Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa akiwa
katika kikao kazi na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara. Kulia kwake ni
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati, Dk. Juliana Pallangyo na
Kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Madini, Profesa
James Mdoe.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (Kulia)
akimkabidhi mwongozo wa majukumu ya kazi Naibu Katibu Mkuu
anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe. Wanaoshuhudia ni Wakuu wa
Idara na Vitengo wa Wizara.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (Kushoto)
akimkabidhi mwongozo wa majukumu ya kazi Naibu Katibu Mkuu
anayeshughulikia Nishati, Dk. Juliana Pallangyo. Wanaoshuhudia ni Wakuu
wa Idara na Vitengo wa Wizara.
Na Veronica Simba
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa amesema ni
jukumu la watendaji wote wa Wizara kuhakikisha wananchi wananufaika
ipasavyo na rasilimali zinazotokana na sekta husika.
Aliyasema hayo hivi karibuni katika kikao chake cha kwanza cha kazi na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara.Profesa
Ntalikwa alisema pamoja na jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa
zikifanywa na Wizara kuhakikisha wananchi wananufaika ipasavyo na
rasilimali hizo, bado kuna manung'uniko kutoka kwa jamii hali ambayo
inaashiria kuwa jitihada zaidi zinahitajika.
Akizungumzia
sekta ya nishati, Profesa Ntalikwa alisema wananchi wanalalamika kuhusu
kukatika-katika kwa umeme, gharama kubwa za umeme na ukosefu wa umeme
wa uhakika na wa kutosha. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, alisema
kunahitajika kuwepo miradi mipya ya kuzalisha umeme.
Aidha,
alisema kuwa moja ya malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa wananchi
ni kufufua na kujenga viwanda ili kukuza na kuimarisha uchumi. “Viwanda
ni umeme, hivyo hatuna budi kuzalisha umeme wa kutosha.”
Kwa
upande wa sekta ya madini, Katibu Mkuu Ntalikwa alisema jitihada
zinatakiwa ili kufikia malengo ya kuongeza mchango wake katika pato la
taifa kutoka asilimia 3.5 ya sasa hadi kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka
2025.
“Tunapaswa kuweka mikakati thabiti itakayotuwezesha kufikia malengo hayo na kuyavuka ikiwezekana,” alisema.Profesa
Justin Ntalikwa ni miongoni mwa Makatibu Wakuu wapya wa Wizara
mbalimbali walioteuliwa na kuapishwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli.
Manaibu
Katibu Wakuu wapya wa Wizara ya Nishati na Madini walioteuliwa na
kuapishwa na Rais Magufuli ni Profesa James Mdoe anayeshughulikia sekta
ya Madini na Dk. Juliana Pallangyo anayeshughulikia sekta ya Nishati.
No comments:
Post a Comment