Saturday, March 19, 2016

JOPO LA NGAZI YA JUU KUHUSU UWEZESHAJI WANAWAKE KIUCHUMI LAZINDULIWA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon (katikati) akiwa na wenyeviti wenza wa Jopo a ngazi ya juu kuhusu uwezeshaji wa wanawake kiuchumi pamoja na baadhi ya wajumbe wa Jopo siku ya uzinduzi wa Jopo hilo uliofanyika sambamba na mkutano wa 60 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Wanawake (CSW) unaoendelea hapa Umoja wa Mataifa
Wenyeviti -Wenza wa Jopo la Ngazi ya Juu kuhusu Uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, Rais wa Costa Rica, Mhe. Luis Guillerma Solis na Mkurugenzi Mtendaji wa IKEA Switzerland Bi. Simona Scarpaleggia wakibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Kundi la Nchi za Afrika katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi, mara baada ya kundi hilo kuzinduliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, mapema wiki hii. Mmoja wa wajumbe wa Jopo ambao idadi yao ni 21 ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Hassan Suluhu. Ban Ki Moon ameunda Jopo hilo ili limpatie maoni na mapendekezo kuhusu uwezeshwaji wa mwanamke kupitia utekelezaji wa Agenda 2030 ya Maendeleo Endelevu.

Na Mwandishi Maalum, New York

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amezindua Jopo la Nganzi ya Juu ambalo ameliunda kusaidia kufanya uchambuzi na kutoa mapendekeo ya namna ya kuchagiza kasi ya kuwawezesha Wanawake Kiuchumi.

Jopo hilo ambalo linaundwa na viongozi na wataalamu wa kada mbalimbali linaongozwa na WenyeViti -Wenza ambao ni Rais wa Costa Rika, Mhe. Luis Guillerma Solis na Bi. Simona Scarpaleggia ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa IKEA Switzerland.

Wajumbe wa Jopo ni pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Hassan Suluhu, Mkuu wa Banki ya Dunia, Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Fedha ( IMF) Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Mkurugenzi Mtendaji wa UN- WOMEN, wapo pia Maprofessa na wataalamu wa uchumi, watafiti, viongozi wa vyama vya wafanyakazi, wawakilishi kutoka serikalini, wataalamu wa masuala ya jinsia na fursa sawa na wafanyabiashara. Kwa pamoja jopo hilo linakuwa na wajumbe 21.

Mara baada ya kuzinduliwa rasmi kwa Jopo hilo, Marchi 15 sambamba na Mkutano wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya wanawake. Wenyeviti- wenza walianza ratiba ya kukutanana na Wenyeviti wa Makundi ya Kikanda ya Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa madhamuni ya kupata ushauri na mawazo yao ya awali kuhusu mapendekezo ya nini Jopo hilo linatakiwa kuzingatia katika utafiti wake na hatimaye kile kitakachoingizwa kwenye andiko lao.

Mwenyekiti wa Kundi la nchi za Afrika, kwa mwezi Marchi, Balozi Tuvako Manongi alikuwa miongini mwa wenyeviti waliokutana na wenye-viti wenza wa Jopo, ambapo aliwasilisha baadhi ya maeneo ambayo Afrika inaamini kwamba yakiendelea kutiliwa mkazo yatachagiza kasi ya kuwainua wanawake kiuchumi.

Baadhi ya maeneo hayo ni fursa ya wanawake kupata elimu pamoja na elimu ya juu, upatikanaji wa mitaji na mikopo, nafasi za uongozi zikiwamo za kisiasa, umiliki wa mali na haki ya kumiliki ardhi, afya ya uzazi na uzazi wa mpango na salama, kuondokana na umaskini na affirmative action na fursa za kupata misaada na ushauri wa kisheria.

Balozi Manongi amewaeleza wenye-vita wenza wa Jopo kuwa mapendekezo anayowasilisha kwa niaba ya nchi za Afrika si mpya kwani yanaendelea kufanyiwa kazi na serikali mbaliambali. Lakini ni Imani ya Afrika kwamba kama yakiendelea kupewa msukumo unaostahili pamoja na mengine yatakayokuwa yanawasilishwa kwa Jopo bila shaka kasi ya uwezeshwaji wa wanawake kiuchumi itakuwa kubwa zaidi.

Jukumu la Jopo hilo la Uwezeshwaji wa Wanawake kiuchumi pamoja na mambo mengine ni kutoa mapendekezo kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya uwezeshwaji wa wanawake kupitia utekelezaji wa Ajenda 2030 ya Maendeleo Endelevu kwa kuboresha matokeo ya kiuchumi kwa wanawake, kupaisha uongozi wa wanawake katika kusukuma mbele ajenda 2030 ambayo ni jumuishi, endelevu na inayojali mazingira.

Vile vile Jopo litatakiwa kutoa mapendekezo ambayo watendaji na watoa maamuzi serikalini, katika sekta binafasi, Taasisi za Umoja wa Mataifa, na wadau wengine wataweza kuyafanyia kazi. Ripoti ya kwanza Jopo inatarajiwa kuwasilishwa mwezi Septemba 2016.

No comments: