Monday, December 7, 2015

Wasanii SHIWATA kumpa Magufuli ufagio wa chuma

Na Mwandishi Wetu

MTANDAO wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) umeamua kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano, John Magufuli la kufanya usafi nchini siku ya sherehe za Uhuru 9/12/2015 kufagia, kulima, kuzoa taka na kusafisha maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim Taalib alisema jana Dar es Salaam kuwa usafi huo utaanzia makao makuu yao Ilala Bungoni, soko la Ilala,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mmachinga Complex, Soko la Mitumba Karume, Kariakoo, Mnazi Mmoja, Soko la Kisutu, Posta ya zamani, soko la samaki Feri mpaka Ikulu.

Alisema zaidi ya wanachama 300 wa SHIWATA kutoka fani mbalimbali za wanamichezo, wasanii, waandishi wa habari na wadau wamethibitisha kushiriki kufanya usafi huo kutokomeza ugonjwa wa kipundupindu unashika kasi katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam.

Taalib alisema kazi ya usafi huo itaanza saa 1.30 asubuhi kila mmoja aje na fagio, jembe, reki, au zana yeyote ya kufanyia usafi na kuvaa mavazi rasmi ya kufanyia kazi za usafi.

"Baada ya kukamilisha kazi ya usafi tutamkabidhi Rais Dkt. Magufuli fagio maalum wa Chuma kumuunga mkono katika operesheni aliyoianza ya kupambana na mafisadi na wezi wa mali ya umma" alisema Mwenyekiti Taalib.

Alisema fagio hilo la chuma ni mfano wa zana ambayo itamwezesha kuwafagia na kuwatokomeza mafisadi wote hapa nchini wanajilimbikizia mali wakati watanzania wakiishi maisha ya magumu ya mlo mmoja kwa siku.

Mwenyekiti Taalib alisma maazimio ya kumuunga mkono Dkt. Magufuli kwa vitendo ilifanyika Novemba 28 katika mkutano Mkuu wa mwaka wa SHIWATA uliofanyika Dar es Salaam ambapo wanachama zaidi ya 300 waliohudhuria kwa pamoja waliunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa Awamu ya Tano kupambana na wezi wa mali ya umma.

Alisema wasanii hao bila kujali itikadi zao kisiasa wanamuunga Dkt. Magufuli na wameahidi kumsaidia kufichua wote wanaotuhumiwa kula fedha za umma ili kuleta maendeleo ya kweli nchini.

SHIWATA yenye wanachama zaidi ya 8,000 nchini wanamuunga mkono Rais Magufuli kwa uongozi wake na wanamkaribisha kujiunga na wasanii katika kijiji cha Mwanzega Mkuranga chenye ukubwa wa hekari 300 za makazi ambapo mpaka sasa wamejenga nyumba 137 kati ya hizo 17 zinakabidhiwa Desemba 12, mwaka huu.

Pia Shiwata inalo shamba la hekari 500 katika kijiji cha Ngarambe, Mkuranga ambako wanatarajia kulima mazao mbalimbali.

No comments: