Wednesday, March 30, 2016

JAJI MKUU WA TANZANIA AFANYA ZIARA YA KUTEMBELEA MAHAKAMA KATIKA MIKOA YA IRINGA, NJOMBE NA RUVUMA, AISIFU MAHAKAMA KANDA YA SONGEA KWA KUFANYA VIZURI.

Na Mwandishi Wetu, Mahakama ya Tanzania.

Mahakama ya Tanzania ni moja kati ya Taasisi iliyopo katika mchakato wa kuboresha huduma zake. Katika kufanikisha azma hii jitihada/maboresho mbalimbali yameendelea kufanyika ili kuwezesha Mhimili huu muhimu kuwa na mazingira rafiki ya utoaji haki kwa wananchi.

Hivi karibuni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman alitembelea katika Mahakama za mikoa ya Iringa, Njombe pamoja na Ruvuma, lengo la ziara ikiwa ni kukagua na kujionea hali ya utendaji wa Mahakama na mwenendo wa uendeshaji wa mashauri.
 Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania akiweka sahihi katika kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Mahakama ya Wilaya ya Songea.
 
Katika ziara yake Mhe. Jaji Mkuu alipata nafasi ya kutembelea Mahakama Kuu Songea, Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea, Mahakama ya Wilaya Songea. Mahakama ya Wilaya Mbinga, Mahakama ya Wilaya Nyasa inayotarajiwa kuanza kazi hivi karibuni na baadhi ya Mahakama za Mwanzo.

Mhe. Jaji Mkuu aliongozana na Watendaji wengine wa Mahakama katika ziara yake ambao ni; Mtendaji Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Msajili Mkuu pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Wote walipata fursa ya kujionea hali halisi ya miundo mbinu ya Mahakama ikiwa ni pamoja na kupata taarifa za Mahakama hizo kutoka kwa Jaji Mfawidhi/Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hizo.
 Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania (wa kwanza kushoto) akipata taarifa fupi ya Mahakama Kanda ya Songea kutoka kwa Mhe. John S.Mgetta, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Songea (aliyesimama), mara baada ya kuwasili Mahakama Kuu kanda ya Songea.

Akisoma taarifa yake mbele ya Mhe. Jaji Mkuu, Mhe. John Mgetta, Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Songea alisema kuwa Kanda yake ina Mahakama Kuu moja (1), Mahakama ya Hakimu moja (1) ya Mahahakama za Wilaya tano (5) ambazo ni Songea, Namtumbo, Tunduru, Mbinga na Mahakama ya Wilaya Nyasa.

Hata hivyo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Mhe. John Mgetta alikiri Mahakama yake kukabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi hususani Makarani na ubovu wa majengo ya Mahakama, kwani hayatoshi na ni machakavu.

Mhe. Jaji Mkuu, Kanda ya Songea inakabiliwa na uhaba wa watumishi, hususani makarani. Ukiachia mbali changamoto hii tunakabiliwa pia na uchakavu wa miundombinu ya majengo.
 Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania (kushoto), Mhe. John S.Mgetta Jaji Mfawidhi Kanda ya Songea (kulia), wakisoma majalada ya kesi katika Mahakama ya Mwanzo Kigonsera mkoani Songea.

 “Mhe. Jaji Mkuu, majengo mengi yanayotumiwa na baadhi ya Mahakama mfano Mahakama Hakimu Mkazi na Wilaya za Songea pamoja na Mahakama nyingi za Mwanzo ni ya kuazima. kwa ujumla hali ya majengo ya Mahakama katika Kanda hii si ya kuridhisha, Mahakama nyingi zina majengo mabovu sana, hasa Mahakama za Mwanzo, ama yanahitaji ukarabati mkubwa au kubomolewa na kujengwa upya,” alieleza Mhe. Jaji Mgetta.

Licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa, Mahakama Kanda ya Songea ni moja ya Kanda inayoongoza nchini kwa umalizaji wa Mashauri yanayofunguliwa katika Mahakama mkoani humo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Tehama, Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba alisema kwa mujibu wa Takwimu za uondoshaji wa Mashauri nchini, Kanda ya Songea ndio inayoongoza kwa kasi kubwa ya kumaliza kwa wakati kesi zinazofunguliwa.

“Napenda nikiri kuwa Kanda ya Songea ndio Kanda inayoongoza kwa uondoshaji wa Mashauri, hii inatokana na jitihada zifanywazo na Majaji na Mahakimu wa Mahakama katika kanda hiyo,” alisema Essaba.
Aliongeza kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Songea ina jumla ya Majaji wawili tu na kuongeza kuwa kila Jaji anawastani wa mzigo wa kazi (work load) wa kesi 215 kwa kila mmoja. 

Alisema; uwezo wao wa kumaliza mashauri yanayofunguliwa (clearance rate) ni 154% na kila kesi iliyofunguliwa ilimalizika kwa wakati kwa asilimia 100% huku wakiendelea kutoa maamuzi ya kesi za zamani kwa asilimia 54%.
Kwa upande wa Mahakama ya Mkoa/Hakimu Mkazi, Mkurugenzi Msaidizi huyo alisema Mahakama hiyo haina kesi yenye Zaidi ya miezi 18 Mahakamani na kuongeza kuwa Mahakama hiyo ina jumla ya Mahakimu wanne (4) wenye wastani wa mzigo wa kazi wa kesi 117 na uwezo wao wa kuondoa mashauri yanayoingia ni asilimia 112, na kuongeza kuwa utendaji huu unarudisha Imani ya Mahakama kwa wananchi.

Bw. Essaba aliendelea kueleza juu ya utendaji wa Mahakama katika Kanda ya Songea, kwa kuongeza kuwa kuna jumla ya Mahakama za Wilaya nne (4) Mahakama zote zikiwa na jumla ya Mahakimu sita (6) na kila mmoja ana wastani wa mzigo wa kazi ‘workload’ wa kesi 186 na uwezo wao wa kuondoa kesi zinazofunguliwa ni asilimia 135 na kupelekea kumaliza mlundikano wa mashauri katika Mahakama hizo.

Bw. Essaba alimaliza kwa kuongelea juu ya Mahakama za Mwanzo zilizopo Kanda ya Songea ambazo jumla yake ni 45 na kuongeza kuwa Mahakama hizo zina jumla ya Mahakimu 52 ambapo kila mmoja ana mzigo wa kazi wa kesi 157 na uwezo wao wa kuondoa kesi zinazofunguliwa kwa Mahakama zote za Mwanzo ni 104.

“Hakuna kesi/shauri lolote lililokaa kwenye Mahakama hizo zaidi ya mwaka mmoja, kwa ujumla Kanda ya Songea ni moja ya kielelezo cha utendaji uliotukuka katika Mahakama ya Tanzania,” alisisitiza Essaba.

Hata hivyo; Mahakama ya Tanzania kwa ujumla wake ipo katika mchakato wa maboresho, ulioanza muda wa takribani miaka mitatu sasa wa kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kuondosha mashauri ya muda mrefu Mahakama na kutoruhusu Mashauri kukaa Mahakamani Zaidi ya miaka miwili (2).

Kwa upande wake Mhe. Jaji Mkuu, aliupongeza uongozi wa Mahakama Kanda ya Songea kwa jitihada zao za dhati katika kuhakikisha wanatoa haki kwa wakati, na kuongeza kuwa hali hii inawapa Imani wananchi na kuifanya Mahakama kuwa kimbilio lao katika upatikanaji wa haki.
Kwa upande wao Watendaji walioambatana na Mhe. Jaji Mkuu katika ziara yake walisema wamefarijika sana na kasi ya Kanda ya Songea kwa uondoshaji wa Mashauri na kudai kuwa hali hii imesababisha hata idadi ya wafungwa/mahabusu gerezani kupungua.
 Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revocati, akipitia jalada moja baada ya jingine kuona hali halisi ya utoaji haki kwa Wananchi katika Mahakama ya Mwanzo Kigonsera mkoani Songea.
“Binafsi nimefarijika sana na mabadiliko tuliyoyaona Songea, idadi yawafungwa imepungua ghafla na wananchi walio wengi wanaonekana kufurahia na kusifu jitihada hizi za Mahakama mkoani Ruvuma,” alisema Mhe. Katarina Revokati, Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania.
Pamoja na jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanyika kuboresha huduma za Mahakama nchini, Mhe. Jaji Mkuu aliwasihi watumishi kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia misingi na kanuni zilizowekwa.
 Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania, (katikati), Mhe. John Mgetta, Jaji Mfawidhi- Mahakama Kuu Kanda ya Songea (wa pili kushoto), Mhe. Salima Chikoyo, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Mhe. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu-Mahakama ya Tanzania (wa kwanza kushoto), Mhe. Katarina Revocati, Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania (wa kwanza kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wa Mkoa wa Songea.

No comments: