Thursday, February 25, 2016

Wawekezaji sekta ndogo ya gesi watakiwa kuongeza kasi utekelezaji miradi.

 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akizungumza na wawekezaji wa Makampuni ya utafiti na uchimbaji wa Mafuta na Gesi (hawaonekani pichani). Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Utafiti wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kelvin Komba, wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania TPDC, Dkt.  James Mataragio na kushoto ni  Afisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Albert Diliwa.
 Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt.  James Mataragio (katikati) akiongea jambo wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa kwanza kushoto) na wawekezaji wa Kampuni za kutatifi na kuchimba mafuta na gesi nchini. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Utafiti wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio.

  Baadhi ya Wawekezaji wa Kampuni za kutafiti na kuchimba mafuta na gesi nchini, wakimsikiliza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) wakati wa kikao chake na wawekezaji hao.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Dodsal, K. Surendran, akitoa taarifa ya utafiti kuhusu Kampuni hiyo kugundua gesi eneo la Ruvu. Wengine wanaomsikiliza ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati). Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio (wa pili kulia), Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Utafiti wa TPDC, Kelvin Komba, na kushoto ni Afisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Albert Diliwa.Asteria Muhozya na Zuena Msuya.
Imeelezwa kuwa, Tanzania inahitaji kufanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi kupitia rasilimali ya Gesi asilia ambayo inatajwa kuwa chachu ya ongezeko la nishati ya umeme jambo ambalo litachochea ukuaji wa viwanda nchini.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati akihitimisha vikao vyake na  wawekezaji wa  makampuni   yanayofanya shughuli za  utafiti  na uchimbaji wa   Mafuta na gesi nchini, na kuwataka wawekezaji hao kuongeza kasi ya utekelezaji wa  miradi hiyo kutokana mahitaji ya nishati  hiyo nchini.

Profesa Muhongo aliwaeleza wawekezaji hao msimamo wa Serikali kuhusu nishati hiyo kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda vikubwa na vidogo huku rasilimali ya gesi asilia ikitajwa kuwa injini ya kufikia malengo hayo na kuwataka kuhakikisha kuwa gesi inapatikana nchini.

“Hatujagundua mafuta, lakini tuna hazina kubwa ya gesi ambayo inawezesha kufikia malengo hayo. Ni lazima kampuni hizi zibadili mwenendo wao wa namna ya kufanya kazi. Tunataka kasi zaidi katika suala hili na kuhakikisha gesi inapatikana. Tunataka umeme mwingi unaotokana na gesi, umeme nafuu na wa uhakika,”amesisitiza Prof. Muhongo.

Aliongeza kuwa, Serikali imelenga kujenga viwanda viwili vya Mbolea kutokana na gesi asilia na kuyataja maeneo ambayo viwanda hivyo vitajengwa kuwa ni Kilwa Mkoani Lindi na Mtwara.

Aidha, mbali na kutaja ujenzi wa viwanda vya mbolea, alisema kuwa, mipango mingine ya Serikali ni kujenga mitambo ya kusindika gesi ili pia Tanzania iweze kushindana na nchi nyingine kusafirisha gesi iliyosindikwa nje ya nchi, jambo ambalo litawezesha kupata fedha   nyingi za kigeni.

“Tunataka kujenga mtambo wa kusindika gesi asilia mkoani Lindi. Gharama za ujenzi huo zinatarajia kufikia kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 30, utakuwa mradi mkubwa zaidi na tayari eneo la ujenzi wa mtambo huo limepatikana,” amesema Prof. Muhongo.

Pia alisema kuwa, mipango mingine ni  kutumia gesi majumbani ili kuachana na matumizi ya mkaa ambayo yanatajwa kuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira kwa kukata miti hovyo, na kuongeza kuwa, kwa Mkoa wa Dar es Salaam pekee matumizi ya mkaa kwa siku moja yanafikia kiasi cha magunia elfu hamsini (50,000).

Vilevile, aliongeza kuwa,  gesi asilia ni kichochea kingine muhimu kitakachosaidia kuondokana na umaskini na kuongeza pato la Taifa ikizingatia kuwa, ongezeko la  mahitaji ya kiuchumi linapanda kutokana na kuongezeka la idadi ya watu wa kipato cha kati na kuongeza kuwa, “ tunataka Tanzania iondokane na umaskini kupitia rasilimali za gesi na mafuta”.

Aidha, mbali na nishati ya gesi asilia, Prof. Muhongo aliwaeleza wawekezaji hao kuwa, zipo rasilimali nyingine  ambazo wawekezaji wanaweza kuwekeza nchini na kuzitaja kuwa ni nishati jadidifu, pamoja na vyanzo vingine vya upepo, mawimbi,  umeme wa jua  na makaa ya mawe.

Katika hatua nyingine, Prof. Muhongo aliwata  wawekezaji hao kutoa taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa miradi yao ifikapo tarehe 1 Juni, tarehe 1 Septemba na tarehe 31 Novemba, 2016 na kuongeza kuwa, Serikali itatoa ushirikiano mkubwa kwa kampuni hizo kuhakikisha zinatekeleza mipango yao kwa wakati.

Profesa Muhongo alihitimisha vikao na wawekezaji katika kampuni za utafiti na uchimbaji wa  mafuta na gesi tarehe 24 Februari,2016 ambapo  alianza kukutana na wazalishaji wadogo wa umeme wa chini ya   megawati 20 unaotokana na maji  mwezi Janurari, 2016, na wiki ya kuanzia tarehe 15 Februari,2016  alikutana na wawekezaji mbalimbali wenye nia ya kuwekeza katika sekta ndogo ya umeme.

No comments: