Tuesday, December 1, 2015

Taarifa ya Balozi Sefue kuhusu kurejeshwa fedha kutoka Uingereza


Utangulizi

1.1             Jana, tarehe 30 Novemba, 2015, mahakama jijini London ilitoza Standard Bank $ 32.2 milioni. Kati ya hizo $ 16.8 milioni ni faini inayolipwa kwa Serious Fraud Office (SFO), $8.4 milioni ni “disgorgement of profits”; na $ 7 milioni zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania. Fedha hizo ni $ 6 milioni ambazo tulitozwa isivyostahili na $ 1 milioni ni riba ya fedha hizo. Fedha tunazorejeshewa zililipwa isivyostahili kwa kampuni ya Kitanzania iitwayo EGMA. Kesi inayohusika ilifunguliwa na SFO dhidi ya Standard Bank.

1.2             Mwaka 2012/13, Serikali ya Tanzania iliamua kukopa fedha ($600 milioni) kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Huu ni utaratibu wa kawaida, ambapo Serikali inaingia mkataba na Benki moja (Lead arranger) ambayo inatafuta fedha kutoka kwenye benki na taasisi nyingine za fedha. Ni utaratibu wa kawaida pia kuwa Lead Arranger analipwa ada kwa kazi hiyo.

1.3             Serikali ya Tanzania ilitoa kazi hiyo kwa Standard Bank, kupitia Stanbic (T) Ltd. Fedha tulizohitaji, $600 milioni ambazo wakati huo zilikuwa sawa na Sh.947,673,240,000.00 zilipatikana na zikatumika kama ilivyokusudiwa. Standard Bank ililipwa asilimia 2.4 ya fedha hizo kama ada yao. Mkopo ulikuwa na masharti ya grace period ya miaka miwili na nusu na kulipwa kwa miaka 7 (2019).


2.0             Uchunguzi Nchini Tanzania

2.1             Mwaka 2013 kulikuwa na matatizo kwenye Stanbic Bank (T) Ltd, wakati huo ikiongozwa na Bwana Bashir AWALE. Kwa kutumia mamlaka yake chini ya Kifungu 47 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 na Kifungu 31 cha Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu ilifanya ukaguzi wa kulenga (Targeted Examination) benki hiyo.

2.2             Wakaguzi wa Benki Kuu, pamoja na mambo mengine, walibaini malipo yasiyokuwa ya kawaida kuhusiana na kampuni ya Kitanzania inayoitwa EGMA. Malipo hayo yalikuwa kinyume na taratibu za kibenki, na baadhi ya watumishi wa Stanbic Bank (T) walishindwa kuvumilia hali hiyo. Wakaguzi wa Benki Kuu walifuatilia malalamiko hayo na kujiridhisha kuwa uongozi wa Stanbic Bank (T) ulifanya mambo ambayo ni kinyume na taratibu zinazokubalika kibenki. Fedha kiasi cha $ 6 milioni kiliingizwa kwenye akaunti ya EGMA na siku chache baadaye zilitolewa zote kwa fedha taslimu na wala benki haikukusanya kodi ya zuio (withholding tax) kwa mujibu wa sheria ya mapato ya kodi ya mwaka 2004 kutokana na mapato ya Standard Bank kwa kazi ya ushauri iliyoifanya.

2.3             Kama ulivyo utaratibu, Benki Kuu ilitoa taarifa ya ukaguzi kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Stanbic Bank (T) Ltd na kuitaka Bodi hiyo kuchukua hatua za kurekebisha kasoro ndani ya benki, pamoja na kutoa taarifa kwa Financial Intelligence Unit kuhusiana na miamala yenye mashaka kwenye akaunti ya EGMA kwa mujibu wa Sheria ya Anti-Money Laundering Act 2006.

2.4             Taarifa tulizopewa ni kuwa bodi ilikutana na kuchukua hatua zinazostahili, ikiwemo kutoa taarifa FIU kuhusiana na miamala kwenye akaunti ya EGMA, na kwa Wizara ya Fedha kuhusiana na kodi ya zuio.

2.5             Vile vile tumesikia kuwa bodi ya Standard Bank iliona kuwa makosa yaliyobainishwa na wakaguzi wa Benki Kuu ya Tanzania yalistahili kutolewa taarifa kwa SFO nchini Uingereza ambao walianzisha uchunguzi ambao hatimaye ulipelekea kesi kufunguliwa.

3.0             Udanganyifu ulivyofanyika

3.1             Kwa taarifa zilizopo, inaelekea kuwa Standard Bank ilipanga kututoza ada ya asilimia 1.4 tu, yaani $ 8,400,000. Hata hivyo ukafanyika ujanja wa kudai kuwa ati anahitajika local agent wa benki hiyo, ambaye naye alipwe asilimia 1 nyingine, na kufikisha ada yote kuwa asilimia 2.4 ($14,400,000).

3.2             Local agent huyo alikuwa kampuni ya EGMA, ambayo miamala yao kuhusiana na hizo $6,000,000 walizochukua ndiyo ilishtua wakaguzi wa Benki Kuu na taarifa kutolewa kwa Bodi ya Stanbic (T) Ltd na hatimaye Standard Bank, SFO na Mahakama Uingereza.


4.0             Uchunguzi Uingereza

4.1             Tarehe 29 Septemba, 2015, Mkuu wa Idara ya Rushwa kwenye SFO aliiandikia Benki Kuu, akiomba ushirikiano wa Benki Kuu kwenye uchunguzi na uendeshaji wa kesi dhidi ya Standard Bank Plc (ambayo sasa inajulikana kama ICBC Standard Bank Plc).

4.2             Tarehe 29 Oktoba, 2015, Benki Kuu, iliiandikia SFO kutoa taarifa kuhusu ukaguzi-lengwa ambao Benki Kuu iliufanya tarehe 15 – 19 Julai, 2013 kwenye Benki ya Stanbic Bank (T) Ltd. Ushahidi huo kutoka Benki Kuu ulikuwa sehemu ya ushahidi uliosaidia SFO kushinda kesi. Katika kipindi chote ambacho SFO ilikuwa inafanya uchunguzi, ilishirikiana na taasisi zetu ikiwamo TAKUKURU, Benki Kuu, FIU na wengine. Mafanikio haya yaliyopelekea kwenye uamuzi wa Tanzania kurejeshewa $ 7 milioni (Sh.15 bilioni/=) yametokana na dhamira  ya kweli ya Serikali ya  Uingereza na Serikali ya Tanzania kupambana na rushwa.

5.0             Hitimisho

5.1       Tunaishukuru Serikali ya Uingereza, pamoja na SFO, kwa kuonesha njia katika kusaidia nchi maskini zinazodhulumiwa na wapokea rushwa na watoa rushwa. Maana zipo nchi nyingine tajiri ambazo wanapigia kelele rushwa kwa kuangalia upande wa mpokeaji tu, na kusahau makampuni makubwa kutoka kwao yanayopenda kuhonga watu wetu. Natoa wito kwa nchi nyingine tajiri kutoa ushirikiano kama huu wa Serikali ya Uingereza. Nazishukuru taasisi zetu, Benki Kuu, na TAKUKURU, FIU na wengine kwa kutimiza wajibu wao na kutoa ushirikiano kwa SFO uliowezesha SFO kushinda kesi hii, na sisi kurejeshewa fedha ambazo zitatumika kutatua matatizo yetu ya maendeleo na kero za wananchi.

5.2       Baada ya ushindi huo uchunguzi unaendelea ndani ya nchi ili tujue hizo $ 6 milioni zimekwenda wapi, na kama zilitumika kumhonga mtu tujue ni nani. Katika hili tutaomba ushirikiano wa wenye kampuni hiyo ya EGMA ambao kwa taarifa za vyombo vya habari vya Uingereza ni Bwana Harry KITILLYA, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bwana MBOYA ambaye ni marehemu na Bwana Gasper NJUU.  
 



No comments: