Tuesday, December 8, 2015

Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa EU watoa wito kwa ukamilishwaji haraka wa mchakato wa uchaguzi Zanzibar kulingana na kanuni za chaguzi shirikishi, za uwazi, zinazotekelezwa kwa wakati na za kuaminika

Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU EOM) kwa Tanzania unatoa tena wito kwa ukamilishwaji haraka wa mchakato wa uchaguzi Zanzibar kulingana na kanuni za chaguzi shirikishi, za uwazi, zinazotekelezwa kwa wakati na za kuaminika. 

Kufuatia Siku ya Uchaguzi tarehe 25 Oktoba, Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya umebaki nchini kufuatilia chaguzi zilizoahirishwa Tanzania Bara na mchakato uliyositishwa Visiwani Zanzibar, baada ya tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) la tarehe 28 Oktoba, lililofuta matokeo ya uchaguzi mkuu Zanzibar.

 EU EOM ilikutana na wadau wakuu Visiwani, vikiwemo vyama vya siasa, Mwana Sheria Mkuu wa Serikali wa zamani na wa sasa, wadau wa sharia na mahakama, asasi za kiraia na maafisa uchaguzi. Bahati mbaya EU EOM haikuweza kukutana na Mwenyekiti wa ZEC.

EU EOM inafahamu kuhusu mazungumzo yanayoendelea kati ya CCM na CUF, yanayowashirikisha Marais Wastaafu wa Zanzibar. EU EOM inarudia tena wito uliyotolewa kwa pamoja na jumbe zingine za uangalizi za kimataifa tarehe 29 Oktoba, unaoishauri ZEC kuonyesha uwazi kamili kufuatia uamuzi wake wa kufuta uchaguzi na uongozi wa kisiasa Zanzibar kuweka maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar kwanza, kwa lengo la ukamilishwaji haraka wa mchakato wa uchaguzi, kulingana na kanuni za kidemokrasia za chaguzi pamoja na sheria za Zanzibar.

“EU EOM imekuwepo nchini tangu 11 Septemba kufuatilia mchakato wa uchaguzi ndani ya Muungano na Zanzibar. Idadi kubwa ya waangalizi 141 wa EU nchini walirejea Ulaya katikati ya mwezi Novemba, lakini timu ndogo ya watathmini wa uchaguzi ilibaki nchini kufuatilia ngazi zilizobaki za mchakato wa uchaguzi,” alisema Muangalizi Mkuu wa EU EOM, Judith Sargentini.  

“Japokuwa mchakato wa uchaguzi Zanzibar haujakamilika, EU EOM itarejea Ulaya kwa muda tarehe 8 Desemba. Umoja wa Ulaya unaendelea hata hivyo, kuunga mkono kikamilifu mchakato wa uchaguzi Zanzibar na kwa mchakato mpana zaidi wa kidemokrasia Tanzania. EU EOM iko tayari kurejea na kuangalia mchakato wa uchaguzi Zanzibar pindi makubaliano ya kuendelea na mchakato huo yanayolingana na chaguzi shirikishi, za uwazi, zinazotekelezwa kwa wakati na za kuaminika yatakapofikiwa,” aliongeza Muangalizi Mkuu.

EU EOM ilitumwa kufuatia mialiko toka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar. EU EOM inapenda kutoa shukrani zake kwa NEC kwa kuiongezea muda wake kupita muda uliyopangwa awali, jambo linaloashiria upana wa wigo na mamlaka ya EU EOM, ambayo yanahusisha zaidi ya uangalizi wa muda mfupi. Ujumbe ulitoa  tamko lake la awali la mchakato wa uchaguzi tarehe 27 Oktoba. 

Tarehe 29 Oktoba, EU EOM, pamoja na jumba zingine za waangalizi za kimataifa za Umoja wa Afrika, SADC na Jumuiya ya Madola, ilitoa tamko la pamoja kuhus Zanzibar. EU EOM itawasilisha ripoti kamili ya kina, ikiwemo mapendekezo kwa chaguzi zijazo, ndani ya miezi mitatu ya kukamilika kwa mchakato wa uchaguzi.

No comments: