Monday, December 21, 2015

WASHINDI KAMATI ZA KUDHIBITI UKIMWI PANGANI WAPATA ZAWADI


Meza kuu,wa kwanza kulia ni Meneja wa redio PANGANI FM Maimuna Msangi, wa pili kutoka kulia ni Mkurugenzi wa shirika la UZIKWASA ambalo limeratibu tamasha hilo VERA PIEROTH,wa tatu ni Kaimu mgeni Rasmi ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya PANGANI Bi Patricia, na wanne ni Mratibu wa masuala ya UKIMWI wilaya ya PANGANI.

Na Mwandishi wetu

Shirika lisilo la kiserikali Wilayani Pangani la UZIKWASA linalojishughulisha na kuziwezesha kamati za kudhibiti Ukimwi, VMACK limezawadia kamati bora za kudhibiti ukimwi Wilayani humo.

Sherehe hizo zimefanyika sanjari na kuwazawadia kijana bora mfano wa kuigwa na mama bora mfano wa kuigwa.

Katika sherehe zilizofanyika kijiji cha Jaira,K ata ya Madanga wilayani Pangani na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wananchi na viongozi kutoka halmashauri ya Wilaya ya Pangani mgeni rasmi alikuwa Kaimu Afisa Maendeleo Wilaya ya Pangani, Bi.Patricia Kinyange.

Akizungumza katika hadhara hiyo Bi. Kinyange amelipongeza shirika hilo kwa kuzijengea uwezo kamati hizo ambazo zinafanya kazi kubwa kwa jamii.
 
Mkurugenzi wa shirika la UZIKWASA, VERA PIEROTH akizungumza jambo wakati wa kuwakaribisha wananchi wa PANGANI katika tamasha hilo.



“Kwa kweli shirika la UZIKWASA nawapongeza sana, mnafanya kazi kubwa kwenye jamii ya Pangani na kwakweli watu wa Pangani wanapaswa kujivunia uwepo wenu. Nimeshangaa kuona mambo makubwa yanayofanywa na kamati kutokana na elimu mnayowapatia,mnastahili pongezi kubwa”alisema Bi.Kinyange.

“Mfano mzuri mimi ARUSHA nilipokua nafanya kazi, kamati zipo lakini kwakweli wamelala,unakuta kamati inakutana mara mbili kwa mwaka mzima,lakini huku ni zaidi ya mara kumi,kwakweli nimeshangaa sana,nyinyi ni shirika ambalo linafaa kuigwa,lakini wanakamati niwaombee mzidishe juhudi msiwaangushe wanauzikwasa na sisi kama halmashauri tutajitahidi kushirikiana kwa karibu kabisha na UZIKWASA ili kuendeleza juhudi hizi.”

Katika hatua nyingine mgeni huyo rasmi amempongeza kijana aliyeibuka mshindi katika shindano la kijana bora mfano wa kuigwa na kumtaka kuendeleza juhudi zake na kwamba Halmashauri watamtumia kama darasa kwa ajili ya vijana wengine kujifunza kutoka kwake.
 
Burudani ya ngoma ilikua sehemu ya tamasha hilo.


Kwa upande wao kamati iliyoibuka mshindi kwa mwaka wa tatu mfululizo kutoka katika kijiji cha Mseko wamesema umoja na mshikamano ndio nguzo pekee ya ushindi wao,na kwamba shukrani pekee zinapaswa kwenda kwa UZIKWASA kwa mafunzo na ufuatiliaji wao kwani ndio vilivyowafanya kutekeleza mipango waliojiwekea kama wanakamati hadi kuibuka washindi.

‘Naweza kusema kamati yetu imejitoa sana,wanakamati wanatumia muda wao mwingi wa ziada katika kuhakikisha tunatekeleza mipango tuliojiwekea,lakini pia msukumo mkubwa ni kutoka UZIKWASA kwakweli tunawashukuru sana”Alisema Afisa mtendaji mseko.

Kwa upande wake Mratibu wa shughuli hizo kutoka shirika la UZIKWASA ambaye pia ni Afisa wa mradi wa jinsia na uongozi wenye mabadiliko, Bi.Salvata Kalanga amesema haikuwa kazi rahisi kuzipata kamati bora 8,kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo kwa washiriki 15,lakini wanashukuru kumpata mshindi ambaye wanaamini anastahili kutokana na kazi waliyoifanya.
 
Wanakamati wa kijiji cha Mseko katika picha ya pamoja baada ya kutangazwa washindi, na wameibuka washindi kwa mwaka wa 3 mfululizo.


Katika sherehe hizo,mshindi wa kwanza amepata zawadi ya ngao,pamoja na fedha taslimu shilingi laki sita,mshindi wa pili alipata laki 4 na nusu,na mshindi wa tatu alipata shilingi laki 4.

Sherehe ya kuzizawadia kamati bora za kudhibiti UKIMWI hufanyika kila mwaka chini ya shirika la UZIKWASA,lengo ni kuzipa motisha kamati hizo ili zifanye vizuri zaidi.

Mashindano haya na tamasha hili husimamiwa na kuwezeshwa na Asasi ya UZIKWASA Pangani kwa lengo na Kuamsha hamasa, kuchochea, kutafakari na kujifunza na kujenga uwajibikaji miongoni mwa vijana, akinamama na Kamati za Kudhibiti UKIMWI jinsia na uongozi za vijiji.

Mashindano haya huanza baada ya UZIKWASA kuwezesha kamati hizi kwa kuzijengea uwezo na baadae maafisa wa UZIKWASA kuzitembelea kamati hizo na makundi yaliyotajwa na kupima utekelezaji wake kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na kukubaliwa na wadau hao.

Kamati, vijana, na akina mama walioanishwa kufanya vizuri hutembelewa na kamati nyingine kuweza kujifunza kwa pamoja na kujirudhisha kwa utekelezaji wa kamati hizo. Pia kwa vijana na wakinamama hutembeleana na kupeana taarifa za utekelezaji na kujifunza kwa pamoja. Kamatai hizo na hao vijana na akinamama huchujwa na kubaki wachache ambao wanatekeleza vizuri zaidi.

Baada ya zoezi hilo la kutembeleana walioanishwa huitwa Pangani na kukutanishwa na waamuzi ambao huwasikiliza na kuchambua washindi.

Mwaka 2015 kamati 12 zilichaguliwa kuingia kwenye ushindani huo ambazo ni Mseko, Mwembeni, mkwajuni, mbulizaga, Bweni, mzambarauni, Mtonga, Mikocheni, Langoni,Tungamaa, Sange na Jaira.

Akina mama bora waliongia sita bora kati ya 33 ni kutoka Masaika, Kwa kibuyu, Stahabu, Mwembeni, Mtonga na Langoni. (watatu watazawadiwa)

Vijana bora waliongia sita bora kati ya 33 ni kutoka Msaraza, Kimanga, Mikocheni, Mseko, Boza na Mivumoni.(watatu watazawadiwa).

Mashindano haya yalianzishwa mwaka 2010 ili kuleta msukumo, ushindani na chachu ya utekelezaji wa mipango ya vijiji ya ukimwi na maendeleo ya kijiji kwa ujumla na kuotesha mbegu ya uwajibikaji.

Mwaka 2010 Kamati ya Sanga iliibuka mshindi, mwaka 2011 kamati ya Langoni, iliibuka mshindi, mwaka 2012 kamati ya Langoni iliibuka mshindi tena. Mwaka 2013 kamati ya Mseko iliibuka mshindi na mwaka 2014 Mseko iliibuka mshindi tena.

Mwaka huu wa 2015 mchuano ulikuwa mkubwa na kamati zimejituma na kuwajibika katika utekelezaji wa mipango yao ya maendeleo pamoja na kuyasaidia makundi mbalimbali yenye uhitaji.

Kamati kumi 15 zimetekeleza vizuri. Kamati 12 zimetekeleza wastani. kamati 6 ikiwepo, Ushongo, Kipumbwi, Masaika, Kigurusimba, kimang,a na Mivumoni zinahitaji msukumo wa ziada kwa Kukosa uwajibikaji.

Mashindano haya yameleta msukumo katika shughuli zote za kiuongozi na maendeleo ya vijiji. Palipo na uongozi mzuri na utekelezaji mzuri unakuwepo pia.

UZIKWASA itaendelea kuwajengea uwezo viongozi wangazi zote na wanajamii kuweza kujitathmini, kuzama na kujichunguza na kuweza kufanyia kazi changamoto za kiuongoza na kuwezesha maendeleo katika jamii. Suala la kupinga unyanyasaji wa wanawake na watoto wa kike litapewa kipaumbele.
Kaimu mgeni rasmi ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii Bi.Patricia akizungumza na wananchi waliohudhuria katika tamasha hilo.
Washehereshaji wa tamasha hilio, Pili Mlindwa na Shabani Kizamba wakiwajibika.
Mkurugenzi wa shirika la Uzikwasa na Meneja wa Pangani FM.
Mmoja wa wanakamati ya VMACK ya kijiji cha mseko akicheza kwa furaha mbele ya meza kuu baada ya kutangazwa washindi,
Kaimu Mgeni rasmi Bi.Patricia akiwa ameshika ngao ambayo ni zawadi ya washindi wa VMACK kwa mwaka 2015.
Katibu wa kamati hiyo akipokea zawadi, Ngao na Hundi ya shilingi laki sita.
Vijana bora wa mfano wa kuigwa walioingia katika hatua ya 3 bora, na aliyeibuka mshindi ni kijana aliyevaa tshirt rangi ya njano.
Wamama walioingia katika tatu bora mama mfano wa kuigwa, na aliyeibuka mshindi ni mama ambaye ameshikilia pochi, ambaye anajulikana kwa jina maaarufu kuti kavu.
Hapa akipokea zawadi ya hundi ya shilingi laki 1 kwa kua mama/mwanamke bora mfano wa kuigwa kwa mwaka 2015.
Mwenyekiti wa kijiji cha Jaira akigawa zawadi ya sare za shule kwa viongozi wa vijiji vyote vya Wilaya ya PANGANI kwa niaba ya Aliyekua kijana bora mfano wa kuigwa mwaka 2013-2014,ambayo aliahidi kwa watoto yatima alipochaguliwa.
Wamama wakifurahia jambo.
Sehemu ya wananchi waliohudhuria katika tamasha la kuzizawadia kamati bora za kudhibiti UKIMWI, kijana bora na mama bora wa mfano wa kuigwa kwa mwaka 2015 zilizofanyika katika kijiji cha JAIRA kata ya MADANGA Wilayani PANGANI.
Waandishi wa habari kutoka redio PANGANI FM, iliyochini ya shirika la UZIKWASA wakifuatilia kwa makini tamasha hilo (waliovaa tshirt za PANGANI FM).
Wananchi wa Pangani waliofika katika kijiji cha Jaira wakifuatilia kwa ukaribu tamasha hilo.

No comments: