Tuesday, February 16, 2016

MADEREVA WA MAGARI YA JESHI LA MAGEREZA NCHINI WAASWA KUZINGATIA SHERIA ZA USALAMA BARABARANI, MKOANI MOROGORO

Na Lucas Mboje; Morogoro

MADEREVA wote wa magari ya Jeshi la Magereza nchini wametakiwa kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani wakati wote wanapoendesha magari ili kujiepusha na ajali zisizo za lazima.

Rai hiyo imetolewa na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Casmir Minja wakati akizungumza kwenye hafla ya kufunga Mafunzo ya Udereva Kozi ya Msasa kwa Maofisa wa Jeshi la Magereza kutoka Mikoa yote Tanzania Bara yaliyofanyika katika Chuo cha Udereva na Ufundi, Kingolwira Mkoani Morogoro.

Jenerali Minja amewaagiza Wahitimu wa Mafunzo hayo kuhakikisha kuwa wanawajibika pia kuyatunza magari watakayokabidhiwa kuyaendesha ili yaweze kudumu kwa muda mrefu kama ilivyokusudiwa.

"Nawataka mjiepushe na uzembe wakati mnapoendesha magari ya Jeshi letu ikiwa ni pamoja na kutokujihusisha na ulevi na kuendesha magari hayo kwa mwendo kasi bila kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani". Alisema Jenerali Minja.

Aidha Jenerali Minja amezungumzia upungufu mkubwa wa magari katika Jeshi hilo ambapo katika kushughulikia changamoto hiyo Jeshi la Magereza kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa limesaini Mkataba na Kampuni za Ashok Layland na Jeep na magari mia tisa na tano(905) yanategemewa kupokelewa mapema mwanzoni mwa mwezi Mei Mwaka huu.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Udereva na Ufundi Kingolwira, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Osmond Ndunguru kupitia risala yake kwa Mgeni rasmi amesema kuwa Wahitimu hao wamejifunza Mafunzo yote yaliyopo kwenye Mtaala wa Mafunzo ya Udereva kwa nadharia na vitendo ikiwemo mbinu mbalimbali katika fani ya Udereva wa Magari ambapo jumla ya Wanafunzi 125 wamehitimu Mafunzo hayo miongoni mwao Wanaume ni 133 na wa kike ni 2.

Aidha Kamishna Msaidizi wa Magereza, Nduguru alieleza changamoto mbalimbali ambazo Chuo hicho kinakabiliana nazo ikiwemo upungufu wa magari ya kujifunzia pamoja na uchakavu wa miundombinu ya majengo hali inayoathili utoaji taaluma ya mafunzo hayo.

Chuo cha Udereva na Ufundi cha Kingolwira, kilichopo Mkoani Morogoro kinamilikiwa na Jeshi la Magereza ambacho hutoa Mafunzo ya Udereva kwa Maofisa wa Jeshi la Magereza ambao huendesha magari ya Jeshi hilo na katika Taasisi mbalimbali za Umma hapa nchini.
Kamishna Jenerali John Casmir Minja akipokea Salaam ya Utii kutoka kwa Gadi Maalam iliyoandaliwa na Maofisa wa Jeshi la Magereza, Wahitimu wa Mafunzo ya Udereva(hawapo pichani) katika Chuo cha Udereva Kingolwira Mkoani Morogoro. Hafla hiyo imefanyika katika Viwanja vya Chuo hicho 16 Februari, 2016.
Kamishna Jenerali wa Magereza John Casmir Minja akikagua Gadi Maalum iliyoandaliwa na Wahitimu wa Mafunzo ya Udereva katika Chuo cha Uderevau na Ufundi Kingolwira, Mkoani Morogoro.
Wahitimu wa Mafunzo hayo wakipita mbele ya Mgeni rasmi katika mwendo wa kasi kama wanavyoonekana katika picha.
Kamishna Jenerali wa Magereza John Casmir Minja akipokea taarifa fupi Ofsini kwa Mkuu wa Chuo cha Udereva na Ufundi Kingolwira, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Osmond Nduguru(hayupo pichani).
Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja akimtunuku cheti Askari Mhitimu wa Mafunzo ya Udereva kwa niaba ya Wahitimu wote wa mafunzo hayo.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wa Mkoani Morogoro wakifanya Mahojiano Maalum na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja.
Mgeni rasmi, Kamishna Jenerali wa Magereza John Casmir Minja(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wahitimu wa Mafunzo ya Udereva katika Chuo cha Udereva na Ufundi, Kingolwira Mkoani Morogoro.

No comments: