Tuesday, February 9, 2016

WAZIRI MAGHEMBE AELEZEA JINSI MAJANGIRI YANAYOTUHUMIWA KUTUNGUA HELIKOPTA YALIVYOKAMATWA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu kukamatwa kwa majangili 9 yanayotuhumiwa kuitungua helikopta ya Doria na kuuawa kwa Rubani Rodgers Gower hivi karibuni katika eneo la Pori la  Maswa na Ranchi ya Wanyamapori ya Mwiba, wilayani Meatu, Mkoa wa Simiyu.  Kushoto ni Mkuu wa Jeshi la Poilisi nchini, IGP, Ernest Mangu na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Ramo Makani (wa pili kulia) na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali, Gaudance Milanzi. (PICHA NA RICHARD MWAIKENDA;KAMANDA WA MATUKIO BLOG)
Waziri Maghembe akisisitiza jambo katika mkutano huo na wanahabari

IGP Ernest Mangu ajibu moja ya maswali hasa kuhusu ushiriki wa jeshi hili katika mapambano ya kuwasaka majangiri nchini
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Milanzi (katikati) akijadiliana jambo na  IGP Mangu (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Wanyamapori wa wizara hiyo.
IGP Mangu akiondoka
Profesa Magembe akimsindikiza IGP Mangu

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU TUKIO LA KUSHAMBULIWA KWA HELKOPTA YA DORIA NA KUUAWA KWA RUBANI ROGERS GOWER TAREHE 29/01/2016

1.0 UTANGULIZI

Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 29/01/2016 lilitokea tukio la kuhuzunisha ambapo majangili walishambulia helikopta iliyokuwa inafanya doria katika maeneo ya Pori la Akiba Maswa na Ranchi ya Wanyamapori ya Mwiba. Shambulio hilo lilisababisha kifo cha Rubani Bw. Rogers Gower raia wa Uingereza na kuharibika vibaya kwa helkopta hiyo baada ya kuanguka. Aidha, katika tukio hilo Bw. Nick Desta aliyekuwa pamoja na Bw. Rogers aliweza kunusurika na kukimbizwa Nairobi kwa ajili ya matibabu zaidi.

Tarehe 30/01/2016 nilitembelea eneo la tukio ili kujionea hali halisi na kutoa tamko la serikali. Haiyumkini, kutokana na kuguswa na kadhia hiyo, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John P. Magufuli alitoa maelekezo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii ya kuanza kufanya msako haraka wa kuhakikisha kuwa wahalifu hao wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria. Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Major Gen. Gaudence Millanzi akifuatana na Mwenyekiti wa Bodi  ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Major Gen. Hamisi Semfuko na baadhi ya watendaji wa Wizara walitembelea eneo hilo tarehe 02 hadi 03/02/2016.

Napenda kuwajulisha kuwa, katika ziara zote mbili tuliweza kushuhudia namna watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii (Pori la Akiba Maswa, Kikosi Dhidi Ujangili Bunda, Hifadhi ya Taifa Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro)  kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Taifa na vya Mkoa wa Simiyu na Wilaya ya Meatu na Maofisa kutoka Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Viongozi  wa FRIEDKIN CONSERVATION FUND, Bw. Dan Friedkin na Bw.  Pratik Patel na watumishi wengine kwa pamoja walisaidiana sana katika kuendesha msako kwa juhudi kubwa na weledi wa hali ya juu. Kazi hii ilifanyika usiku na mchana katika mazingira magumu na hatarishi. Mara kadhaa watendaji hao wamekuwa wanalazimika kuvuka makorongo na mito yenye maji mengi kwa kuogelea kutokana na mvua zinazoendelea kunyeesha katika maeneo hayo.

Mtakumbuka kuwa taarifa zilizopatikana baada ya tukio hilo la kusikitisha zilibainisha kuwa majangili waliohusika na tukio hilo walikuwa watatu (03) na kwamba walikuwa na bunduki mbili aina ya rifle zenye ukubwa wa mtutu (calibre) wa 303 na .458 mtawalio. Aidha, wakati wa tukio hilo, majangili hao tayari walikuwa wamefanikiwa kuua tembo mmoja na kutoweka na meno yake mawili.

2.0 HATUA ZILIZOFIKIWA:

Kama mlivyosikia kwenye taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, sote kwa pamoja tunafarijika kuwajulisha kuwa jitihada zilizofanyika za kuwasaka wahalifu hao ndani ya kipindi cha wiki moja zimeleta matokeo mazuri ambapo:

  • watuhumiwa wote muhimu (key suspects) waliotajwa kuhusika na tukio hilo wamekamatwa na wote wamekiri kuwepo kwenye tukio. Mmojawapo anatuhumiwa kuhusika moja kwa moja na kufyatua risasi iliyosababisha kuanguka kwa ndege hiyo na hatimaye kifo cha rubani.

  • bunduki mbili zilizotumika aina ya Rifle Calibre 303 na .458 zinazoshukiwa kutumika kwenye uhalifu huo zimekamatwa pamoja na risasi 5 za .458 na moja ya 303;

  • meno mawili ya tembo aliyeuawa siku ya tukio yenye uzito wa kilo 31 yamekamatwa;

  • pikipiki moja ambayo inashukiwa kuhusika katika tukio hilo na matukio mengine ya uhalifu imekamatwa;

  • raia wema wanaendelea kutoa taarifa zinazobainisha kuwepo kwa mtandao mkubwa wa ujangili katika Mkoa wa Simiyu na maeneo ya jirani. Taarifa hizo zimesaidia kupanua wigo wa operesheni na kuwezesha kuboresha mbinu za mapambano dhidi ujangili.

3.0 MPANGO MAHSUSI WA WIZARA KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI  UJANGILI NA USAFIRISHAJI HARAMU WA MAZAO YA WANYAMAPORI NA MISITU

Tukio hili limetoa funzo kubwa kwa nchi yetu na linadhihirisha kuwa hivi sasa  baadhi ya majangili wamefikia hatua ya kujijengea uthubutu na ujasiri wa kutisha.

Kutokana na mazingira haya, Wizara ya Maliasili na Utalii imeamua kurejea (review) kwa haraka na kwa upana zaidi mbinu na mikakati yake ya vita dhidi ujangili wa wanyamapori na mazao ya misitu pamoja na usafirishai haramu wa mazao ya wanyamapori na misitu  kwa kufanya yafuatayo:

  1. Kukamilisha haraka uanzishaji wa Kikosi Maalum cha Kupambana na Uhalifu  wa wanyamampori (Wildlife Crime Unit);

  1. Kikosi hiki kitaundwa kwa kushirikisha Taasisi zote za Wizara (Idara ya Wanyamapori, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS). Aidha, kitafanya kazi kwa karibu na Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Sheria, Mamlaka ya Bandari, Viwanja vya Ndege, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Taasisi za Uhifadhi za ndani na nje ya Nchi na wadau wengine wa Uhifadhi;

  1. Kikosi hiki kitakuwa na jukumu la kuratibu na kufuatilia utendaji wa vikosi vidogo (Taskforce Coordinating Groups TCGs)) vilivyoundwa kwenye kanda nane za kiikolojia (ecosystem approach) ili kukabili kwa haraka nyendo zote za ujangili wa wanyamapori, uvunaji na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na misitu;

  1. Kuharakisha ukamilishaji wa kubadilisha muundo wa utendaji kazi wa Wahifadhi Wanyamapori kutoka mfumo wa Kiraia  kuelekea mfumo wa Jeshi Usu (Paramilitary);

  1. Kuharakisha usimikaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) iliyozinduliwa Oktoba 2015 katika jitihada za kuimarisha na kuboresha uwekezaji binafsi wa Serikali katika maeneo yaliyopo nje na ndani ya Hifadhi za Taifa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorogoro;

  1. Kurejesha utaratibu wa kuwa na kada ya walinzi wa misitu (Forest Rangers) ambao watakuwa na uwezo wa kutumia silaha ambapo pamoja na kudhibiti uvunaji haramu wa misitu, utapanua wigo wa kukabili ujangili katika Hifadhi za Misitu;

  1. Kuishauri serikali kuangalia upya endapo bado kuna sababu za msingi kwa wananchi kuendelea kununua na kumiliki bunduki zenye mitutu mikubwa. Uamuzi huu unatokana na kuongezeka kwa matukio ya kukamatwa kwa silaha hizo zikiwa zinatumika kwenye vitendo vya uhalifu nje ya mikono ya wamiliki halali;

  1. Kuboresha utendaji kazi wa wahifadhi kwa kuwapatia mafunzo ya mbinu mpya za ukusanyaji habari na ufuatiliaji wa nyendo za majangili (intelijensia), kukusanya na kutunza kumbukumbu za ushahidi na kuendesha mashtaka (Inteligence, investigation and prosecution);


  1. Kuimarisha upatikanaji wa vifaa vya kisasa ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau wa uhifadhi katika kuchangia ununuzi/upatikanaji wa vifaa hivyo ili kukabili kasi ya mbinu mpya zinazotumiwa na majangili na wasafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na misitu;
  2.  Kwa kuwa katika Operesheni hiyo, wako Askari wa Wanyamapori wanaotuhumiwa kushiriki katika uhalifu wa kijangili, askari hao watafikishwa katika Mahakama ya kijeshi ili kukabiliana na mashitaka ya kijeshi ya kukiuka kiapo na dhamana waliyopewa.

4.0 HITIMISHO
Napenda kutumia fursa hii kutambua na kuwapongeza watendaji wote, Uongozi wa Mkoa wa Simiyu na Wilaya ya Meatu.  Napenda kupongeza na kuishukuru  Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi, Usalama wa Taifa Shirika la Friedkin Foundation  na  wadau wengine wote walioshiriki katika msako huu hadi kufanikisha na kutimiza azma iliyokusudiwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Watanzania wote wenye mapenzi mema na Taifa letu.

Kama nilivyotangulia kueleza, pamoja na mazingira magumu yaliyojitokeza wakati wa kutekeleza kazi hii, washiriki wote waliweza kuendesha operesheni hii kwa ari kubwa na weledi wa hali ya juu hadi kukamilisha lengo kuu  ndani ya kipindi kifupi. Aidha, naomba kuwashukuru wananchi wote ambao kwa namna ya pekee waliweza kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa muhimu zilizoweza kufanikisha lengo hili.

Pia nawashukuru wadau wote walioweza kutoa michango ya hali na mali kwa watendaji wa operesheni hii. Michango yao ilikuwa chachu kwa washiriki wa operesheni kuwajengea mazingira kuendelea kujituma kwa kupunguza makali ya ugumu wa mazingira wakati wanatekeleza jukumu hili.  Aidha, natoa wito kwa wananchi wote waendelee kuisaidia Wizara katika vita hii kubwa ya kukabili ujangili na usafirishaji haramu wa rasilimali zetu.

No comments: