Herieth
Paul mwanamitindo wa Kitanzania anayeishi jijini New York, Marekani ambako
anafanyia kazi zake ameingia mkataba na kampuni ya vipodozi ya kimataifa ya MAYBELLINE ya New York, Marekani na
kutangazwa kuwa BALOZI wake wa kimataifa
kuanzia mwezi Februari 2016; shughuli ambazo zitamfanya kwenda maeneo
mbalimbali yakiwemo Bara la Ulaya, Marekani, Afrika, Asia na kwingineko
duniani. Kampuni ya Maybelline ilimtangaza rasmi hivi karibuni, Mwanamitindo wa
Kimataifa Herieth Paul, akiwa ni Mtanzania wa kwanza Mwanamitindo kuunyakua
ushindi huu mkubwa.
Herieth mwenye umri wa miaka 20 aligundulika
kuwa na kipaji hicho akiwa na umri wa miaka kumi na nne (14) akiwa nchini
Canada alipokuwa akisoma na kuishi na wazazi wake.
Mbali
na uteuzi wa kuwa BALOZI wa kampuni ya Vipodozi ya Maybelline, Herieth Paul
amefanikiwa kufanya kazi na makampuni mbalimbali ya mitindo na vipodozi duniani
ikiwepo kampuni ya Diane Von Furstenberg, Lacoste, Tom Ford, Zac Posen, Phillip
Lim, Mac, Sephora nk...,
Mwanamitindo
wa Kimataifa Herieth Paul ambaye ameipeperusha Bendera ya Tanzania Dunia nzima
anafanya masomo yake ya Chuo kwa njia ya mtandao na pia akijihusisha na
shughuli za kijamii nyumbani alikozaliwa nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na
kuwasaidia watoto yatima na wale wenye mazingira magumu ili waweze kutimiza malengo yao ya kimaisha
ikiwa ni pamoja na elimu na mahitaji yao ya kila siku.
Mafanikio
ya Herieth ni mfano wa kuigwa na vijana wa Kitanzania kwa kuwa na uamuzi
sahihi, malengo dhabiti na bidii ya kazi, ni vichocheo muhimu vinavyoweza
kufanya mtu afanikiwe katika maisha.
Gazeti
la GLAMOUR la New York, Marekani
lilifanya mahojiano na Bi Herieth Paul wakati wa sherehe fupi ya kuteuliwa
kwake iliyofanyika jijiji New York Marekani:
Lipstick:
Hongera kwa kuteuliwa kuwa Balozi wa
Maybelline na kuwa mmoja kati ya wasichana waliokwisha kufanya kazi na kampuni
hii. Je, kati ya wasichana waliowahi kufanya kazi na Maybelline ni nani anayekuhamasisha
sana?.
Herieth: Sijui niseme ni nani kati ya Christy
Turlington na Jourdan Dunn. Christy ni mwanamke mwenye bidii ya kazi, ni mzazi
na anasaidia mashirika yanayohudumia wasiojiweza. Jourdan pia ni mzazi na
anatoa misaada kwa watu wengine.
Lipstick: Ni mwanamke gani anayekuvutia sana kwa
urembo?
Herieth: Mama yangu, ana uzuri wa asili, ngozi ya
mwili ambayo ni nyeupe kidogo kuliko yangu ambayo inameremeta. Lakini pia anampenda
Beyoncé.
Lipstick:
Katika kazi yako hii mpya kutakuwa na
kila aina ya vipodozi. Kipodozi kipi unachokipenda zaidi?
Herieth: Ninapenda kipodozi cha mdomoni chekundu
na mara nyingi hujipaka kipodozi hiki ninapokuwa na marafiki zangu. Pia hupaka mascara kwenye kope na hasa hasa Maybelline “Falsies Puch Up Drama Mascara”. Hii naibeba kila mahali niendapo.
Lipstick: Vipi, unapendelea mtindo gani wa nywele
wakati wote?
Herieth: Huwa nachana mitindo mbalimbali hasa
napenda kuwa na nywele fupi. Natumia mafuta ya “Olive” yanayoitwa “Ecostlyer
Gel”. Napaka nywele baada ya kuziosha asubuhi na kisha kuzifuta.
Lipstick: Hebu eleza ni wakati gani ulijiona
umependeza na kwanini?
Herieth: Hiki kinaonekana kama kitu cha mzaha
lakini huu ndio muda wangu muafaka kueleza urembo wangu. Siku hiyo nilijipodoa
mwenyewe. Niliweka nyusi za bandia, nikapaka rangi ya kahawia na rangi ya nude mdomoni. Nilipendeza na kuonekana
mrembo sana. Kabla ya hapo niliangalia kwenye “Video ya Jaclyn Hill You Tube”
namna ya kuremba “kope”. Akina mama wengi niliokutana nao walipendezwa na
kuvutiwa na nilivyoremba “kope”
zangu. Aidha waliniuliza nani aliyeniremba, niliwaambia nilijiremba mwenyewe.
Lipstick: Vipi unaonaje kuhusu uchaguzi wa wasichana
wa warembo kutangaza vipodozi na vifaa mbalimbali.
Herieth: Mwaka 2011 nilipoanza kazi hii ya
uanamitindo walikuwepo wasichana wachache sana weusi. Sasa hivi nawaona wengi
kutoka sehemu mbalimbali za dunia kama vile bara la Asia, India n.k. Naona hali
inaendelea kuwa nzuri, kuna mabadiliko na ninatumaini wasichana wengi wa aina
hii wataingia katika kazi hii ya mitindo.
Lipstick: Wakati wa sherehe ya mitindo ya mwezi,
unatunzaje ngozi yako ya mwili wakati unatumia vipodozi vya aina nyingi bila
kuiathiri ngozi yako?
Herieth: Huwa nakwenda kwa mtaalamu wa utunzaji wa
ngozi Mamie kila wiki. Yeye ndiye
anahudumia wasichana wengi wenye ngozi nyeusi. Nahitaji mtu mwenye utaalamu wa
ngozi yangu. Aidha huwa naangalia video kwenye mitandao ambayo inaniwezesha
kutengeneza aina ya kipodozi ambacho ni rafiki kwa ngozi yangu. Pia nanunua
aina mbalimbali ya vyakula ambavyo nachanganya na “distilled water” na “lavender
oil” ambavyo natumia kila siku kurutubisha mwili wangu. Uzuri wa “hyaluronic acid” ni kuwa inaifanya ngozi
yako ya mwili kuwa na unyevunyevu wakati wote. Naiweka kwenye jokofu wakati
natumia, baada ya wiki naimwaga na kutengeneza nyingine. Ningependa kushauri
wengine wanaopenda watumie pia wataona faida yake.
Lipstick: Nini siri yako kuwa na nguvu wakati wote?
Herieth: Ni mambo ya kawaida. Kwanza lazima nipate
usingizi wa kutosha, lazima nilale kwa saa kumi (10). Naingia kitandani saa
mbili (2) usiku. Marafiki zangu mara nyingine wananishangaa lakini nawaambia
nisipopata usingizi wa kutosha asubuhi macho yangu yanakuwa mazito. Pia nafanya
mazoezi ya viungo.
Lipstick: Tumesikia kuwa unashughulika na misaada
kwa watoto yatima. Hebu tueleze.
Herieth: Nimejifunza na kuiga kutoka kwa mama.
Tangu nikiwa mdogo nilikuwa namsikia na baadaye kuona mama anasaidia shule ya
watoto yatima kule kwetu Tanzania. Mama amesaidia wasichana kadhaa ambao
wengine wamemaliza masomo ya kidato cha sita (vi) na wengine wamekwenda kusomea
kozi mbalimbali. Nami nasaidiana na mama kuwalipia karo vyuo vikuu,
tunawanunulia vitabu, tunawapa pesa ya usafiri. Msaada huu utawasaidia katika
maisha yao.
No comments:
Post a Comment