Watendaji wa Taasisi zilizochini
ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakimpokea na kumkaribisha
kuanza kazi Ofisini kwake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi baada ya kuteuliwa tena na Rais wa Zanzibar kuendelea kushika wadhifa huo
katika kipindi cha Pili cha Awamu ya Saba.
Katibu wa Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Abdullah Ali Abdullah { Kitole } aliyeinama akinong’onezana
kitu na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Ahmad
Kassim kwenye hafla ya kupokea Balozi Seif kuanza rasmi majukumu yake Vuga
Mjini Zanzibar.
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Ahmad Kassim akimpongeza Balozi Seif kutokana
na juhudi zake zilizopelekea watendaji wa ofisi yake kupata mafanikio makubwa
ndani ya kipindi cha uongozi wake wa miaka mitano iliyopita.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif akiwashukuru watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi
yake baada ya kufanyakazi pamoja atika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alisema Watendaji wa Taasisi za Umma Nchini wanapaswa kuwa makini katika
kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha kwenye Taasisi zao ili kuipa nguvu
Serikali kuu kuvuka vyema katika kipindi hichi cha mpito.
Alitahadharisha kwamba kipindi hichi hali ya fedha
si nzuri kutokana na mambo mengi yaliyofanywa
katika kipindi kifupi kilichopita ikiwemo suala la uchaguzi Mkuu ambalo
limelazimika kutumia fedha nyingi.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati
akizungumza na Wawakilishi wa watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake walipompokea
rasmi kuingia ofisini kwake na kuanza kazi mara baada ya kuteuliwa tena na Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein kushika
wadhifa huo katika kipindi chengine cha miaka mitano ijayo.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga
kuendesha Taasisi zake za Umma kwa kutumia fedha inazokusanya kupitia vianzio
vyake mbali mbali chini ya usimamizi wa watendaji watakaoonyesha uadilifu
kwenye usimamizi huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea
kuchukiwa kwake na baadhi ya watendaji wa Umma wenye tabia mbaya ya kuwekeana
chuki katika utekelezaji wa majukumu yao yanayowakabili ya kila siku.
Balozi Seif alisema tabia hiyo potofu inayolaaniwa hata katika imani na Vitabu vya
Kidini ikiachiliwa kuendelea hatma yake inaweza kuzaa uadui utakaoleta
hasara kubwa hapo baadae.
Aliwapongeza na kuwashukuru Viongozi pamoja na
watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake kwa kazi kubwa waliyoifanya
iliyomuwezesha kutekeleza majuku yake ya ufanisi mkubwa ndani ya kipindi cha
miaka mitano ya uongozi wake.
Balozi Seif aliwanasihi Viongozi na watendaji hao
kuendelea kushirikiana na kushikamana kwa kufanya kazi kama ndugu wamoja ili
kazi ya Utumishi waliokabidhiwa na Taifa ifikie malengo yaliyokusudiwa.
Alisema zipo kasoro, changamoto na hata mikwaruzano
iliyojitokeza na kupelekea kukoseana baina ya baadhi ya watendaji na Viongozi
hao akiwemo na yeye pia ndani ya kipindi kilichopita cha miaka mitano. Hivyo
njia pekee ya kuzishinda changamoto na kasoro hizo ni kusameheana ili kufuta
kasoro hizo.
Mapema Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Nd. Ahmad Kassim kwa niaba ya watendaji wa Ofisi hiyo
amempongeza Balozi Seif kwa kuteuliwa tena kushika wadhifa huo.
Nd. Ahmad alisema ndoto na dua za Viongozi na
Watendaji wa Taasisi za Ofisi hiyo zimesibu kwa Mwenyezi Muungu aliyempa ilham
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein
kumteua tena Balozi Seif kuendelea kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Alisema ahadi waliobeba Viongozi na Watendaji wa
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ni kushirikiana nae bega kwa bega
kadri ya uwezo wao kiutendaji ili kufanikisha majukumu yao kwa upeo mkubwa
zaidi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
31/3/2016
No comments:
Post a Comment