Watendaji wa Kituo cha Maendeleo cha Jamii ya Uchunga wilayani Kishapu wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi mbele ya jengo la kituo hicho likiwa limekamilika kutokana na michango yao ya fedha na nguvu kazi.
Na Krantz Mwantepele ,Kishapu
Mabadiliko katika jamii yoyote kwa kiasi kikubwa huchangiwa na ongezeo la mahitaji ya binadamu katika mambo mbalimbali. Kwamba, kadri dunia inavyopitia mabadiliko, kadiri ile ile changamoto, mahitaji na huduma katika jamii husika huongezeka.
Ili kufikia malengo yanayotokana na misukumo na mageuzi yasiyokwepeka, binadamu amelazimika kubuni mikakati mbalimbali ya maendeleo. Si hivyo tu, mabadiliko haya yamemfungulia binadamu fursa ya uthubutu wa kujaribu mambo mbalimbali, siyo tu kwa faida yake, bali jamii nzima inayomzunguka.
"Sikutegemea kama siku moja katika maisha yangu nitapata wazo ambalo lingebadili na kushawishi watu kuchukua hatua kwa mustakabali wa jamii.”
Hiyo ni kauli ya mraghbishi Revocatus Richard ambaye pia, kitaaluma ni mwalimu katika shule ya msingi Uchunga. Richard alitoa kauli hiyo baada ya kupitia mafunzo ya uraghbishi na mwalimu mwenzake, Restusta Katobesi, ambao baadaye kwa pamoja, walianzisha Kituo cha KIMAJU (Kituo cha Maendeleo cha Jamii ya Uchunga) kwa kushirikiana na uongozi wa kijiji na wananchi. Na hilo ndiyo lilifanya achaguliwe kuwa Mkurugenzi wa kituo hicho.
Walimu hao walikuwa miongoni mwa waraghbishi 30 walioshiriki mafunzo ya uraghbishi yaliyotolewa mwezi Machi, mwaka 2012 wilayani Kishapu katika mkoa wa Shinyanga. Kutokana na faida na maarifa waliyoyapata kwenye mafunzo hayo, walimu hao waliamua kuunda umoja uliokuwa chachu ya kuanzishwa kituo hicho cha maendeleo.
Mwanazuoni Sarah Earl, aliwahi kusema: "Maendeleo ni watu na mazingira yao. Kwamba, kusingekuwa na maana iwapo barabara, hospitali, shule na miradi mingine ya maendeleo inayojengwa kwa ajili ya watu isingetumika."
Kwa mantiki hiyo, miradi yote ya maendeleo, ikiwamo Chukua Hatua ni kwa ajili ya ustawi wa maisha ya watu. Kwa kuwa kiini cha maendeleo ni watu. Shabaha kubwa ya mradi huu wa Chukua Hatua ni kuhakikisha wananchi (waraghbishi) wanajielewa na kujitambua katika kutimiza majukumu yao na kupata haki zao zikiwamo huduma bora za kijamii na kuhakikisha wananufaika na rasilimali zao. Pia unawasaidia kuwawajibisha viongozi wao ili watimize majukumu yao ya kuhamasisha maendeleo na kutatua shida za wananchi.
Mraghbishi ni mwananchi anayeleta uhai mpya ndani ya jamii kwa kutambua matatizo na kupendekeza njia sahihi za kuyatatua.Katika kipindi cha miaka mitano ya mradi, zaidi ya waraghbishi 380 wameleta uhai katika jamii zao, hususani kwenye vijiji vya mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Geita na Arusha hasa katika wilaya ya Ngorongoro.
Tafsiri ya uhai huu ni pamoja na kuwachukulia hatua viongozi wabadhirifu, watendaji wabovu, kuandaa midahalo, kudai huduma bora za kijamii, kuibua na kufuatilia matatizo mbalimbali katika vijiji vyao kama ambavyo waraghbishaji Richard na Katobesi wamefanya.
Uraghbishi Kijiji cha Uchunga
Baada ya kupatiwa mafunzo ya uraghbishi, walimu hawa walirudi kijijini kwao wakiwa na jukumu moja la kutambua changamoto zinazoikabili jamii yao na kupendekeza nini kifanyike wakitumia nafasi na uwezo walio nao.
Kikubwa walichoangalia ni mustakabali wa mtoto wa Kijiji cha Uchunga, kwa maana ya nafasi ya mtoto, ikiwamo ya kufahamu huduma anazopata.Katika kufikiria sehemu ya kuanzia na ili kumpa mtoto wa kike nafasi katika jamii, hasa ya kuongoza, walianza na wanafunzi wa shule wanayofundisha, Uchunga.
“Nimepata bahati ya kuwa mwalimu mkuu msaidizi mara kadhaa na nimetumia fursa hiyo kuleta mabadiliko, nikianzia kubadilisha utaratibu wa kuchagua viongozi wa wanafunzi katika shule yetu," alisema Richard na kuongeza:
"Kwanza tulibadilisha wazo la Kaka Mkuu na badala yake tukasema tutakuwa na Kiranja Mkuu, ili kutoa fursa kwa wanafunzi wa kike kushika nafasi za uongozi wa wanafunzi."
Hadi sasa chaguzi mbili za kidemokrasia za kuchagua viongozi wa wanafunzi zimefanyika shuleni Uchunga Julai 2012 na Mei 2013.
Katika kuhakikisha wanaendeleza mawazo hayo, waraghbishi hao walikuja na wazo la kujenga kituo cha kujisomea. Walianza kuwatembelea wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Uchunga wanaoishi katika kijijini hapo.
Baadhi ya wananchi na wajumbe wa Kituo cha Maendeleo cha Uchunga wakiwa mbele ya kituo kabla hakijaezekwa na mabati.
Ili kufikia malengo yao, waliomba ushirikiano, siyo tu kwa walengwa ambao ni wanafunzi, bali kutoka kada zingine ndani ya jamii.
Akielezea jinsi walivyoanza, mraghbishi Katobesi alisema:
“Tulikutana na wanafunzi na kuunda umoja wa kikundi wa Wanafunzi wa Sekondari Uchunga (UWASU). Kikundi hiki kiliamsha hamasa kwa wanafunzi waliokukubali kujitolea kufanya kazi.”
Na baadhi ya wanafunzi hao wametembelea shule nyingine na kuhamasisha wenzao kujitolea kusaidia kazi mbalimbali kama kuchota maji na kuokota mawe kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kituo hicho cha kujisomea.
Ndani ya jamii yoyote kuna mamlaka, hivyo ili malengo yao yatimie kuliwalazimu waraghbishaji hao kupata ruhusa kutoka kwa walimu na aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji wakati huo, Mahona Punguja.
“Baada ya kutoka kwenye mafunzo yao, walikuja kuzungumza na mimi kuhusiana na mambo waliyojifunza na jinsi watakavyoleta mabadiliko. Nilikubaliana nao na kuweka utaratibu wa kuwashirikisha wazazi kama wadau muhimu na makundi mengine maalumu,” alisema Punguja.
Makundi maalumu ni pamoja na watumishi wa uma, kwa maana ya walimu na mtendaji wa kijiji na kata, wazee maarufu, viongozi wa dini, vijana na wajumbe wa halmashauri ya serikali ya kijiji. Waraghbishi hawa kwa ushirikiano na uliokuwa uongozi wa serikali ya kijiji waliweza kukutana na makundi hayo ili kuwaelimisha kuhusu wazo la kituo cha kujisomea. Baada ya kila kundi kukutana na waraghbishi, uliitishwa mkutano wa pamoja wa kujadili jambo hilo na kamati ikaundwa ya kusimamia mchakato mzima. Kamati hii ilichaguliwa kwa kila kundi kuwa na mwakilishi wake.
“Njia ya kwanza ilikuwa ni kukusanya fedha, kisha kuwaomba wananchi kuchangia nguvu zao. Kila mmoja kwa nafasi yake alijitolea. Wengine tulisomba mawe na kuchimba msingi. Wanawake walileta vyakula kwa ajili ya mafundi ambao nao walijitolea pia utaalamu wao bure”, anaelezea Michael Butu, Mwenyekiti wa Kituo cha KIMAJU.
Wanajamii waliohamasika waliombwa kuchangia kila mmoja Shilingi 10,000 za Kitanzania, ingawa baadhi walitoa nusu ya mchango huo. Kila kitongoji kiliombwa kuchangia Shilingi 60,000. Michango hii ilikusanywa baada ya kuundwa kwa nguvu ya pamoja na wenyeviti wa vitongoji. Kati ya vitongoji vitatu, viwili vilikamilisha ahadi zao.
Harakati hizi ziliwezesha wanajamii kujenga kituo hadi ngazi ya linta, kabla ya mlezi wa kituo hicho, Charles Dida kutoa shilingi 355,000 kama mkopo kwa ajili ya kununua mabati na mbao.
“Nilipoona jengo letu linasuasua, niliamua kujitolea kufanikisha ujenzi. Niliamua kumshirikisha mke wangu, ambaye aliunga mkono uamuzi wangu kwa kujua mafanikio yatakayopatikana ni ya jamii nzima,” alisema Charles Dida.
Katika hili tumejifunza mahusiano yaliyopo baina ya baba na mama katika kufanya maamuzi ya pamoja. Ni tofauti na mfumo dume uliozoeleka katika jamiii ya kisukuma. Na mpaka sasa kituo kimeweza kulipa kiasi cha Shilingi 110,000 na hivyo bado kinadaiwa Shilingi 245,000.
Ili kuhakikisha kituo kinaendelea kutoa huduma kwa watoto wa Uchunga wajumbe wa kamati tendaji wanafanyakazi kwa kujitolea kwa kuwa wao kuwa sehemu ya jamii ya wananchi wa kijiji cha Uchunga.
“Nilihamasika baada ya kupendezwa na wazo la kuanzishwa kwa kituo hiki. Na siku nilipoombwa kuwa sehemu ya kuleta mafanikio, nilikubali mara moja na kushiriki mikutano na ratiba nyingine,” alifafanua katibu wa vijana, Bahati Juma.
Moja ya majukumu aliyokabidhiwa ni huhakikisha kituo kinafunguliwa saa mbili asubuhi na kufungwa saa 10 jioni. Kwa wastani, kituo kinahudumia wanafunzi 20 kwa siku.
Mbali na katibu huyo, watendaji wengine ni pamoja na mkurugenzi, katibu, mhasibu, na kamati tendaji chini ya mwenyekiti na mlezi wa Kituo. Nafasi hizi zote zina wasaidizi isipokuwa ya mkurugenzi na mlezi.
Uongozi huu ulipatikana kidemokrasia kwa kuchaguliwa kwenye mkutano mkuu wa kijiji. Baada ya kupata uongozi walitengeneza katiba na kukisajili kituo chao. Kwa mujibu wa katiba ya kituo hicho, uongozi unachaguliwa kila baada ya miaka mitatu.
“Waasisi wa kituo ndio waliopendekeza mfumo wa uongozi na baada ya hapo wakauwakilisha kwenye mkutano mkuu wa kijiji. Kwa hiyo walioweza walishiriki. Na kila mtu aliyeona anafaa kuwa sehemu ya uongozi wa kituo hicho alipendekeza jina lake ama la mwenzake. Baada ya majina hayo kupatikana ndipo yalipigiwa kura na kupata viongozi,” anafafanua mwenyekiti wa kituo, Michael Butu.
Tukiachilia suala la uongozi, kuna utaratibu maalumu wa kuendesha kituo hicho. Kuna vijana wanaohusika na kuhakikissha ofisi inafunguliwa ili kutoa huduma za kujisoma bure, ikiwa ni mkakati wa kuhamasisha watu na kukifahamu kituo.
Huduma za KIMAJU
Taasisi hii ya kijamii kwa kiasi kikubwa imelenga kwenye uzalishaji maarifa kwa kutoa huduma ya maktaba, ambayo wanafunzi wanaoishi kijiji cha Uchunga hutumia kusoma na kufanya kazi za nyumbani baada ya masomo shuleni.
Katika ziara za ufuatiliaji na uwezeshaji, wafanyakazi wa shirika mtendaji la TAMASHA katika mradi huo wa Chukua Hatua, walishauri kituo kupanua wigo wa huduma zake, kama anavyoelezea Afisa Mradi Winston Churchill.
“Tuliwashauri kuwalenga pia vijana walio nje ya shule ili kuwawezesha vijana wote kutumia kituo hicho vizuri kijijini hapo.”
Watu wazima pia wanatumia kituo hicho kujisomea magazeti, ambayo huwa ni ya siku nyingi na hii ndio sababu ya umuhimu wa kutafuta redio ili watu wasikilize taarifa za habari.
Hali hii imehamasisha wanafunzi wa shule za sekondari na msingi kuja kujisomea, kama anavyoelezea mwanafunzi wa darasa la saba Leticia Isaka kutoka Shule ya Msingi Uchunga,
“Kituo kinanisaidia kutambua mambo mbalimbali, kwa mfano kupitia mafunzo ya hapa, napata malezi bora ya kuniandaa niwe mwalimu au daktari. Lakini si hivyo tu, wakati wa mapumziko ya saa sita huwa tunakuja kujisomea hapa baada ya kupatiwa mazoezi na walimu shuleni,”
Pamoja na sababu nyingine, uwepo wa kituo hiki umechangia kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu katika shule ya sekondari ya kata ya Uchunga, ambapo mwaka 2013 jumla ya wanafunzi .... tu ndio waliofaulu katika ngazi ya ... , wakati mwaka uliofuata waliongezeka na kufikia kiasi cha ...
"Mbali na mafanikio haya, kituo kina changamoto kadhaa ikiwamo ukosefu wa meza, viti na makabati ya kuhifadhia vitabu," anasema mkurugenzi wa kituo, Richard na kuongeza:
“Haya mabenchi na meza tumeazima kanisani na tukimaliza tunarudisha sehemu husika. Hatuna vitabu vya mitaala kwa ajili ya wanafunzi wetu, ingawa eneo la kujisomea lipo vizuri, nishati ya umeme nayo ni shida.”
Kimsingi, wanajamii wa Uchunga kwa kushirikiana na waraghbishi na uongozi kwa kijiji wamefanikiwa kufikia malengo.
No comments:
Post a Comment