Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
Mnamo tarehe 5 Novemba 2015 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ilishuhudia Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiapishwa kuwa Rais wa Awamu ya
Tano katika sherehe zilizofanyika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam. Huu ndio
ulikuwa mwanzo mpya wa Tanzania ya uwajibikaji na maendeleo ya mtu wa hali ya
chini ambayo watanzania wengi walisubiri kwa muda mrefu vizazi na vizazi
kuiona.
Siku 100 tangu Rais wa awamu ya tano aiingie madarakani mambo
mengi yametiliwa mkazo kama vile Elimu, Afya, Biashara, Viwanda,Kilimo,Ufugaji,Uvuvi
na mengine mengi ambayo serikali imeamua kuyaangalia kiundani zaidi ili
kufanikisha azma yake ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Katika makala hii tuangalie jinsi uongozi wa Serikali ya
Awamu ya Tano katika siku 100 ulivyojikita kuimarisha usafi wa mazingira ili kukabiliana
na magonjwa ya mlipuko yanayotokea mara kwa mara katika mikoa mbalimbali nchini
kwa kuhamasisha usafi katika maeneo hayo. Hapa tunamsikia Mhe. Rais John Pombe
Magufuli akisema, “Hatuwezi kufanya sherehe huku watu wetu bado wanakufa kwa
ugonjwa wa kipindupindu ambao unatokana na uchafu, badala yake nchi nzima
tufanye usafi siku hiyo”.
Kwa kuliona hilo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni
Sefue alitangaza rasmi kuwa siku ya tarehe 9 Desemba mwaka 2015, itakuwa ni
siku ya uhuru na kazi na maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru wa Tanganyika kuwa yatafanyika kwa watu kufanya usafi
katika maeneo yao siku hiyo, ikiwa ni jitihada za Serikali kuimarisha usafi na kupambana
na magonjwa ya mlipuko kama vile Kipindupindu.
Kero ya uchafu ilimfanya Mhe. Rais kufanya tendo la
kihistoria ambalo halijawahi kufanyika kwa takribani zaidi ya nusu karne ya
uhai wa Tanzania. Tukio hili ni kuhamisha maadhimisho tuliozoea ya kuona
gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na halaiki na lakini sasa tunashuhudia
machepe, troli, ndoo, fyekeo na zana nyinginezo za usafi zikitumika siku hiyo.
Ama kweli Dr. Magufuli ni kiongozi mwenye uthubutu.
Katika kufanya usafi kama maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa
Tanganyika, Rais John Magufuli aliongoza
kwa vitendo zoezi la kufanya usafi kama
alivyoelekeza baada ya kufuta shamrashamra za maadhimisho ya siku ya Uhuru, Desemba
9. Rais Magufuli na mkewe Janeth
Magufuli walifanya usafi katika maeneo ya Feri, eneo ambalo liko mita kadhaa kutoka
Ikulu Jijini Dar es Salaam naye Makamu wa
Rais, Samia Suluhu yeye alionekana akifanya usafi katika eneo la ufukwe wa Bahari
wa ‘Coco Beach’na baadae kuelekea maeneo ya Kinondoni Morocco Jijini Dar es
Salaam. Katika maadhimisho hayo, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa
aliunagana na wananchi kufanya usafi katika maeneo ya Kariakoo Jijini Dare s
Salaam. Wizara,Taasisi ,Idara,Wakala wa Serikali ,mashirika binafsi Asasi
zisizo za kiserikali, mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao walishiriki kufanya
usafi katika maeneo mbalimbali katika kutimiza agizo la kuifanya siku ya 9
Desemba iwe ya kufanya usafi.
Baada ya Rais kushiriki katika kufanya usafi,wananchi wengi
walipata mwamko wa kufanya suala la usafi kuwa ni moja ya utaratibu wao wa kila
siku katika maeneo yao hata kwa baadhi ya sehemu kutangaza baadhi ya siku kuwa
ni siku rasmi za kufanya usafi katika maeneo yao na hatimaye Naibu Waziri wananchi
Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luaga Mpina alitangaza kuwa
kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi itakuwa siku rasmi ya kufanya usafi wa
mazingira ili kupambana na magonjwa yanayosababishwa na uchafu kama vile kipindupindu.
Katika kulilipa nguvu swala kuimarisha mazingira kwa kuzingatia
usafi katika maeneo mbalimbali,Halmashauri za Majiji ,Wilaya na Miji zilianzisha faini kupitia sheria ndogo
ndogo zilizopo ili kupambana na uchafuzi wa mazingira unaofanywa kwa makusudi
na baadhi ya watu, na kwa kuanza Halmashauri ya Manispaa ya wilaya ya Ilala
ilitangaza rasmi kwa yoyote atakayekamatwa anatupa taka sehemu isiyostahili
atatozwa faini ya shilingi elfu 50 taslimu na kutangaza kutoa nusu ya fedha ya
faini kama zawadi kwa kuwahamasisha wananchi kutoa taarifa au kufanikisha
kukamatwa kwa mtu atakayevunja Sheria hiyo.
Kamapeni za usafi zilifanyika katika Mikoa,Wilaya ,Miji na Vijiji
nchi kote kwqa wananchi kushirika katika kufanya usafi na kufanya usafi kuwa ni
utamaduni wao na sio mpaka litolewe tamko juu ya kusafisha mazingira
yanayowazunguka, katiak kampeni hii ya usafi siku ya 9 Desemba ilikubwa na
baadhi ya changamoto ikiwa baadhi ya wananchi kutoshiriki kampeni hizo katika
maeneo yao na kuwepo kwa uhaba wa magari ya kuzolea taka katika Halmashauri za
Majiji, Wilaya na Miji iliy osababisha taka kukaa kwa muda mrefu katika baadhi
ya maeneo lakini juhudi toka Halmashauri hizo zilifanyika na kuwezesha kuzolewa
na kutupwa katika madampo husika.
Katika kutekeleza suala la kuimarisha usafi wa mazingira Serikali
kupitia Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na watoto kupitia
waziri wake Mhe. Ummy Mwalimu ilitoa tamko la kupiga marufuku uuzwaji wa
vyakula ovyo katika maeneo yasiyo rasmi na ya wazi na uzwaji wa matunda
yaliyokatwa ikiwa ni jitihada za Serikali kupambana na wafanyabiashara
wasiozingatia kanuni za usafi na Afya ambazo zinaweza kuhatarisha afya za
walaji wa vyakula hivyo ikiwemo mlipuko wa magonjwa kama Kipindupindu.
Kampeni hizo za usafi siku ya 9 Desemba zilileta mafanikio makubwa
katika jamii ya watanzania hususani kuhamasisha tabia ya kufanya usafi katika
maeneo yao ili kuweka mazingira safi na pia kupambana na magonjwa ya mlipuko.Katika
kuweka mazingira safi makampuni mbalimbali yaliunga mkono agizo la Mhe Rais la
kufanya usafi siku ya 9 Desemba na kushiriki katika usafi katika maeneo
mbalimbali nchini.
Baadhi ya makampuni yaliyoshiriki katika kufanya usafi siku hiyo
ya Uhuru wa Tanganyika ni pamoja na Clouds Media Group, Msalaba Mwekundu, Max
Malipo, NSSF, Benki ya Biashara ya Akiba (ACB), Shirika la Afya Duniani (WHO)
na Kliniki ya Tiba Mbadala ya Ifakara Herbalist Clinic waliofanya usafi katika
soko la Tandale., Wwengine ni Mohamed Enterprises Group MeTL Benki ya FNB
waliofanya usafi ufukwe wa Coco,GEPF na kampuni ya Saruji ya DANGOTE walifanya
usafi soko la Mbae Mkoani Mtwara, Airtel Tanzania ilifanya usafi Hospitali ya
Wilaya ya Nzega Tabora, kampuni ya PUMA ilishiriki na kutoa vifaa vya usafi
katika Manispaa ya Temeke na Azania Bank nayo ilitoa vifaa vya usafi na
kushiriki usafi katika Halmashauri ya Mji wa Moshi.
Juhudi zimefanya Wizara inayohusika na Mazingira kwa kushirikiana
na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto katika kutoa elimu
juu ya umuhimu wa kufanya usafi katika mazingira ili kujenga tabia ya kuweka
mazingira safi na kujiweka mbali na magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na
uchafu.
Haya shime Watanzania tumuunge mkono Rais wetu kwa kuufanya usafi
kuwa ni tabia katika maisha ya kila siku ingawa kuna changamoto mbalimbali
zinazokabili maeneo yetu zikiwemo
Halmasahuri za Majiji,Wilaya na Miji katika kutatua changamoto hizo,hivyo basi
hatuna budi kushirikiana na Serikali ya Rais Magufuli kuboresha mazingira yetu
kwa kufanya usafi kwa faidi yetu na vizazi vyetu.
No comments:
Post a Comment