Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akiwa katika kikao na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Ofisi ya Mkuu wa wilaya Tarime na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (wa pili kushoto) kilicholenga kutatua kero wanazokumbana nazo wananchi wanaozunguka mgodi wa dhahabu wa Acacia NorthMara pamoja na Mgodi husika. Kushoto kwa Waziri ni Mkuu wa wilaya ya Tarime, Glorious Luoga. Wa kwanza kulia Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Ziwa Victoria Magharibi, Mhandisi Juma Sementa, Wa pili kulia ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje na Wa kwanza kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Madini, Leseni,John Nayopa.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (kushoto) wakijadiliana jambo mara baada ya kumaliza kikao kilicholenga kutatua kero za wananchi wanaozunguka mgodi wa dhahabu wa Acacia NorthMara pamoja na Mgodi husika.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kulia) akitembelea maeneo yanayolalamikiwa na wananchi wanaozunguka mgodi wa dhahabu wa Acacia NorthMara wakati alipofanya ziara ya kikazi wilayani Tarime. Kulia kwa Waziri ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, na kulia kwa Mbunge ni Mkuu wa wilaya ya Tarime, Glorious Luoga.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akimsikiliza mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Nyakungulu wilayani Tarime ambaye alikuwa akiwasilisha kero za wananchi wanaozunguka mgodi wa dhahabu wa Acacia North Mara wakati Profesa Muhongo alipofanya ziara ya kikazi wilayani Tarime.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa kwanza kulia) akioneshwa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga baadhi ya nyumba zinazodaiwa kutegeshwa kwa ajili ya kulipwa fidia katika moja ya maeneo yanayozunguka mgodi wa Dhahabu wa Acacia North Mara. Profesa Muhongo alifika katika eneo la Nyamongo linalozunguka mgodi huo ili kuzungumza na wananchi na kukagua athari ambazo zinadaiwa kusababishwa na mgodi katika eneo hilo.
Na Teresia Mhagama, Tarime
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameipa siku 30 Kamati aliyoiunda ya kutathmini kero za wananchi wanaozunguka mgodi wa dhahabu wa Acacia North Mara ambapo Kamati hiyo inatakiwa kutoa ripoti tarehe 23 Machi 2016.
Kamati hiyo itakuwa na makundi mawili yatakayofanya kazi sambamba kwa kuzunguka katika vitongoji tofauti vinavyozunguka mgodi kuanzia tarehe 22 Februari, 2016.
Timu hiyo itaundwa na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Sehemu ya Leseni, Mazingira, Ukaguzi wa Migodi na Idara ya Sheria.
“Wataalam wengine watakaounda Kamati hii ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Watathmini kutoka Wizara ya Ardhi, Baraza la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira ( NEMC) na Wizara ya Maji na Umwagiliaji,” alisema Profesa Muhongo.
Aliongeza kuwa Wajumbe wengine ni Wenyeviti wa Vitongoji vitakavyozungukiwa na Kamati, Wawakilishi wa Mbunge wa Tarime Vijijini, Mgodi wa Acacia North Mara na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Alisema kuwa Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Tarime, Halmashauri ya Tarime na Vyombo vya Usalama wilayani humo havitashiriki katika Kamati husika kwani baadhi ya tuhuma za wananchi zimeelekezwa katika Ofisi hizo.
Kila upande unaohusika na zoezi hilo umetakiwa kuwasilisha majina ya wajumbe wa Kamati kwa Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje, siku ya Jumanne tarehe 16 Februari, 2016.
Alieleza kuwa Mwenyekiti na Makamu wa Kamati hiyo watatoka Wizara ya Nishati na Madini na kwamba kamati itafanya kazi katika siku zilizopangwa na si vinginevyo na mwenendo wa Kazi wa Kamati husika utakuwa ukifuatiliwa katika kila wiki.
Baada ya zoezi la upangaji wa Kamati hiyo kukamilika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, alimshukuru Waziri wa Nishati na Madini na serikali kwa ujumla kwa kulipa uzito jambo hilo ambalo halijatafutiwa ufumbuzi kwa miaka kadhaa na kuitakia kamati kila la heri katika utendaji kazi ili kila mtu apate haki yake anayostahili.
Naye Meneja Uendelezaji, Mgodi wa dhahabu wa Acacia North Mara, Abel Yiga kwa niaba ya Mgodi huo amemshukuru Profesa Sospeter Muhongo kwa kufika wilayani Tarime ili kutatua changamoto kati ya Mgodi na wananchi kwani wamekuwa wakiwasilisha changamoto zao katika ngazi mbalimbali za uamuzi lakini utatuzi bado haujapatikana.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tarime, Glorious Luoga pia ametoa pongezi kwa Profesa Muhongo kwa kutoa muongozo utakaopelekea kupata suluhisho la kero zinazowapata wananchi wanaozunguka mgodi pamoja na kero ambazo mgodi unazipata katika utekelezaji wa majukumu yake.
Alitoa wito kwa wananchi wilayani Tarime kuwa na imani na Kamati hiyo na kila upande ukubaliane na taarifa itakayotolewa na Kamati husika.
Baadhi ya kero zitakazofanyiwa kazi na kamati hiyo ni pamoja na suala la fidia kwa wananchi waliopisha Mgodi, utegeshaji wa nyumba ndani ya eneo la Mgodi, athari za mitetemo inayotokana na upasuaji wa miamba, ajira kwa watanzania ndani ya mgodi, utoaji wa huduma katika mgodi na masuala mengine yatakayojitokeza wakati zoezi la tathmini litakapoanza.
No comments:
Post a Comment