Mkuu wa chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbilin (MUHAS) na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Al-Haj Dr Ali Hassan Mwinyi, akimtunuku shahada (degree) ya Uzamili moja wa wahitimu katika Mahafali ya tisa ya chuo hicho yalifanyika mwishoni mwa wiki chuoni hapo jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia ni pamoja na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof Ephata Kaaya (wa kwanza kushoto).
Baadhi ya wahitimu wa chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kutunukiwa shahada ya Uzamivu ya udaktari wa falsafa ya chuo hicho.
Baadhi ya wahitimu wa MUHAS wakila kiapo cha taaluma kwenye mahafali hayo.
Baada ya kiapo ikawa ni furaha na kujipongeza.
Mkuu wa chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbilin (MUHAS) na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Al-Haj Dr Ali Hassan Mwinyi, (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na uongozi wa chuo hicho.
Baadhi ya wahitimu wa chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kutunukiwa shahada zao.
WAHITIMU wa Chuo Kikuu Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kwa mwaka huu wameombwa kuzingatia kauli mbiu ya Rais John Pombe Magufuli ya ‘Hapa ni Kazi tu’ kwa kuwahudumia wananchi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa kulingana na maadili ya taaluma zao.
Wito huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho,Bw Deogratias Ntukamazina, juzi katika Mahafali ya tisa ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye pia ni Mkuu wa chuo hicho.
Alisema ili kutekeleza wajibu wao kwa kasi inayotakikana na Rais Magufuli, wahitimu hao wanatakiwa kuonesha umahiri mkubwa katika kazi zao ili kuwa mfano wa kuigwa utakaokiletea heshima chuo hicho.
“Lakini pia ili kukabiliana na uhaba wa wataalamu wa sekta ya afya nchini, naishauri serikali kupandisha umri wa kustaafu kwa wanataaluma wa elimu ya juu ili kukabili upungufu uliopo kwa sasa kama mkakati wa haraka.
“Pia kuangalia namna ya kuboresha mchakato wa ajira, masilahi na mazingira ya wanataaluma wa elimu ya juu ili kuvutia wataalamu vijana wenye sifa kujiunga na taasisi za elimu ya juu kama mpango wa muda mrefu,” alisema.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Ephata Kaaya, alisema katika mahafali ya mwaka huu jumla ya wahitimu 878 wamehitimu fani mbalimbali kati yao 318 ni wahitimu wa kike sawa na asilimia 36.2
“Katika mwaka huu wahitimu 323 wametunukiwa stashahada, 10 wametunukiwa stashahada za juu katika nafasi mbalimbali za afya na sayansi shirikishi. Pia wahitimu 351 wamepata shahada ya kwanza na wengine 220 shahada ya uzamili. Vilevile wahitimu 11 wametunukiwa shahada za uzamili wa utaalamu mbalimbali na wawili wametunukiwa shahada za uzamivu.
“Pamoja na mambo mengine tunaiomba serikali iendelee kutufadhili ili kukamilisha mradi mkubwa wa ujenzi wa kampasi ya Mloganzila ambayo inatarajiwa kukamilika Juni mwaka 2016. Kampasi hii itakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi zaidi ya 15,000 kutoka wanafunzi 3500 tunaowadahili sasa.
“Pia tunaiomba serikali itupatie kibali cha kuajiri watumishi 968 katika mwaka huu wa fedha 2015/16 ili waweze kuhudumia hospitali ya Kampasi hii inayotarajiwa kukamilika Juni mwaka ujao,” alisema.
Aidha, alisema changamoto za sekta afya nchini ziliainishwa kwenye mpango wa matokeo makubwa sasa, haziwezi kutatuliwa kutokana na ukweli kuwa tathmini halisi ya ajira za wafanyakazi wa afya iliyoainishwa katika mpango huo inaonesha kuwa utaratibu wa ajira katika sekta hiyo una mlolongo mrefu ambao unachelewesha ajira za wafanyakazi hao.
No comments:
Post a Comment