HOTUBA YA MHE. KASSIM MAJALIWA MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA PILI WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TAREHE 5 FEBRUARI, 2016
I: UTANGULIZI
(a) Masuala ya Jumla
Mheshimiwa Naibu Spika,
1. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutujalia afya njema na uwezo katika kutenda yote yaliyo mema. Tumekuwepo hapa kwa takriban siku 11 katika shughuli za Mkutano wa Pili wa Bunge lako Tukufu. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo.
2. Tumekutana hapa tukiwa tumeshuhudia uundwaji wa Serikali unaoendelea ambapo Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya uteuzi wa Baraza jipya la Mawaziri ambao ni Waheshimiwa Wabunge wenzetu. Niruhusu nitumie nafasi hii ya awali kuwapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri wote ambao wameteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Awamu ya Tano.
(b) Chaguzi Mbalimbali
Mheshimiwa Naibu Spika,
3. Katika Mkutano huu, tumeweza kufanya Chaguzi za Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge. Vilevile, tumefanya chaguzi za Wenyeviti wa Bunge letu na Wajumbe wa kutuwakilisha katika Taasisi mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa. Kwa vile orodha ni ndefu, napenda nitumie nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kabisa na kwa ujumla wao wote waliogombea nafasi hizo na kushinda. Ni matarajio yangu kwamba tutatumia nafasi hizo vizuri katika kuleta ushirikiano, mshikamano na kufanya kazi pamoja kama Wawakilishi wa Wananchi na kutekeleza majukumu yetu kama Wabunge ndani ya Bunge hili.
(c) Maafa na Ajali
Mheshimiwa Naibu Spika,
4. Tarehe 27 Januari, 2016 wakati Bunge lako Tukufu likiendelea na Vikao, Waheshimiwa Wabunge walipewa taarifa ya kusikitisha ya kuzama kwa Kivuko cha Kilombero, ambapo katika tukio hilo watu walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa. Aidha, mali za abiria zimepotea. Wakati huo huo, mvua zinazoendelea kunyesha nchini katika baadhi ya maeneo zimesababisha mafuriko, vifo, uharibifu wa mali ikiwemo mazao na miundombinu. Katika baadhi ya maeneo, mvua hizi zimesababisha njaa na athari nyingine kwa jamii.
5. Pamoja na maafa ya mvua na mafuriko, wapo wananchi waliofariki na wengine kupata ulemavu katika ajali mbalimbali za vyombo vya usafiri. Nitumie fursa hii kuwapa pole wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika matukio yote hayo. Aidha, napenda kuwatakia afya njema wote waliopata majeraha. Kwa wale wote waliopoteza maisha tunawaombea Roho zao zilale mahali pema peponi - Amina.
6. Kuhusu uharibifu wa miundombinu, tunazo taarifa za uharibifu mkubwa wa Miundombinu katika maeneo kadhaa. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali itafanya kila liwezekanalo kurekebisha miundo mbinu ya barabara iliyoharibika. Tunatambua gharama kubwa inayohitajika, lakini ni wajibu wetu kama Serikali kuhakikisha Wananchi wanapata huduma muhimu hasa za mawasiliano kati ya eneo moja na jingine.
(d) Maswali
Mheshimiwa Naibu Spika,
7. Leo tunahitimisha Mkutano wetu wa Pili wa Bunge tukiwa tumefanya shughuli mbalimbali ndani ya Bunge letu. Katika Mkutano wetu, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kuuliza maswali ya kawaida na yale ya papo papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Jumla ya maswali115 ya msingi na 307 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali.
(e) Mjadala wa Hotuba ya Rais
Mheshimiwa Naibu Spika,
8. Katika Mkutano huu moja ya agenda iliyochukua nafasi kubwa ni Hoja ya Serikali ya kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Maufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hoja hiyo tuliihitimisha vizuri na kwa mafanikio makubwa. Kazi kubwa iliyoko mbele yetu ni kutekeleza yale tuliyokusudia kama wajibu wetu. Napenda kuwapongeza tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki katika mjadala wa Hotuba hiyo vizuri. Nichukue tena nafasi hii kuliahidi Bunge lako Tukufu kwamba michango ya Waheshimiwa Wabunge na maoni yao yatazingatiwa kwa utekelezaji.
II: MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO
Mheshimiwa Naibu Spika,
9. Katika Mkutano huu wa Bunge, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kujadili na kuidhinisha Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka wa Fedha 2016/2017. Vilevile, Bunge limejadili na kutoa maoni na ushauri katika mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika mwaka wa Fedha, 2016/2017. Kipekee, naomba nimshukuru Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango(Mb) na Naibu wake Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (Mb.) pamoja na Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara za Kisekta kwa ufafanuzi mzuri walioutoa wakati wa kuhitimisha hoja hii. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao mizuri, maoni na ushauri ambao Serikali itauzingatia katika kukamilisha maandalizi ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika,
10. Naomba nami uniruhusu nitoe maelezo mafupi ya msisitizo katika maeneo machache yaliyopata michango mingi kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja ya Serikali ya mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo. Waheshimiwa Wabunge wengi wamesisitiza kuhusu umuhimu wa Serikali kuongeza uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuimarisha udhibiti wa matumizi ya Serikali. Aidha, Waheshimiwa Wabunge wameishauri pia Serikali kuweka kipaumbele cha ujenzi wa Reli mpya ya Kati, kujenga uchumi wa Viwanda, kuanza na kusimamia ujenzi na Mitambo ya kuchakata gesi asilia (LNG) na Kiwanda cha Mbolea Mkoani Lindi, kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme Vijijini, ujenzi wa Bandari Mtwara, kutatua changamoto zinazowakabili Wakulima na Wafugaji pamoja na Wachimbaji Madini.
Vilevile, kuweka mikakati thabiti ya utekelezaji wa Miradi ya Sekta za Elimu, Afya, Maji na huduma kwa wenye Ulemavu na pia kuzingatia utawala bora. Serikali inatambua kuwa maeneo haya ni muhimu sana katika kujenga uchumi imara na endelevu na pia kuondoa umasikini. Hivyo, itazingatia sana ushauri huu mzuri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika,
11. Naomba nitumie fursa hii kumpongoeza Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa umahiri mkubwa na umakini aliouonesha ikiwa ni mwanzo mzuri wa kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano. Mheshimiwa Rais ameonesha kasi kubwa na dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania katika kujenga uchumi imara, unaokuwa na endelevu. Waheshimiwa Wabunge wengi watakubaliana nami kwamba Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi chake cha mwanzo cha siku 100, imeonesha dhahiri nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba makusanyo ya mapato yetu yanaongezeka. Jitihada hizo za kuongeza makusanyo ya mapato ya Serikali zimefafanuliwa vizuri kwenye Hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango. Serikali itaendelea na mikakati yake ya kuongeza Mapato yake na kudhibiti mianya ya kukwepa kodi. Ni matumaini yangu kuwa Waheshimiwa Wabunge, Wafanyabiashara na Wananchi wote wataunga mkono dhamira hiyo njema ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika,
12. Kuhusu matumizi, tayari Serikali imeanza kuchukua hatua thabiti za kudhibiti matumizi yasiyo na tija katika Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea na Taasisi zote za Umma pamoja Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Lengo la hatua zinazochukuliwa ni kuhakikisha kwamba Serikali inasimamia kwa umakini matumizi ya fedha za Umma ili zitumike ipasavyo kwa malengo yaliyokusudiwa. Hatua hizi zitaimarishwa zaidi katika mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika,
13. Kama nilivyoeleza awali hoja nyingi za msingi zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge kuhusu Mpango wa Taifa, zimefafanuliwa vizuri na Waheshimiwa Mawaziri wa Kisekta na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Naomba niwaahidi kuwa tutazizingatia katika mchakato wa maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017, kwa kadri itakavyowezekana. Waheshimiwa Wabunge watashirikishwa kikamilifu katika mchakato huo kupitia Kamati mbalimbali za Bunge. Serikali itafarijika sana kupata maoni na ushauri zaidi ili tuweze kuboresha mipango yetu ya muda mfupi na muda mrefu.
III: SEKTA YA KILIMO
Uzalishaji wa Mazao ya Chakula 2014/2015 na Upatikaji wa Chakula 2015/2016
Mheshimiwa Naibu Spika,
14. Hali ya chakula kwa mwaka 2015/2016 katika maeneo mengi ya nchi imeendelea kuwa ya kuridhisha kufuatia mavuno mazuri yaliyopatikana msimu wa kilimo wa 2014/2015. Takwimu za Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi zinaonesha kuwa albaki kutoka msimu uliopita nchi ilikuwa na ziada ya chakula licha ya kuwepo kwa maeneo machache ambayo hayakuwa na chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika,
14. Kutokana na uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2014/2015 kuwa Tani milioni 15.5 na mahitaji ya chakula kwa mwaka 2015/2016 kuwa Tani milioni 12.9 hivyo nchi imejitosheleza kwa chakula kwa ziada ya Tani milioni 2.5 sawa na asilimia 120. Napenda kuwahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendelea kuhudumia maeneo yote yenye uhaba wa chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika,
15. Pamoja na Taifa kuwa na ziada ya asilimia 120 ya chakula, tathmini ya hali ya chakula nchini inaonesha kuwa kuna Halmashauri 69 katika mikoa 18 nchini yenye maeneo yenye dalili za upungufu wa chakula. Maeneo hayo yapo katika Mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Lindi, Singida, Tabora, Arusha, Geita, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Tanga, Simiyu, Mwanza, Morogoro, Iringa, Njombe, Mtwara, na Pwani.
Mheshimiwa Naibu Spika,
16. Ili kukabiliana na hali ya uhaba wa chakula katika maeneo hayo, Serikali inaendelea kutoa chakula katika maeneo hayo ambapo jumla ya Tani 23,871.6 za chakula zilitengwa kwa ajili hiyo. Hadi kufikia tarehe 17 Januari, 2016, jumla ya Tani 11,860.8 zilikuwa zimechukuliwa toka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwenda kwenye Halmashauri za Wilaya zenye upungufu wa chakula kwa ajili ya usambazaji. Natoa wito kwa Halmashauri ambazo hazijachukua mgao wao kufanya hivyo mara moja ili Wananchi katika maeneo hayo wasizidi kuathirika.
Mheshimiwa Naibu Spika,
17. Sambamba na utoaji wa chakula cha msaada, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaendelea kutoa mahindi katika maghala ya Songea na Sumbawanga kwa ajili ya kuuzwa kwa wafanyabishara wa nafaka walioidhinishwa na mikoa yenye uhaba wa Chakula. Lengo ni kuongeza upatikanaji wa chakula na kukabiliana na kasi ya kupanda kwa bei ya vyakula katika maeneo hayo. Chini ya utaratibu huo, vibali vimeshatolewa kwa wafanyabiashara wa Mikoa 17, vya kununua jumla ya Tani 77,166. Hadi kufikia tarehe 18 Januari, 2016 jumla ya Tani 56,817.5 kati ya Tani 64,817.3 zilizokuwa zimelipiwa kutoka NFRA tayari zilikuwa zimechukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika,
18. Ili kuongeza na kuimarisha uhakika na usalama wa chakula hapa nchini, Serikali imelenga kujenga maghala 275kwa awamu katika sehemu zenye uzalishaji mkubwa wa zao la mahindi ambapo hadi sasa jumla ya maghala 125yanaendelea kujengwa na kukarabatiwa katika maeneo hayo. Aidha, Serikali kwa kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaendelea kujenga maghala ya kimkakati kwa ajili ya kuhifadhi akiba ya Taifa. Kwa sasa ghala moja lenye uwezo wa kuhifadhi Tani 5,000 limeshajengwa Wilayani Mbozi Mkoani Mbeya. Aidha, Serikali imepata mkopo wenye masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland ambao utawezesha kujenga vihenge vya kisasa (silos) vyenye uwezo wa kuhifadhi Tani 160,000 na maghala yenye uwezo wa kuhifadhi Tani 90,000.
Mheshimiwa Naibu Spika,
19. Pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali, ninawataka viongozi wa Mikoa, Wilaya na atendaji katika Halmashauri zote Nchini kuwahamasisha Wananchi kutumia vizuri mvua zinazonyesha nchini kote kulima kwa bidii ili kuweza kuvuna na kujiwekea akiba ya chakula cha kutosha kwa ajili ya kaya zao wakati wote wa mwaka. Aidha, wawahamasishe wafanyabiashara na wadau wengine kusaidia Serikali kuchukua chakula kutoka maeneo yenye ziada na kupeleka katika maeneo yenye upungufu. Ni imani yangu kwamba tukizingatia maelekezo haya pamoja na juhudi za Serikali zilizooneshwa, tatizo la uhaba wa chakula nchini litapungua, kama siyo kumalizika kabisa.
IV: MIFUGO:
Hatua zilizochukulwa na Serikali katika Kushughulikia Migogoro ya Wakulima na Wafugaji;
Mheshimiwa Naibu Spika,
20. Migogoro ya ardhi hapa nchini ina sura nne; migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji, mgogoro kati ya Wananchi na Wawekezaji; migogoro kati ya Wananchi na Serikali na migogoro kati ya Mamlaka moja na Mamlaka nyingine ndani ya Serikali. Migogoro hii imeenea nchi nzima kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo kuongezeka kwa matumizi ya rasilimali ya ardhi.
21. Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi kwa kutumia Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 na Sheria ya matumizi ya Ardhi Na. 6 ya mwaka 2007, hadi kufikia mwezi Juni 2015 jumla ya Vijiji 620 katika Wilaya 81 kwenye Mikoa 22 zimeweza kutenga Hekta Milioni 1.9 kwa ajili ya Wafugaji. Wito wangu kwa Wananchi na Wadau wa Kilimo na Ufugaji nawaomba kutunza na kuendeleza maeneo haya ili yaweze kutumika kwa mujibu wa malengo yaliyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika,
22. Nitumie fursa hii pia kulijulisha Bunge lako Tukufu kuhusu hatua ambazo Serikali imechukua kukabiliana na migogoro ya Wakulima na Wafugaji iliyotokea katika Mikoa ya Morogoro (Wilaya za Mvomero na Kilombero) na Manyara (Wilaya ya Kiteto). Katika kushughulikia tatizo hili, Jumla ya Vijiji 53 vimeainisha maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo Kilimo na Ufugaji. Aidha, jumla ya Mashamba Pori Manane (8) yameanishwa na orodha yake imewasilishwa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua za kufutiwa hati miliki na hatimaye kufanya utaratibu wa kuyatumia kwa ufugaji. Ni matarajio yangu kuwa maeneo haya yatapunguza sana kwa kiasi kikubwa matatizo ya uhaba wa malisho hapa Nchini. Wito wangu niwatake Viongozi wa Vijiji kusimamia vizuri matumizi ya maeneo yatakayotolewa kwa ajili ya malisho ili tatizo hili la kukosa maeneo ya malisho lisijirudie tena.
Mheshimiwa Naibu Spika,
23. Bado kuna mgogoro wa Wafugaji na Wakulima katika Bonde Oevu la Kilombero ambao umetafutiwa ufumbuzi kwa kuweka alama (branding) mifugo yote katika eneo hili ambapo jumla ya Mifugo 52,780 ilipata usajili wa Wilaya. Aidha, jumla ya Mifugo 24,586 imeondolewa katika eneo la Bonde la Kilombero. Kwa kuzingatia hatua zilizochukuliwa na Serikali Wananchi wanapaswa kufuata Sheria na kuhakikisha Mifugo hairudi tena katika maeneo yaliyokatazwa na kwamba maeneo haya yanahifadhiwa kwa mujibu wa Sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika,
24. Mgogoro wa Wafugaji na Wakulima katika maeneo ya Kiteto ni wa muda mrefu na kwa bahati mbaya sana umeleta madhara makubwa kwa maisha ya Wanadamu na uharibifu wa mali. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Tume iliyoundwa na aliyekuwa Waziri Mkuu (Mstaafu) Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda ikiongozwa na Askofu Amos Mhagachi imekamilisha hatua muhimu ya kuleta maelewanao na maridhiano katika pande zilizoathirika na mgogoro huo. Kwa sasa hali imeendelea kuimarika na tunaendelea kufuatilia kuhakikisha inakuwa shwari kwa muda wote.
25. Vilevile tarehe 29 Januari 2016 nimekutana na Viongozi wa Serikali, Halmashauri ya Wilaya na Chama kutoka Wilaya ya Kiteto hapa Dodoma ambapo nilipata fursa ya kupokea taarifa ya Tume niliyoitaja hivi punde. Nimeiagiza Tume kuendelea na hatua iliyobakia ili kurejesha utulivu na amani kwa wananchi wa Kiteto. Hata hivyo, nimepanga kufanya ziara Wilayani Kiteto katika siku chanche zijazo ili niweze kukutana na Wananchi walioathirika na mgogoro huu na ikiwa ni pamoja na kujionea hali halisi Wilayani Kiteto ili tuweze kutatua migogoro yote. Wito wangu kwa ndugu zangu wa Kiteto ni kuwaomba waendelee kuvumilia wakati jitihada za Serikali katika kutatua migogoro hiyo inaendelea.
V: UTEKELEZAJI WA ELIMU MSINGI BILA MALIPO
Mheshimiwa Naibu Spika,
26. Tangu Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli atoe maaelezo ya utekelezaji wa elimu ya msingi bila malipo, kumekuwa na umuhimu wa kutoa elimu na ufafanuzi zaidi juu ya utekelezaji wa agizo la elemu bila malipo kwa Watanzania kuanzia darasa la awali hadi Kidato cha Nne katika Shule za Umma. Hii ni hatua ya Serikali katika kuhakikisha uwepo wa fursa ya elimu bora kwa wote kwa kuwapunguzia mzigo wazazi na walezi kugharamia au kuchangia upatikanaji wa elimumsingi.
Katika mpango huu, Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa mwanafunzi atasoma kuanzia darasa la awali hadi kidato cha Nne bila ya wazazi na walezi kulipa ada ya shule, gharama za mitihani na michango mbalimbali. Hata hivyo, yapo majukumu ambayo yataendelea kutekelezwa na wazazi na walezi wote ambayo ni pamoja na kununua sare za shule na michezo, madaftari, kalamu na chakula kwa wanafunzi wa shule za kutwa zilizojiwekea utaratibu huo. Maeneo mengine ni kulipia nauli ya kwenda na kurudi shule, na mahitaji mengine kama kununua godoro, shuka na vifaa vya usafi binafsi. Mzazi au mlezi anao wajibu wa kugharamia matibabu ya mtoto wake.
Mheshimiwa Naibu Spika,
27. Napenda nitumie nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote tushirikiane katika juhudi za kuunga mkono uamuzi wa Serikali kuhusu elimu bila malipo. Aidha, nawaomba wote kwa ujumla wetu kushirikiana kuwaelimisha Wananchi wetu kuhusu utaratibu huu na wajibu wa kila mmoja wetu kama Mzazi/Mlezi, Serikali na jamii kuhusu utekelezaji wa zoezi hili. Nia yetu ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata fursa ya kupata elimu bora kwa mtoto mwenye umri wa kwenda Shule na wote walioko katika Shule za Msingi na Sekondari. Napenda pia kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kama tulivyokwisha sema suala la ada elekezi inafanyiwa kazi na ikikamilika Wananchi watajulishwa kuhusu utaratibu huo. Vikao vya pamoja baina ya Serikali na wadau vitaanza hivi karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika;
28. Katika kutekeleza mpango huu, Serikali imetenga fedha shilingi Bilioni 131.4 kuanzia mwezi Disemba 2015 hadi Juni, 2016, kuhudumia wanafunzi wa bweni kwa chakula, kufidia gharama za ada za mitihani, ada ya shule na kutoa fedha za uendeshaji wa shule (Capitation Grants). Aidha, kupitia Waraka wa Elimu Na. 5 wa mwaka 2015, Serikaliimefuta michango yote iliyokuwa inachangishwa shuleni kwa idhini ya Kamati na Bodi za Shule.
Mheshimiwa Naibu Spika,
29. Tunatambua katika utekelezaji wa zoezi hili zipo changamoto zilizojitokeza. Kwa mfano, baadhi ya shule zenye wanafunzi wachache kupata fedha kidogo sana kwa kuwa ugawaji wa fedha unazingatia idadi ya wanafunzi. Lakini pia zipo changamoto katika kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa kutwa na uendeshaji wa Hosteli ambazo wazazi na walezi au jamii walikuwa wanachangia fedha za chakula. Serikali inaendelea kuzifanyia kazi changamoto hizo zilizojitokeza katika utekelezaji wa mpango huu ikiwemo uelewa wa jamii na wadau kuhusu mpango mzima kwa ujumla wake.
VI: HUDUMA YA MIKOPO KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Mheshimiwa Naibu Spika,
30. Serikali imeendelea kutoa huduma ya mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2015/2016 kwa kuzingatia Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Namba 9 ya mwaka 2004 (Kama ilivyorekebishwa), Kanuni za Utoaji Mikopo za mwaka 2008, na Mwongozo wa utoaji Mikopo na Ruzuku kwa mwaka wa masomo 2015/2016. Hadi kufikia mwishoni mwa Januari 2016, Serikali ilikuwa imetoa mikopo yenye thamani ya ShilingiBilioni 207.9 kwa wanafunzi 122,786 wa elimu ya juu, wakiwemo wanafunzi wa mwaka wa kwanza 53,850 ambao ni asilimia 98.9 ya wanafunzi 55,254 walioomba mikopo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika,
31. Ili Taifa liendelee kuwa na wataalamu wa kutosha katika nyanja muhimu, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele cha kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wanaodahiliwa katika programu za kipaumbele ikiwemo Sayansi za Tiba, Ualimu wa Sayansi na Hesabu, Uhandisi wa Mafuta na Gesi, Uhandisi Umwagiliaji, Sayansi za Kilimo, Wanyama na Ardhi. Aidha, Serikali inaendelea kufanyia kazi mikakati ya kuimarisha urejeshaji wa mikopo pamoja na kuwa na vyanzo endelevu vya kupata fedha za kumudu ongezeko la wanafunzi wenye mahitaji ya mikopo.
VII: HALI YA USALAMA NCHINI
Mheshimiwa Naibu Spika,
32. Hali ya usalama katika Nchi yetu kwa ujumla ni shwari. Hata hivyo, katika kipindi hiki nchi yetu imekuwa ikikabiliana na changamoto ya ongezeko kubwa la Wakimbizi hususan katika Mkoa wa Kigoma. Kambi zetu zilizoko mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora na Tanga zinahifadhi wakimbizi wapatao 218,895 kutoka mataifa ya Burundi (wakimbizi 156,377), Congo-DRC (wakimbizi 62,176), Somalia (wakimbizi 150) na Mataifa Mchanganyiko (wakimbizi192) kutoka nchi za Rwanda, Uganda, Sudan ya Kusini na Ethiopia. Kwa ujumla, katika kipindi hiki wamepokelewa wakimbizi zaidi ya 122,267 kutoka Burundi. Aidha, hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2015 kambi mpya ya wakimbizi ya Nduta imepokea wakimbizi 38,994 wengi kati yao wamehamishiwa kutoka Kambi ya Nyarugusu na wachache wakiwa wameingia moja kwa moja kutokea Burundi.
Mheshimiwa Naibu Spika,
33. Kufuatia ujio wa wimbi kubwa la wakimbizi toka Burundi kumejitokeza matukio ya uhalifu wa kutumia silaha za moto ndani na nje ya kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu. Aidha, kutokana na upekuzi na ukaguzi kwa wakimbizi unaofanywa kwa pamoja na vyombo vya dola sanjari na taarifa za ki-intelijensia imebainika kuwepo kwa askari waasi waliokimbia pamoja na raia wa kawaida ambao wanajaribu kuwashawishi vijana kujisajili ili kujiunga na vikundi vya waasi. Nitoe wito kwa wananchi na wakimbizi kushirikiana na vyombo vyetu vya usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu, hususan umiliki haramu wa silaha za moto kwenye makambi na katika maeneo mbalimbali.
VIII: MPANGO ENDELEVU WA USAFI WA MAZINGIRA NCHNI
Mheshimiwa Naibu Spika,
34. Mtakumbuka kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, aliamua maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru ya terehe 9 Desemba, 2015 yafanyike kwa kufanya usafi wa mazingira katika maeneo ya Umma na maeneo yanayowazunguka. Kwa ujumla Wananchi, Taasisi za Umma na Binafsi ziliitikia agizo hilo na kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo. Nichukue fursa hii kuwapongeza kwa dhati wananchi, taasisi za umma na binafsi wote kwa kushiriki katika zoezi hilo kikamilifu. Mlionesha moyo wa uzalendo na ari kwa nchi yenu. Nawapongeza sana!
Mheshimiwa Naibu Spika,
35. Usafi ni dhana muhimu katika kulinda afya za binadamu na kudhibiti magonjwa mbalimbali ya mlipuko ikiwemo kipindupindu. Ili kufanikisha lengo hili, kunahitajika juhudi za makusudi na za pamoja katika usimamizi wa sheria, kanuni na taratibu tulizojiwekea. Hivyo, Serikali imeamua kulifanya zoezi la usafi wa mazingira kuwa endelevu. Kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Serikali imetoa Waraka unaoelekeza kuwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi iwe Siku Maalum ya kufanya Usafi wa Mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika,
36. Napenda kuendelea kusisitiza katika kila ngazi yaani Viongozi na Wananchi kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha zoezi hili linakuwa endelevu. Aidha, napenda kuwahimiza Viongozi wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri kusimamia usafi wa mazingira katika maeneo yao ya utawala zoezi ambalo litakuwa linafanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi. Kila Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya nchini awe na mikakati ya kudumu ya usafi ikiwa ni pamoja kuhakikisha kuwa kuna sheria ndogo za usafi wa mazingira na zinatekelezwa ipasavyo. Aidha, Halmashauri zote nchini zihakikishe kuwa uchafu uliokusanywa katika maeneo mbalimbali unazolewa na kupelekwa katika maeneo mahususi ya dampo. Simamieni kikamilifu wakandarasi waliopewa zabuni hizo na kuona wanatimiza wajibu wao kikamilifu.
Mheshimiwa Naibu Spika,
37. Kama tulivyoona Usafi wa mazingira ni jukumu la kila Mwananchi na linapaswa kuwa endelevu. Rai yangu kwa Watanzania wote ni kujenga tabia ya kuhakikisha kuwa mahali pa kazi na mazingira yanayowazunguka yanakuwa safi wakati wote. Kufanya hivyo, kutasaidia kuimarisha usafi wa mazingira na kuboresha afya. Hali kadhalika kupunguza mlipuko wa magonjwa yakiwemo kipindupindu.
38. Wito wangu kwa Wananchi ni kuona kuwa zoezi la usafi ni la kila mmoja wetu na kuepuka kuchafua mazingira kwa makusudi ikiwemo kuepuka tabia za kutupa taka hovyo wanapokuwa katika vyombo vya usafiri na pia kutofanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa ili kuzuia kutupwa taka hovyo. Wamiliki wa mabasi yanayofanya safari ndefu wanatakiwa waweke vifaa vya takataka. Yeyote atakayebainika kutupa takataka dirishani, atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na mmiliki wa basi hilo.
Watendaji wa Mitaa na Kata na Vijiji kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha maeneo wanayoyasimamia yanakuwa katika hali ya usafi. Nitumie fursa hii kuwahimiza Wananchi, Taasisi na Jumuiya zote kuhakikisha wanaweka mazingira katika hali ya usafi na pia kushiriki katika siku ya usafi kama iliyopangwa na Serikali.
IX: UHUSIANO WA KIMATAIFA
Mheshimiwa Naibu Spika,
39. Nchi yetu imeendelea kuwa kivutio kikubwa katika mahusiano baina ya Nchi na Nchi, Jumuiya za Kikanda na Kimataifa. Hii inatokana na Viongozi wetu ambao wamekuwa katika mstari wa mbele kudumisha mahusiano yetu katika Medani za Kimataifa. Yapo mambo mengi yaliyofanyika na yanayo endelea kufanyika kama mwendelezo wa kudumisha ushirikiano katika Jumuia hizi za Kikanda na Kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika,
40. Kutokana na juhudi za Viongozi wetu kutangaza Nchi yetu Kimataifa, ni hivi karibuni tu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Ban Ki-moon kuwa mmoja wa Wenyeviti wa jopo la ushauri la ngazi ya juu kuhusu Afya ya Mama na Mtoto Duniani (Every Woman, Every Child). Hii ni heshima kubwa kwa nchi yetu kwa kuwa itaiweka Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yenye kuheshimika duniani. Aidha, uteuzi huu ni chachu ambayo inaleta matumaini mapya katika kukabiliana na changamoto za afya ya mama na mtoto, hususan katika nchi zinazoendelea kama Tanzania. Nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa uteuzi huo. Tunamuombea heri na baraka tele katika kutekeleza jukumu hilo kubwa la Kimataifa kwa maendeleo ya watu wetu.
X: KUIMARISHA UTENDAJI SERIKALINI NA MAADILI
Mheshimiwa Naibu Spika,
41. Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi imedhamiria kurejesha nidhamu na maadili ya Watendaji wa Serikali na Watumishi wa Umma katika kutoa huduma mbalimbali kwa Wananchi kwenye maeneo mbalimbali. Katika kuhakikisha Watumishi wa Umma na Watanzania wote wanafanya kazi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuja na kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”. Tafsiri ya falsafa hii ni kuwataka Watanzania wote katika nafasi mbalimbali walizopo kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na vitendo vya uzembe, urasimu na kutenda kazi kwa mazoea.
42. Aidha, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 chini ya Ibara ya 22 inaainisha kuwa, kilaMtu anayo haki ya kufanya kazi. Vilevile, Ibara ya 25 inafafanua kuwa kufanya kazi ndiyo njia pekee ya kumwezesha Mtanzania kupata utajiri na ndilo chimbuko la ustawi wa wananchi na ni kipimo cha utu.
Wakati akihutubia Mkutano wa kwanza wa Bunge lako Tukufu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa maneno yake alisema, napenda kunukuu:-
“Serikali nitakayounda, nataka iwe inawahudumia Wananchi kwa haraka na sio kuwasumbua sumbua na kuwazungusha. Natoa rai kwa Watumishi wa Serikali, hasa ambao ni wazembe na wavivu, kujiandaa. Wamevumiliwa kwa muda mrefu sasa basi. Kwa sababu Watumishi wa aina hiyo hawatavumiliwa katika Serikali nitakayoiongoza. Lugha za “Hiyo ni changamoto tutaishughulikia” au “Mchakato unaendelea”hazitavumiliwa katika Serikali ya Awamu ya Tano. Mimi nataka watu wa Kazi tu. Hatuwezi kulea watu ambao wanalipwa mishahara lakini hawafanyi kazi wanazotakiwa kufanya, au wamegeuza Ofisi za Umma kuwa ni mahala pa kuchuma bila kufanya kazi.”mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Naibu Spika,
43. Ili kutekeleza maneno ya Mheshimiwa Rais na kuhimiza matakwa ya Kikatiba, kila Mtanzania anapaswa kushiriki na kujituma kwa uaminifu katika kazi halali za uzalishaji mali. Aidha, kila Mwananchi anapaswa kuwa na nidhamu ya kazi na kuhakikisha anafikia malengo yaliyowekwa. Nitumie fursa hii pia kuwakumbusha Watumishi wa Umma kuwa wamepewa dhamana ya kuwahudumia Wananchi kwa niaba ya Serikali. Hivyo wanawajibika kuhakikisha wanawahudumia Wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na kwa taaluma zao. Ni lazima wahakikishe kuwa wanatatua kero za Wananchi. Sio sahihi wananchi kuwasilisha kero zao kwa viongozi wa ngazi za kitaifa hasa wakati wa ziara ilhali viongozi wa mikoa na wilaya wapo katika maeneo hayo kwa wakati wote.
44. Tunatambua kuwa wapo Watumishi wanaotekeleza vyema majukumu yao. Lakini pia wapo Watumishi ambao hawazingatii maadili ya kazi zao na pia wanafanya kazi kwa uzembe. Serikali haitaacha kuchukua hatua za nidhamu kwa watumishi wote wasiozingatia kikamilifu sheria, kanuni na taratibu katika Utumishi wa Umma. Aidha, kwa kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Viongozi na Watumishi wote wa Umma lazima tufanye kazi kwa kuzingatia weledi na kujiamini. Kila mtu anapaswa kujitathmini kama dhamana aliyopewa anaitendea haki.
Mheshimiwa Naibu Spika,
45. Huu sasa ni wakati wa kufanya mabadiliko ya dhati katika utendaji na uadilifu. Kwa maana hiyo napenda kusisitiza mambo yafuatayo kwamba:-
(i) Kila Kiongozi na Mamlaka ya nidhamu ni lazima kuwajibika kusimamia Utendaji na Maadili ya Kazi. Hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa wakati na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi. TUSIONE HAYA HATA MARA MOJA, CHUKUENI HATUA.
(ii) Wananchi wahudumiwe ipasavyo na kwa weledi, haki, uadilifu na heshima. Mambo haya yakizingatiwa hakuna mwananchi atakayesafiri kutoka kijijini, wilayani au mkoani kutafuta huduma Makao Makuu ya Wizara, Ofisi ya Waziri Mkuu au IKULU.
(iii) Madawati ya malalamiko yawepo katika Ofisi za Umma. Aidha, tayari maelekezo yametolewa ya Watumishi wa Umma wazingatie utaratibu wa kuvaa vitambulisho vyenye majina yao kwa urahisi wa wananchi kuwatambua wanapowahudumia. AGIZO HILI LITEKELEZWE.
Mheshimiwa Naibu Spika,
46. Ni kweli kwamba, Mheshimiwa Rais ametumia dhana ya “kutumbua jipu” kama dawa ya kusimamia uwajibikaji hasa katika wale wenye dalili ya kukosa maadili ya Utumishi wa Umma. Tafsiri ya dhana hii ya “Kutumbua jipu”inalenga katika kuwarejesha Watumishi wa Umma na walioko Serikalini katika mstari mzuri wa utendaji. Nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote kama tulivyo na kwa umoja wetu, tumuunge mkono Mheshimiwa Rais katika vita hii kubwa ya “Kutumbua Majipu”. Tukiwa pamoja na kwa kushirikiana tutaweza kuibadilisha nchi yetu kuwa nchi ya maadili na yenye sifa ya juu katika utendaji wa Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika,
47. Aidha, naomba nisisitize kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli inaongozwa na Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu za Nchi. Vilevile inaheshimu na kuthamini haki za Watumishi wa Umma wa ngazi zote na inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Watumishi wa Umma katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa. Kamwe, Serikali haitamwonea mtumishi yeyote wala kumnyanyasa endapo tu atakuwa anatenda yale yanayopasa. Lakini pia haitamvumilia mtumishi mzembe na asiyetimiza wajibu wake. Serikali itaendelea kuchukua hatua za kurejesha nidhamu kwa Watumishi wa Umma ili kuwezesha Nchi yetu kuwa na Utumishi wenye kuzingatia uadilifu na uliotukuka.
XI: HITIMISHO.
Mheshimiwa Naibu Spika,
48. Uzoefu nilioupata katika muda mfupi tuliokaa pamoja hapa Bungeni, nimegundua kuwa tuna Waheshimiwa Wabunge mahiri waliobobea katika nyanja mbalimbali. Wapo wasomi wa ngazi zote, wazee kwa vijana ambao wana uzoefu na utaalam mkubwa. Ni imani yangu kuwa tutatumia utaalam na uwezo mkubwa tulionao katika kuijenga nchi yetu na kuwasaidia Watanzania kutoka hapa tulipo hadi hatua ya mbele katika kuleta maendeleo. Wananchi waliotuchagua wanatutegemea. Nawaomba tutangulize uzalendo katika kila jambo tufanyalo kwa manufaa ya Taifa letu na watu wake. Tufike mahali ambapo kwa elimu, busara na hekima tulizonazo kuacha kabisa ushabiki wa kisiasa badala yake tutizame mbele katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika,
49. Napenda kuhitimisha Hotuba yangu kwa kurejea tena nilivyosema hapo awali kwamba, baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu kwa mafanikio makubwa, kazi kubwa iliyo mbele yetu ni kuijenga nchi yetu kwa umoja na mshikamano. Nawaomba tuweke maslahi ya Watanzania na Taifa letu mbele. Tudumishe amani na utulivu. Tupuuze sera zozote za kudhoofisha utaifa wetu kama Watanzania na kutugawa kwa misingi yoyote ile, iwe ya kikabila, imani za dini, rangi au kwa itikadi za kisiasa. Dhamira yetu sote iwe ni kukuza uchumi wa nchi yetu na kuondoa umaskini ili kuwaletea wananchi wetu maendeleo na maisha mazuri.
50. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa Tanzania inapiga hatua mbele. Tufanye kazi kwa bidii kuunga mkono kaulimbiu yetu ya “Hapa ni Kazi Tu”. Aidha tutumie juhudi, maarifa na ubunifu zaidi katika kila jambo. Mimi naamini kuwa kwa ushirikiano katika Bunge hili na wananchi kwa ujumla, tutaweza kutimiza matarajio ya wananchi waliotuchagua na matarajio ya Watanzania wote.
Mheshimiwa Naibu Spika,
51. Naomba nitumie nafasi hii tena kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha mkutano huu. Nikushukuru wewe Naibu Spika, na Mheshimiwa Spika kwa kutuongoza vizuri na kwa weledi mkubwa. Kipekee niwashukuru Wenyeviti wa Bunge ambao wamekalia kiti kwa mara ya kwanza lakini kwa weledi mkubwa, Hongereni sana!!.
Mheshimiwa Naibu Spika,
52. Nitumie nafasi hii kumshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri ya kuhakikisha mkutano huu unakamilisha shughuli zake kama ilivyopangwa. Niwashukuru Wataalam wote wakiwemo Waandishi wa Habari kwa kazi nzuri waliyofanya kufanikisha Mkutano huu.
Mheshimiwa Naibu Spika,
53. Nimalizie kwa kuwatakia wote safari njema mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi na katika majimbo yenu.Ninaamini kwamba, Mwenyezi Mungu atatulinda na kutuweka salama sote kama tulivyo hadi kukutana tena katika Mkutano ujao.
Mheshimiwa Naibu Spika,
54. Baada ya kusema hayo, naomba sasa kutoa Hoja kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 19 Aprili, 2016 saa 3:00 asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa Tatu kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika,
55. Naomba kutoa Hoja.
No comments:
Post a Comment