Monday, January 18, 2016

DC AWATAKA MADIWANI WASHIRIKIANE KUMALIZA MIGOGORO WILAYANI SIMANJIRO

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Mweri akizungumza juzi kwenye baraza la madiwani wa wilaya hiyo (katikati) ni Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Jackson Sipitieck na Makamu Mwenyekiti Albert Msole.  
Diwani wa Kata ya Ruvu Remit Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Alamayani Ranga akisoma taarifa kwenye baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo juzi juu ya uboreshaji wa huduma za jamii

Na Woinde Shizza, Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Mahmoud Kambona amewataka madiwani wa kata 18 za wilaya hiyo kushirikiana na maofisa watendaji wa vijiji vyao kuhakikisha migogoro inakwisha.
Kambona aliyasema hayo juzi wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo na kuagiza mipaka ya vijiji na vitongoji vya miji midogo ya Orkesumet na Mirerani izingatiwe kwa kupimwa.
Alisema kila diwani akishirikiana na maofisa watendaji wa vijiji wataweza kumaliza migogoro hiyo na maeneo ya kilimo na mifugo yabainishwe na kuhakikisha suala la mifugo kuzagaa likomeshwe ikiwemo punda na ng’ombe.
“Mifugo inazagaa ovyo na kuharibu mazao, lidhibitini hilo kwa kutumia kanuni ndogo zetu, kwani mifugo inaachiwa sana na ukitembelea sehemu nyingine unakuta punda wanaingia hadi kwenye madarasa ya shule,” alisema Kambona.
Pia, Kambona amemuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Lucas Mweri kuwapangia wakuu wa idara, vitengo na watumishi wengine wawe walezi wa kata mbalimbali ili wawe wanazitembelea na kutoa ushauri.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Jackson Sipitieck alisema hivi sasa madiwani na watumishi kwa pamoja wanatakiwa kujipanga kikamilifu ili kuhakikisha wananchi wa kata za eneo hilo wanapatiwa maendeleo.
“Tujipange kikamilifu kwa pamoja na kuhakikisha kuwa wananchi wetu wanapata huduma stahiki, kwani sisi tulichaguliwa kwa ajili ya kutumikia jamii ya Simanjiro ili wapate maendeleo kwenye sekta mbalimbali,” alisema Sipitieck. 

No comments: