Saturday, March 5, 2016

HALMASHAURI YA WILAYA YA MANYONI INAAONGOZA KWA KUSHINDWA KUSHUGHULIKIA KIKAMILIFU KERO ZA WALIMU WA WILAYA HIYO

 Ni Majengo ya ofisi za muda za Halmashauri ya Itigi 
 Baadhi ya walimu wa shule za msingi na sekondari wa Halmashauri ya Itigi,wilayani Manyoni,Mkoani Singida wakiwa katika ukumbi wa mkutano wa shule ya msingi Itigireli wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa CWT.
 Katibu wa idara ya Utumishi wa walimu(TSD) Mkoa wa Singida,Bwana Ole Saitabau(anayeandika mahudhurio katika kitabu) na kulia kwake ni kaimu afisa elimu Mkoa wa Singida. 
 Naibu katibu Mkuu wa CWT,Bwana Eliezer Oluoch akizungumza na walimu wa shule za msingi na sekondari wa Halmashauri ya Itigi.(Picha zote Na Jumbe Ismailly) 

Na Jumbe Ismailly,Itigi        
WILAYA ya Manyoni,Mkoani Singida inaongoza Mkoani hapa kwa kushindwa kushughulikia kero zinazowakabili walimu wa wilaya hiyo,na hivyo kusababisha malalamiko yasiyofanyiwakazi kuongezeka siku hadi siku.
Hayo yamebainishwa na walimu wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Itigi na Halmashauri ya wilaya ya Manyoni waliohudhuria katika kikao kilichoandaliwa rasmi kuonana na Naibu katibu mkuu wa cwt alikuwa na ziara ya siku moja wilayani Manyoni.
Wakizungumza kwa hasira kali kutokana na matatizo yao wanayowasilisha kwa afisa utumishi wa wilaya ya Manyoni na kwa katibu wa idara ya utumishi (TSD) wilaya hiyo,walimu hao wameweka wazi kwamba imekuwa ni kawaida kwao kunyanyaswa na watendaji hao wawili kila wanapokwenda kupeleka matatizo yao.
Mmoja wa walimu hao ambaye pia ni mratibu elimu wa kata ya Tambukareli,katika Halmashauri ya Itigi,Edsoni Nkinga alisema kwamba wamefurahia kusikia kati ya Halmashauri zenye matatizo Manyoni inaongoza kwa kushindwa kusikiliza na kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya walimu wa wilaya hiyo.
“Kwanza nimefurahi kusikia kwamba kati ya wilaya ambazo zina matatizo ya kutoshyghulikiwa kero za walimu wake ni pamoja na Manyoni ni ya kwanza”alisisitiza mratibu huyo huku akionyesha kukerwa na tabia hiyo ya watendaji wenye mamlaka ya kushughulikia kero zao.
Kwa mujibu wa Nkinga tangu alipoajiriwa mwaka 2005 mpaka sasa anachechemea na mshahara wa daraja la C,licha ya kuandika barua za kukumbushia mara kwa mara na kila anapokwenda kuonana na aidha afisa utumishi wa wilaya,Juliana Lunduma au katibu wa idara ya utumishi wa walimu (TSD)Tatu Chuma huwa hapati ufumbuzi zaidi ya kuelezwa kuwa kuna waraka wa siri ambao haiwezekani yeye kuufahamu.
Hata hivyo wakati walimu hao wakiwasilisha kero zao kwa Naibu katibu mkuu (CWT),msafara uliofuatana na Naibu katibu mkuu wa CWT ulijikuta ukipigwa na butwa baada ya kushindwa kufahamu sababu zilizochangia baadhi ya watendaji katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni,kutoonekana katika ziara ya kiongozi huyo wa kitaifa iliyokuwa na lengo la kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero zilizokuwa zikiwakabili walimu wa wilaya hiyo.
Baadhi ya watendaji hao ambao hawakuweza kuonekana na katika kushiriki ziara ya Eliezer Oluoch ambao unaweza kutafsiri kuwa walisusia ziara hiyo,ni pamoja na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni,Afisa utumishi wa wilaya ya Manyoni,Katibu wa idara ya utumishi wa walimu(TSD) wilaya ya Manyoni,Afisa elimu shule ya msingi wilaya ya Manyoni na afisa elimu shule ya sekondari wa wilaya ya Manyoni.
Mkutano huo ulihudhuriwa na walimu 178 kutoka katika shule 13 za Halmashauri hiyo ambazo ni shule za msingi 10 na shule za sekondari tatu,ulianza mapema kama ulivyotarajiwa na ndipo ulipofika wakati wa kujitambulisha hapakuwa na sababu yeyote ile iliyotolewa kuhusu kukosekana kwa maafisa hao muhimu.
Pamoja na mkutano huo kuwahusu walimu ambao mwajiri wao ni mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni ambako ndiko majalada yao bado yapo huko,lakini kilichowashangaza walimu hao ni kutowaona viongozi hao waliokuwa tegemeo kubwa kwao wakati wa kuuliza maswali.
Lakini yote kwa yote ndipo walimu hao kutoka katika shule za sekondari za Handu,Kimadoi na Itigi huku kwa shule za msingi  ni Mlowa,Bangayega,Itigi,Furaha,Ipande, Kitaraka,Doroto,Pentagoni,Mjimpya pamoja na Itigi reli walianza kuwasilisha kero zao kwa mgeni huyo.
Akifungua mlango wa maswali,Nkinga alikishaiwishi kikao hicho kikubaliane naye kwamba walimu wa Itigi wasiwe tayari kuendelea kuhudumiwa na afisa utumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni,Juliana Lunduma pamoja na katibu wa idara ya utumishi wa walimu (TSD) wilaya ya Manyoni,Tatu Chuma.
Akifafanua kwa niaba ya walimu,mratibu huyo alitaka kufahamu CWT  itawasaidiaje walimu wa Halmashauri ya Itigi kupata haki zao kutokana na kauli chafu wanazopewa huku manyanyaso yakizidi kutoka kwa wasimamizi wa sheria za utoaji haki za walimu zinazopaswa kutolewa na afisa utumishi au afisa wa TSD wilaya ya Manyoni.
“CWT ifanye nini kuhakikisha walimu wale ambao wana matatizo ya madaraja ili waweze kupandishwa mara mbili ?”alihoji mratibu elimu kata huyo.
Naye mwalimu wa shule ya msingi Itigi reli,Mwalimu Devota alielekeza tuhuma zake kwa maafisa wenye dhamana ya kusimamia sheria kwamba pamoja na kusisitizwa kwenda kujiendeleza,hususani wanapokwenda kuchukua masomo ya zaidi ya digrii,huambiwa wamesoma kwa faida yao na hivyo kujikuta hawapandishwi madaraja kama walimu wa vyuoni.
Hata hivyo walimu hao wa shule za sekondari na msingi walitumia mkutano huo kuiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwachukulia hatua(kutumbua majipu watumishi hao),hususani katibu wa idara ya utumishi na afisa utumishi wa wilaya ya Manyoni kwa manyanyaso wanayoyapata wanapokwenda kufuatilia haki zao.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi ulibaini kuwa hata katika mkutano uliofanyika katika shule ya sekondari ya Mwanzi,mjini Manyoni,Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni,afisa elimu msingi,afisa elimu sekondari na katibu wa tsd hawakuweza kushiriki mkutano huo kutokana na kinachodaiwa kuhofia kudhalilishwa mbele ya mgeni huyo wa kitaaifa.
Hata hivyo alipotafutwa katibu wa TSD wilaya ya Manyoni,Tatu Chuma ili aweze kuzungumzia tuhuma zinazomkabili simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa kwa muda wote.

No comments: