Remija Salvatory na Nuru Mwasampeta
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Omar Chambo amewaagiza Madaktari wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama kuandaa utaratibu wa kuwawezesha wahanga wa Mgodi wa Nyangalata kwenda Hospitali za rufaa kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya zao.
Mhandisi Chambo aliyasema hayo alipowatembelea wahanga hao waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama kutokana na ajali ya kufukiwa na kifusi na kufanikiwa kuokolewa baada ya kuishi chini ya ardhi kwa siku 41 katika Mgodi wa Nyangalata mkoani Shinyanga.
Katibu Mkuu alitoa maagizo hayo baada ya mmoja wa wahanga hao, Joseph Buruge kueleza kuwa ingawa ngozi za wachimbaji hao zinaonekana kuimarika lakini bado kuna tatizo la vijipele vidogo vidogo mwilini ambavyo baada ya muda hutoa usaa hivyo aliomba uchunguzi wa kina ufanyike ili kutibu tatizo hilo.
“Kwa kweli Mheshimiwa tunaendelea vizuri na matibabu na tunawashukuru madaktari na wauguzi wote wanaotuhudumia na tunaishukuru Wizara na Serikali kwa ujumla kwa misaada na huduma walizotoa, lakini kwa sababu umekuja Mheshimiwa tuna maombi yetu ambayo tunaomba Serikari iweze kutusaidia sisi wahanga wote” , alisema Buruge.
Buruge alisema kuwa pamoja na kuwa afya zao zinaimarika lakini kuna viashiria ambavyo si vizuri kwa sababu ya kula magome ya miti na wadudu chini ya mgodi hivyo wanahitaji uchunguzi kwani magome ya miti yalikuwa yakiwalevya kama wamekunywa pombe kali hivyo ni vyema uchunguzi ukafanyika ili kujua kama magome hayo yalikuwa na sumu na athari zake katika miili yao.
Pamoja na hayo, wameomba pia kufanyika kwa uchunguzi wa tumbo kwa kuwa maji machafu waliyokuwa wakinywa chini ya mgodi yalikuwa na kemikali kwani yalikuwa yamechanganyika na baruti hivyo ni vema kufahamu baruti iliwaathiri kiasi gani.
Baada ya maombi hayo, Mhandisi Chambo aliwaahidi wahanga hao kuwa ataendelea kufanya mawasiliano na Madaktari wa Hospitali hiyo ili kuhakikisha majibu ya maombi yao yanafanyiwa kazi kwa wakati. Aidha aliwahakikishia kuwa vipimo vyote wanavyotakiwa kufanyiwa vitagharamiwa na Serikali.
Alipotakiwa kuanza taratibu za kuwahamishia wahanga hao katika hospitali ya Rufaa ya Bugando, Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Robert Rwebagira alisema kuwa wahanga hao wanahitajika kwenda Hospitali kubwa ya Muhimbili kwani wataweza kupata huduma zote ambazo zitachukua si chini ya miezi Sita.
Alisema kuwa huduma za awali walizopatiwa wahanga hao zilikuwa ni kuangalia miili yao (Physical treatment) na sasa wanahitaji matibabu ya kisaikolojia na kiakili ambayo yatapatikana katika hospitali ya Rufaa ya Muhimbili.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kahama Mjini Jumanne Kishimba ameahidi kushirikiana bega kwa bega na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Vita Kawawa pamoja na Hospitali hiyo ili kuhakikisha kuwa wahanga hao wanapata huduma stahiki na ndani ya wakati.
Wahanga Watano wa mgodi wa Nyangalata waliopokelewa katika hospitali ya wilaya ya Kahama tarehe 16/11/2015 ni Amos Muhongo, Joseph Buruge, Msafiri Gerard, Chacha wambura na Onyiwa Kaiwao ambaye kwa sasa ni marehemu.
No comments:
Post a Comment