Mchungaji
wa kanisa la Umoja wa Makanisa ya Ubatizo Lucas Machibya akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani ) kuhusu baadhi ya shughuli za
uraghabishi katika kijiji cha Pandagichiza.
Baadhi
ya waraghabishi wa kijiji cha Pandagichiza wakiwa na waandishi wa
habari za mtandaoni katika moja ya jengo la jiko la shule ya msingi
Pandagichiza ambalo limetoakana na juhudi zao za uraghabishi
Na Krantz Mwantepele ,Shinyanga
Si
mara nyingi viongozi wa kidini hujihusisha moja kwa moja na harakati za
kisiasa ila wamekuwa mstari wa mbele kukemea matendo yanayofanywa na
wanasiasa. Hawafanyi hivyo kwa bahati mbaya ila kutokana na nafasi yao
katika jamii, hususani kuwaongoza waumini wao kwenda mbinguni.
Hata
hivyo, hii haimaanishi hakuna kabisa viongozi wa dini waioamua
kujiingiza katika harakati za siasa ili kuleta maendeleo ya watu kwa
haraka na ufanisi. Mchungaji Lucas Machibya ni mmoja kati ya viongozi
wachache wa dini wanaoingia katika siasa.
Huyu
ni mchungaji wa kanisa la Umoja wa Makanisa ya Ubatizo lililopo katika
kijiji cha Pandagichiza chenye wakazi wanaokadiriwa 2,481, idadi kubwa
ikiwa ni ya wanawake wanaokadiriwa kufikia 1,476. Hiki ni moja ya vijiji
vilivyopo wilaya ya Shinyanga Vijijini, jimbo la Solwa.
Machibya
ni mmoja wa wachungaji waraghbishi toka mkoa wa Shinyanga ambao
uraghbishi wao umepelekea wananchi kumchagua kuwa mwenyekiti wa kijiji.
Kujibainisha kwake kama mtu mwenye uwezo wa kusimamia anachokiamini na
kushawishi wananchi kutambua majukumu na haki zao na jinsi ya kuzidai
vimekuwa nguzo yake kubwa ya kukubalika.
Kama
walivyo wananchi wengi wa kijiji chake, yeye ni mkulima mdogo ambaye
pia ni mwanachama wa Mtandao wa Wakulima Wadogo Tanzania (MVIWATA).
Kupitia mwaliko wa mkulima mwenzake, Elizabeth Edward, Machibya
amefanikiwa kupata maarifa ya uraghbishi na jinsi ya kufanya uraghbishi;
uwezo wa kuwashawishi na kuwahusisha ama kuwachokoza watu ili waweze
kujitambua na kutojiona wao ni wa jamii ya chini.
Sifa
iliyomfanya aalikwe kwenye mafunzo ya uraghbishi ni uwezo wake wa
kuhoji mambo mbalimbali pasipo kukata tamaa kama anavyosema mwenyewe:
“Mimi
ni mtu wa kuhoji vitu na si mtu wa kuridhika ama kukaa kimya n’napoona
kuna jambo sijalielewa. Kwa kweli yale mafunzo yalinifanya kujiona mtu
tofauti sana nikijilinganisha na nilivyokuwa awali. Nilijihisi tayari
nimekuwa mtaalamu wa masuala ya uwajibikaji na utawala bora.”
Kwa
kuwa wao ni wakulima, walianza uraghbishi wao kwa kutaka kujua nini
kinaendelea kuhusu bei ya pamba. mchungaji Machibya anaeleza ilivyokuwa:
“Kule
tulifundishwa jinsi ya kuuliza maswali. Na cha kwanza tulichotaka kujua
ni kwa nini bei ya zao letu la pamba imeshuka sana. Hili tuliliuliza
sisi sote, mimi na waraghbishi wengine.”
Hawakuishia
hapo tu bali wakaanza pia kufuatilia mapato na matumizi ya fedha za
kijiji toka kwa viongozi wao. Walifanya hivyo kwa kuwatembelea ofisini
na kuomba kupatiwa taarifa hizo na pia walitaka kufanyika mikutano ya
hadhara. Baada ya harakati hizo kushika kasi, iliwabidi waongeze watu
wengine zaidi kwa kuwatembelea majumbani kwao na kuwaraghbisha.
“Mchungaji
aliomba kunitembelea nyumbani na alipofika alinipatia elimu. Kimsingi,
alitaka nijitambue kwa kujua wajibu na haki zangu. Alinitaka nisiogope
kuuliza maswali kwenye mikutano kwa kuwa tuna uhuru wa kufanya hivyo.
Nikajua kuwa nina wajibu kuuliza na kujua mapato ya fedha za kijiji na
na matumizi yake kuwa hiyo ni haki yangu,” anaeleza Bw. Daudi Denis toka
kijiji cha Pandagichiza.
Kufanikisha
haya yote kumewajengea uaminifu mkubwa sana waraghbishi na baadhi yao
wamekuwa wakishirikishwa katika vikao muhimu vya maendeleo na serikali
yao ya kijiji. Baadhi yao wametokea kuaminika zaidi na jamii kiasi cha
kuombwa wagombee nyadhifa mbalimbali za uongozi wa serikali na ndani ya
vyama vya siasa kama ilivyokuwa kwa mchungaji Machibya.
Hivyo
basi, waraghbishi wengi wanaojihusisha na siasa wamejikuta wakinasa
katika mtego huu wa migogoro ya kimaslahi kati ya shughuli zao za
uraghbishi na zile za kisiasa kwa kuchukiwa na baadhi ya watu
wanaotofautiana kimlengo wa kisiasa na kuonekana wasaliti na watu
wasiokuwa na misimamo.
Wakati
mwingine wanachukiwa ikidhaniwa kuhoji kwao mara kwa mara ni njia ya
kujitafutia mtaji wa kisiasa na si kuwatumikia wananchi na kuibua maovu
kwa maslahi ya jamii nzima na kwamba uraghbishi unawanufaisha wao
binafsi na vyama vyao tu.
Uraghbishi
ulimuingiza mchungaji Machibya kwenye mgogoro mkubwa na walinzi wa
jadi, Sungusungu. Katika maeneo mengi ya Kanda ya Ziwa walinzi hawa
wamekuwa na nguvu kubwa na wakati mwingine wanaweza kutoa adhabu kali
kwa yeyote anayebainika kutenda kosa.
Tofauti
hiyo na Sungusungu ilisababisha yeye na waraghbishi wengine sita
kukamatwa na kutozwa faini ya shilingi laki tano na elfu sitini
(560,000/=) kwa mpigo kwa kisingizio cha kuvuruga amani katika kijiji
hicho. Hii ni kwa sababu tu walikuwa wanauliza maswali kuhusu mapato
yanayotokana na faini na michango mingine toka kwa wanakijiji.
Vitisho
na maonyo ya uongozi viliwapunguza kasi baadhi ya waraghbishi na
kuingiwa hofu kiwa wangefikishwa pabaya zaidi ya hapo. Ila mchungaji
Machibya hakuishia hapo bali aliendelea na shughuli hizo kama kawaida.
Baadaye aliteuliwa kuwa katibu wa mtandao wa waraghbishi na huko ndiko
alikojizolea uaminifu na umaarufu zaidi baada ya kuanza kujihusisha na
kuhoji mambo makubwa ya kiutawala na utendaji kijijini hapo.
Hiyo
ilimwongezea hamasa ya kuendelea kuwatumikia watu kwa kuongeza juhudi
katika shughuli za uraghbishaji na kufikia hatua ya kuombwa na wananchi
kugombea wadhifa kichama (siasa) na uongozi katika serikali ya kijiji.
Na
mwaka 2014 wakati wa mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa
ukiendele, ndipo yeye alijikita kwa dhati kuomba nafasi ya kugombea
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kufanikiwa kuteuliwa kugombea.
Akielezea ilivyokuwa, mchungaji Machibya anasema:
“Wapinzani
wangu walipojua kwamba mimi ndio nimepitishwa waliamua kujitoa katika
vyama vyao na kuniunga mkono. Hii kwa sababu hawakuona sababu ya
kupingana nami kwa kuwa wanafahamu uwezo na umakini wangu kiutendaji na
kiuwajibikaji.”
Matokeo
ya harakati hizo ni kwamba Mchungaji Machibya alichaguliwa kwa kishindo
kuwa mwenyekiti wa kijiji na baadaye alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa
wenyeviti wa wilaya nzima. Sanjari na nafasi mwenyekiti wa kijiji,
aliendelea pia kushika nyadhifa nyingine ikiwamo kuwa mraghbishi
kiongozi na mchungaji.
Hizi
ni nyadhifa nyingi zinazoambatana na majukumu mengi kwa mchungaji
Machibya hivyo kujikuta kwenye mazingira magumu sana ya kutumikia
nyadhifa zote. Lakini pia alipata upinzani mkali sana kutoka kwa
viongozi wengine na hata wakati mwingine kushindwa kusimamia kwa pamoja
majukumu yote.
Huku
ni mraghbishi na huku ni mwenyekiti wa kijiji. Hii haikuwa changamoto
ndogo kwake. Akifafanua hilo, mchungaji Machibya anasema:
“Kwa
sababu nilikuwa kiongozi wa waragbishi ilikuwa ni kama nayajua maswali
kabla ya mtihani na wenzangu walikuwa wanashindwa kuhoji vizuri kwa kuwa
mie ni kiongozi wao. Ndipo nikaamua kujitoa uongozi na kuwa mraghbishi
wa kawaida, lakini sikuishia hapo nikajivua na majukumu ya uchungaji wa
kanisa japo ni shughuli niliyoipenda sana na kuwa mzee wa kanisa
kawaida.”
Kwa
haraka haraka, unaweza kusema shughuli ya kuhoji mwenzio inafanana na
kuhojiwa wewe binafsi. Mwanzoni alipata ugumu kidogo kwa sababu kila
mwananchi alikuwa anategemea mabadiliko ya haraka wakati vitu vingine
vilikuwa kimfumo zaidi. Hiyo ilimfanya achelewe kutoa majibu ya haraka.
Na
ili asiangukie kwenye dimbwi la lawama, alihakikisha anakuwa muwazi kwa
wananchi na viongozi wake wa karibu katika kila jambo.
Kuna
mbinu kadhaa alizotumia ikiwa ni pamoja na kuteua viongozi wa
halmashauli ya kijiji wanaoendana na falsafa yake ya uwazi na
uwajibikaji na pia aliendelea kuwatumia waragbishi wenzake katika kuibua
mambo pale alipohisi yanakwama.
Mchungaji
Machibya anafahamu kwamba yeye kama kiongozi ana wajibu wa kuwa na
uelewa wa mambo mbalimbali ikiwemo sheria na sera za nchi. Kwa kuelewa
hilo, alipoanza kutafuta fursa za mafunzo ya uongozi na kukutana na
mashirika mbalimbali yaliomwezesha kupata elimu.
Hakuishia
hapo bali aliendelea kujenga mizizi ya waraghbishi wengi zaidi na mpaka
sasa amefanikiwa kuwajengea uwezo wenyeviti wenzake 40 kati ya 126 wa
wilaya nzima, na bado anaendelea kutafuta maarifa mengine ili awape
wenzake.
Kwa
nafasi yake, anatafuta wadau na mashirika yenye ujuzi huo ili awezeshe
wenyeviti wote kupata mafunzo kwani wengi wao wanatawala wananchi
kimazoea tu. Hawana ufahamu wa namna nzuri ya kutekeleza majukumu yao.
Kwa
misingi hiyo, mchungaji Machibya ameamua kutumia uraghbishi kama nyenzo
ya kumuongezea ufanisi katika majukumu yake na si kutengeneza uadui na
waragbishi kama ilivyo kwa viongozi wengi wa vyama na serikali. Kwa
mfano huu, tunapata picha halisi ni kwa namna gani uragbishi
ukichukuliwa kwa mtazamo chanya unakuwa nyenzo muhimu ya kuongeza chachu
ya utawala bora katika serikali zetu za mitaa, kijiji na taifa kwa
ujumla. Na kwa sasa, anapambana na mambo makuu matano ikiwa ni pamoja na
mradi wa maji utakaomwezesha kukusanya kiasi cha shilingi 500,000.
Pamoja
na mapato mengine yanayokusanywa na Sungusungu pamoja na kuhamasisha
kusomeshwaji kwa wingi kwa watoto wa kike. Na tayari hatua za makusudi
za kuhakikisha kwamba malengo ya kuongeza mapato na hivyo kulipia watoto
wa kike kuhudhuria shuleni zimeshachukuliwa.
Hii
ikiwa ni pamoja kupunguza adhabu kali za viboko, kuunda upya uongozi wa
Sungusungu. Kwa upande wa mapato, wameweka mikakati ya wazi ya
kuhakikisha mapato yanayopatikana yanasomwa mbele ya wananchi. Kwa
upande wa shule, kila mzazi na jamii nzima imeandaliwa mikakati ya
makusudi kuwawajibisha wale wote wanaoshindwa kuwapeleka watoto wa kike.
Waraghbishi wamekuwa chachu kubwa katika uvumbuaji wa taarifa pamoja na
uelimishaji pia.
Jambo
la kwanza kwa kiongozi yeyote anayetaka mafanikio katika uongozi wake
ni kutanguliza maslahi ya wananchi kwanza kabla ya maslahi binafsi au ya
chama chake. Kinyume na hivyo anaweza kutia doa hata huo uraghbishi
wake. Utu wa mtu hupimwa kwa matendo yake na hata mtazamo wa watu
anaowaongoza.
Viongozi
wengi wanatumia uraghbishi kama nyenzo ya kujijengea umaarufu wakati
wenyewe ni kama hulka ama tabia ya mtu kupenda haki na mambo yakiwa
yanasonga. Kwa hiyo unaweza kukuta waraghbishi wengi sana kama matendo
yako yatalenga kukomboa watu na si maslahi binafsi.
Jambo
lingine ambalo alisisitiza ni kwamba hawa viongozi wawe na utamaduni wa
kutafuta maarifa na si kusubiri fursa za kuletewa tu na wahisani.
Kiongozi bora ni lazima aendane na mabadiliko ya kila siku na si
kuongoza watu kwa mazoea. Binadamu wanabadilika kila siku, hivyo kuna
umuhimu wa kuonesha tofauti kati ya kiongozi mraghbishi na wa kawaida.
Hiyo itaibua mwamko mkubwa wa viongozi wengi kuwa waraghbishi.
Kiongozi
asiyejua sheria na sera za nchi ni sawa na kipofu. Siri ya elimu na
ufahamu ipo kwenye maandishi, mafunzoni na kwenye semina elekezi kwani
bila kufanya hivyo utauchukia uraghbishi.
No comments:
Post a Comment