Friday, March 18, 2016

KATIBU MKUU IKULU AKABIDHI GARI JIPYA LA WAGONJWA KWA HOSPITALI YA WILAYA YA CHALINZE KWA NIABA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT. JOHN POMBE MAGUFULI IKULU JIJINI DAR ES SALAAM.

 Katibu Mkuu wa Ikulu Peter Ilomo akimkabidhi funguo za gari jipya la wagonjwa Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya shughuli ya  kubebea wagonjwa katika hospitali ya Wilaya ya Chalinze. Tukio hilo lilifanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete akipokea na kuangalia nyaraka za gari hilo la kubebea wagonjwa kutoka kwa Katibu Mkuu wa Ikulu Peter Ilomo.
 Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete akishukuru mara baada ya kukabidhiwa gari la kubebea Wagonjwa na Katibu Mkuu wa Ikulu Peter Ilomo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa  Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete akiwasha gari jipya la Wagonjwa lililotolewa na na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya kubebea wagonjwa katika hospitali ya Wilaya ya Chalinze.
 Sehemu ya Ndani ya gari hilo kama inavyoonekana .
 Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete akiendesha gari hilo la wagonjwa lililotolewa na na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya kubebea wagonjwa katika hospitali ya Wilaya ya Chalinze.
 Gari  jipya la Wagonjwa lililotolewa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Chalinze kama linavyoonekana kwa nyuma.
 Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete akifurahia mara baada ya kukabidhiwa Gari hilo la Wagonjwa.
Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete akishukuru mara baada ya kukabidhiwa gari na Katibu Mkuu Ikulu Peter Ilomo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Afisa Usafirishaji wa Ikulu  Athuman Natepe wakwanza kushoto, Mwenyekiti wa Wilaya ya Chalinze Said Omar Zikatimu wapili kutoka kulia na Dkt. Nasoro Ally Matuzya wakwanza kulia. Picha na IKULU




Rais wa Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amekabidhi  gari la kubebea wagonjwa kwa hosipitali ya wilaya ya Chalinze, Ikiwa ni utekelezaji wa ilani na  ahadi ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi CCM kwa wananchi ikiwa ni pamoja na wa jimbo la Chalinze.

Gari hilo la kubebea wagonjwa limekabidhiwa kwa niaba ya Rais, na Katibu Mkuu Ikulu Peter Ilomo kwa  Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam.           

Akizungumza mara baada ya kukabidhi gari hilo, Katibu Mkuu Ikulu Ndugu Peter Ilomo amesema gari hilo limetolewa na Mheshimiwa Rais kwa hosipitali hiyo ikiwa ni kuitikia wito na utekelezaji wa ilani na ahadi ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi CCM ya kuboresha huduma ya afya kwa wananchi wake kote nchini. Aidha, Ndugu Ilomo amewaomba viongozi wa jimbo la Chalinze kulitumia gari hilo kwa matumizi yaliyokusudiwa ya kuwahudumia wananchi wa eneo hilo.

Akipokea gari hilo kwa niaba ya wananchi wa jimbo na  Wilaya ya Chalinze, Mbunge wa jimbo la Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete amemshukuru Mheshimiwa Rais    Dkt. John Pombe Magufuli kwa msaada huo na kuahidi kulitumia gari hilo kwa malengo yaliyokusudiwa, na kusema kuwa, utendaji kazi wa Rais Magufuli umekuwa ukiungwa mkono na wananchi wa kada mbalimbali na kuwaomba watanzania kuzidi kumuombea kwa Mungu.

Kwa upande wake Dakta Nasoro Ally Matuzya, amesema gari hilo limekuja kwa wakati muafaka kwa kuwa umezingatia utekelezaji wa malengo ya Milenia hususan lengo namba nne  linalosisitiza kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano

Naye Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Chalinze Ndugu Saidi Omar Zikatimu amesema gari hilo la kubebea wagonjwa litakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa jimbo hilo la Chalinze hususan katika kusaidia kutoa wagonjwa ambao wako katika maeneo ya vijijini wilayani humo na kuwafikisha katika hospitali ya Chalinze na hivyo kunusuru maisha yao kwa kupata huduma za afya kwa haraka.

Mbali na Wilaya ya Chalinze kupata msaada wa gari hilo la kubebea wagonjwa, tayari magari mengine mawili ya kubebea wagonjwa yameshakabidhiwa katika vituo vya afya vya Kiroka na Kisemu mkoani Morogoro.

Hospitali mpya ya Wilaya ya Chalinze imepanda hadhi kutoka kituo cha Msoga ambayo ilikuwa haina gari la kubebea wagonjwa na hivyo kufanya usafirishaji wa wagonjwa kutoka hospitali hiyo hadi hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi au kutoka maeneo ya vijijini kuwa mgumu.

 
Imetolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu

18 Machi 2016. 
  

No comments: