Wednesday, February 17, 2016

JAMII YAASWA KUTUMIA FURSA YA UFUGAJI WA NYUKI NA UPANDAJI WA MITI KIBIASHARA.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Gladyness Mkamba (katikati) akizungumza wakati akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Gen. Gaudence Milanzi katika ufunguzi wa Mkutano wa mapitio ya kukamilisha mradi wa Kitaifa wa Uendelezaji Misitu na Ufugaji Nyuki nchini (NFBKP II) unaofadhiliwa na Serikali ya Finland kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika Chuo cha Taifa cha Utalii Tawi la Bustani Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Februari, 2016. Kushoto ni Mshauri wa masuala ya Malisili kutoka Ubalozi wa Finland hapa nchini Bw. Mikko Leppanen.
Sehemu ya washiriki wa mkutano huo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na TAMISEMI. 
Sehemu ya washiriki wa mkutano huo katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Tawi la Bustani Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Gladyness Mkamba akizungumza na Waandishi wa Habari katika chuo cha Taifa cha Utalii Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Februari, 2016.
Mratibu Msaidizi wa mradi wa NFBKP II, Bi. Magdalena Muya (kulia) akiwasilisha mada ya jumla juu ya mradi huo ambao ulianza mwaka 2013 na kukamilika mwaka huu 2016.
Mshauri wa masuala ya Malisili kutoka Ubalozi wa Finland hapa nchini Bw. Mikko Leppanen akieleza jambo kwa waandishi wa habari.
Picha ya pamoja.
Na Hamza Temba, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Maliasili na Utalii

JAMII hapa nchini imeaswa kutumia fursa iliyopo ya ufugaji wa nyuki na upandaji wa miti kibiashara kujikwamua kwenye lindi la umasikini.

Hayo yamesemwa jana na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Gladyness Mkamba akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam.

Bi. Mkamba alisema kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya kuzalisha asali kwa wingi duniani ambayo ikitumiwa ipasavyo itasaidia kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

"Kwa sasa Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika ambapo inazalisha asali tani 34,000 kwa mwaka baada ya Ethiopia inayozalisha tani 56,000. Hata hivyo kiwango hicho ni kidogo kwa kuwa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha asali tani 1,038,000 kwa mwaka" Alieleza.

Akizungumzia changamaoto kuu inayosababisha kiwango hicho kisifikiwe kirahisi, amesema ni utashi hafifu wa jamii kujishuulisha na kazi za ufugaji nyuki na uhifadhi wa mazingira ikiwemo upandaji wa miti.

Bi. Mkamba aliongeza kuwa Jamii ikihamasishwa vya kutosha juu ya faida za ufugaji nyuki na upandaji wa miti inaweza kutoa matokeo ya haraka kwa kuwa asali ina faida kubwa ikiwemo za kiafya na za kiuchumi.

Kwa upande wake Bi. Magdalena Muya ambaye ni Mratibu Msaidizi wa mradi wa Kitaifa wa Misitu na Ufugaji wa Nyuki nchini (NFBKP II) ameeleza kuwa changamoto zingine zinazokwamisha mafanikio katika sekta ya ufugaji nyuki nchini ni ukosefu wa teknolojia za kisasa za ufugaji nyuki na uzalishaji wa asali pamoja na ukosefu wa mitaji ya kuanzisha miradi mikubwa ya ufugaji wa nyuki.

Nae mshauri wa masuala ya Malisili kutoka Ubalozi wa Finland hapa nchini Bw. Mikko Leppanen, ameeleza kuwa Misitu ya Tanzania inakabiliwa na changamoto ya uharibifu mkubwa unaosababishwa na shughuli za kibinadamu ambapo hupelekea ukame na kuathiri pia uzalishaji wa asali ambao hutegemea malighafi za misitu.

Mshauri huyo ameiasa jamii hapa nchini kutunza mazingira ya misitu, kupanda miti kibiashara na kuhifadhi mazingira ambayo yatasaidia kuweka mazingira bora ya kuishi ikiwa ni pamoja na kuwezesha ufugaji wa nyuki kibiashara na kuwainua watu kiuchumi.

Wakati huo huo Kaimu Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili Bi. Gladyness Mkamba akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Gen. Gaudence Milanzi wakati akifungua mkutano wa siku moja wa mapitio ya kukamilisha Mradi wa Kitaifa wa Misitu na Ufugaji wa Nyuki nchini (NFBKP II) ameishukuru Serikali ya Finland kwa kusaidia ufadhili wa mradi huo.

Ameeleza kuwa mradi huo ambao bajeti yake ni Euro Milioni 19.5 ambazo ni zaidi ya Tsh. Bilioni 47 kwasasa unafadhili mpango wa miaka minne wa Misitu binafsi katika Mikoa ya Iringa, Njombe na Morogoro kwa lengo la kuinua kipato cha wananchi wa vijijini katika Mikoa ya Kusini mwa Tanzania, Mikoa hiyo ni shemu ya Mikoa saba ya jumla inayofadhiliwa na mradi huo.

Amesema hayo yatafanyika kwa kuanzisha misitu ya uhakika yenye faida na kuongeza thamani ya mazao yake kwenye mtiririko wa uzalishaji kuanzia mbegu za miti hadi kwenye bidhaa bora za mbao.


Mradi huo ulianza Oktoba mwaka 2013 hadi Oktoba 2015 na kuongezewa muda wa ziada wa miezi minne ambapo unakamilika mwezi huu wa Februari 2016.

No comments: