo, Mkurugenzi Mkuu na Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Harison Abraham alisema uchelewaji huo umetokana na sababu mbalimbali mojawapo ikiwa ni wajiolojia wa kampuni hiyo ambao alisema walikuja na kampuni yake kutoka nchini Urusi na Armenia kushindwa kumaliza shughuli za utafutaji kwa wakati.
Aidha, katika ziara hiyo mgodini hapo, Profesa Muhongo alizungumza na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Seka ambao walifika mgodini hapo kwa lengo la kuzungumza nae; walimueleza tofauti zilizopo baina yao na kampuni hiyo.
Ilielezwa kwamba awali kampuni hiyo iliingia mkataba na Serikali ya Kijiji cha Seka ambao unailazimu kampuni hiyo kutekeleza masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi kijijini hapo jambo ambalo wanakijiji hao walisema halijafanyika.
Hata hivyo wanakijiji hao walitofautiana miongoni mwao kwani baadhi yao walisema kampuni hiyo imefanya mambo mazuri ambayo ni pamoja na ukarabati wa shule na barabara.
Akijibu tuhuma hizo, Abraham aliwasihi wananchi hao wawe wa kweli na waeleze mazuri pia yaliyofanywa na kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na ajira zilizotolewa mgodini hapo.
"Wananchi wa Seka ni familia yangu, mbali na kwamba hatujaanza uzalishaji nimekua nikisaidiana nao mambo mbalimbali ya kijamii," alisema.
Akizungumzia mkataba huo, Profesa Muhongo alimuagiza Kamishna Msaidizi wa Madini, Mhandisi Sementa kukutana na viongozi wa kijiji pamoja na wawakilishi wa kampuni husika ili kuujadili.
Aliongeza kwamba huenda mkataba huo ukawa ni batili na hivyo kuna umuhimu wa kuutazama upya ili kuepusha migogoro. "Ikigundulika kama mkataba huo ni batili tutausimamisha."
Vilevile Profesa Muhongo aliwaasa wanakijiji hao kuepukana na tabia za kibaguzi na badala yake kutanguliza mbele haki. Vilevile aliwaagiza viongozi wa Serikali ya Kijiji kufanya maamuzi kwa kushirikiana na wanakijiji na siyo kujiamulia bila ya kuwa na makubaliano ya pamoja.
No comments:
Post a Comment