Tuesday, December 8, 2015

TOFAUTI YA SHIRIKA ( FIRM ) NA KAMPUNI KIBIASHARA.

NA BASHIR YAKUB .
BIASHARA  hufanywa kwa mitindo ya aina nyingi kutegemea na mahitaji ya wahusika. Unaweza kufanya biashara kwa mtindo wa kampuni, unaweza kufanya biashara kwa mtindo wa mtu binafsi, lakini pia unaweza kufanya biashara kwa mtindo wa shirika ( firm)/ubia. Mitindo hii yote inatofautiana kiutendaji, kifaida na kiuwajibikaji (liability). 

Kuhusu kampuni tumeeleza mara nyingi faida zake, aina zake, masuala ya hisa, mpaka namna ya kuunda kampuni, ada zinazostahili na kila kitu. Pia yapo makala yaliyoeleza biashara binafsi hasara na faida zake. Leo katika makala haya tutapata kuona biashara ya shirika (firm)/ubia . Tukumbuke kuwa haya yote ni mazao ya sheria na hivyo huwa tunayatizama kwa mtazamo wa sheria.

Sheria imeeleza kwa mapana kabisa aina zote hizi za biashara ili kuepusha migongano baina ya wahusika. Sura ya 345 ya sheria ya mikataba iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 ndiyo inayozungumzia shirika/ubia kama tutakavyoona.

1.SHIRIKA/UBIA NI NINI.
Shirika/Ubia ni uhusiano uliopo baina ya watu wanaofanya biashara ya faida kwa pamoja . Kwa hiyo ili ubia uwepo ni lazima watu wawili au zaidi waungane na waamue kufanya biashara kwa pamoja. Hii ni kwa mujibu kifungu cha 190 cha sheria ya mikataba. Kuungana huku ili kufanya biashara sio kuunda kampuni. 

Ni kuungana ambako hakuhusishi kampuni lakini kunakotambulika kisheria. Muungano wa kufanya biashara kwa pamoja ndio ubia.
Watu walioingia ubia kwa umoja wao wanaitwa shirika ( firm). Kwa hiyo shirika na ubia humaanisha kitu kimoja na ndio maana katika makala maneno haya yanatumika pamoja. Na jina wanalotumia wabia linaitwa jina la shirika ( firm name). 

Mifano ni mingi ila mojawapo ni yale mashirika ya wanasheria yaitwayo law firm, au ya wahasibu yaitwayo accountant firm na mengine mengi. Lakini hata katika biashara za kawaida za uuzaji wa bidhaa na mengineyo nako ubia hufanyika.

2. TOFAUTI YA SHIRIKA UBIA (PARTNERSHIP FIRM ) NA KAMPUNI (COMPANY).
Tofauti ni nyingi ila hizi ni baadhi :
( a ) Katika shirika (firm) ikiwa kuna mkopo umekopwa na shirika kwa ajili ya biashara fulani basi wanashirika wote wanawajibika kwa deni hilo kila mtu mmoja mmoja kwa nafasi yake. Na ikiwa shirika litashindwa kulipa basi  mali binafsi za kila mmoja ya washirika zinaweza kukamatwa kulipia deni hilo. Hii haipo kwenye kampuni. KatIka kampuni haiwezi kutumika mali ya mtu binafsi mwanahisa kufidia deni ambalo kampuni imeshindwa kulipa hasa kama mali hiyo haikutumika kama rehani. Ni mali ya kampuni tu itakayotumika.

( b ) Shirika linaposababisha hasara kwa mtu mwingine ambaye sio mwanashirika kwa maana ya mtu wa tatu basi wanashirika(partners) wanawajibika kufidia hasara hiyo kwa michango yao. Hii ni tofauti na kwenye kampuni ambapo wenye kampuni hawawajibiki kufidia hasara iliyosababishwa na kampuni kwa mtu ambaye si mhusika katika kampuni hiyo. Kampuni kama kampuni ndiyo inayowajibika kufidia hasara hiyo na si wenye kampuni. Mali za kampuni ndizo zitakazotumika na kama hazipo hilo ni jambo jingine. Muhimu ni kuwa mali za wenye kampuni hazitaguswa.

( c ) Katika ubia hakuna mtu anaweza kualikwa kuwa mbia katika shirika bila ridhaa ya wabia wote. Kila mbia ni lazima aridhie ujio wa mbia mpya. Katika kampuni hasa makampuni ya umma (public company) haihitajiki ridhaa ya wana hisa wote ili mtu mpya akubaliwe kuwa mwanahisa. 

3. KANUNI KUU ZINAZOONGOZA SHIRIKA (FIRM).
Kanuni kuu inayoongoza shirika ni makubaliano ya kimkataba. Kile mnachokubaliana kimkataba ndicho kinachotakiwa kutekelezwa. Kama hakuna makubaliano yoyote basi masharti yaliyo katika kifungu cha 194 cha sheria ya mikataba ndiyo yatakayotumika kama makubaliano yenu. Masharti hayo ni pamoja na kila mbia kuwa sehemu ya uongozi wa shirika, maamuzi kufanywa kwa kura za walio wengi, haki ya kukagua vitabu vya shughuli za shirika, kugawana faida kwa usawa, n.k.

4. SHIRIKA (FIRM) HUSAJILIWA WAPI.
Mashirika (firm) husajiliwa kwa msajili wa makampuni na biashara BRELA. Vipo vyeti maalum ambavyo hutolewa kwa ajili ya usajili baada ya ada ya usajili hulipwa. Katika makala nyingine tutaona kipi bora kibiashara kati ya shirika (firm) na kampuni ( company).

MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE, GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com

No comments: