Wednesday, December 16, 2015

WAFANYABIASHARA KUTOKA QATAR WAHIMIZWA KUWEKEZA TANZANIA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa Serikali imeweka mazingira rafiki ya uwekezaji, hivyo alitoa wito kwa wafanyabiashara kutoka Qatar kutumia fursa lukuki za uwekezaji zinazopatikana hapa nchini. 

Balozi Mulamula aliyasema hayo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Taifa ya Qatar iliyofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regence, Kilimanjaro jijini Dar es Salaam jana.

“Tanzania imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, madini, uchukuzi, elimu, afya, nishati, wanyamapori, mafuta na gesi, hivyo natoa wito kwa ndugu zetu wa Qatar watumie fursa ya uhusiano mzuri tulionao kuja kuwekeza nchini”, Balozi Mulamula alisema. 

Balozi Mulamula aliendelea kusema kuwa Serikali inaelekea katika uchumi wa gesi na ina matumani makubwa ya kufaidika na uzoefu wa mshirika wake Qatar ambayo ni mmoja wa wazalishaji wakubwa wa gesi duniani. 

Suala lingine ambalo Katibu Mkuu aliligusia ni umuhimu wa Tanzania na Qatar kuunganisha nguvu ili kutumia rasilimali fedha na ardhi zilizopo kuimarisha sekta ya kilimo kwa madhumuni ya kuodoa changamoto za usalama wa chakula kati ya nchi hizi mbili.

Kwa upande wake, Balozi wa Qatar nchini, Mhe. Abdulla Jassim Al Maadadi pamoja na mambo mengine, aliongelea suala la Qatar kuwa mwenyeji wa mashindano ya mpira wa miguu wa Kombe la Dunia kwa mwaka 2022. Alisema miradi mingi kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo inatarajiwa kukamilika mwaka 2020. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara, mtandao wa reli, viwanja vya mpira, viwanja vya ndege na nyumba za makazi.

Alisema miradi hiyo ni mikubwa hivyo inahitaji wafanyakazi wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani na aliahidi kuwa watu watakaokwenda kufanya kazi nchini humo, haki zao zitalindwa.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi Liberata Mulamula akizungumza kwenye hafla ya kuadhimisha ya Siku ya Taifa la Qatar kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Balozi Augustine Mahiga. Katika maadhimisho hayo, Balozi Mulamula alisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Qatar hususan katika sekta za kiuchumi na biashara. 
Sehemu ya Mabalozi na wageni waalikwa wakimsikiliza Balozi Mulamula (hayupo pichani) 
Balozi Mulamula akiendelea kuzungumza 
Balozi wa Qatar nchini, Mhe. Abdallah Jassim Mohamed Al-Maadadi naye akizungumza katika maadhimisho hayo. 
Sehemu nyingine ya Mabalozi waliohdhuria hafla hiyo. 
Sehemu ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bw. Hangi Mgaka (wa kwanza kulia), na Bw. Batholomeo Jungu (wa pili kutoka kulia) nao wakimsikiliza Balozi Al-Maadadi (hayupo), katika maadhimisho hayo. 
Balozi Mulamula (wa pili kutoka kulia), Balozi wa Qatar nchini (wa tatu kutoka kulia), Balozi wa Demokrasia ya Kongo, Mhe. Juma Mpango (wa nne kutoka kushoto), Balozi wa Oman nchini, Mhe. Soud Ali Bin Mohamed Al Rugaishi (wa kwanza kushoto), Balozi wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), Mhe. Abdulla Ibrahim Ghanim Al suwaidi (wa pili kutoka kushoto) wakishiriki tendo la kukata Keki ya maadhimisho ya Siku ya Taifa la Qatar. 
Balozi Mulamula akizungumza na Balozi Al - Maadadi. 
Balozi Mulamula akimtangaza mshindi wa bahati nasibu iliyochezeshwa hapo jana, mshindi huyo (hayupo pichani) alijishindia tikect ya Ndege ya kuelekea Doha. 
Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Al-Maadadi. 
Katibu Mkuu Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi waliohudhuria maadhimisho hayo. 


Picha na Reginald Philip 

No comments: