Thursday, December 10, 2015

RAIS MSTAAFU JAKAYA KIKWETE ASHIRIKI ZOEZI LA USAFI SOKO KUU LA CHALINZE

Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Eng. Evarist Welle Ndikilo wakielekea soko kuu la Chalinze kushirikiana na wananchi kufanya usafi wa mazingira leo Desemba 9, 2015 ikiwa ni kuadhimisha miaka 54 ya UHURU kama ilivyoagizwa na Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli
Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakifanya usafi katika soko kuu la Chalinze leo Desemba 9, 2015 ikiwa ni kuadhimisha miaka 54 ya UHURU kama ilivyoagizwa na Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli
Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakifanya usafi katika soko kuu la Chalinze leo Desemba 9, 2015 ikiwa ni kuadhimisha miaka 54 ya UHURU kama ilivyoagizwa na Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli
Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na wananchi wa Chalinze baada ya kushirikiana nao kufanya usafi wa mazingira ya soko kuu la Chalinze leo Desemba 9, 2015 ikiwa ni kuadhimisha miaka 54 ya UHURU kama ilivyoagizwa na Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli.

RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, amesema katika uongozi wake wa miaka 10, hakuwahi kuagiza mtu asamehewe kontena lake lisilipe kodi na angefanya hivyo, mapato ya Serikali yasingeongezeka kutoka Sh bilioni 177 kwa mwezi mpaka Sh bilioni 900.

Akizungumza baada ya kuwashitukiza wananchi wa Chalinze katika Soko Kuu la eneo hilo kwa kuungana nao kufanya usafi kuitikia agizo la Rais John Magufuli jana asubuhi, Kikwete alisema katika uongozi wake hakuwahi kuagiza mtu anayestahili kulipa kodi asilipe kodi.

Amesema wakati huu ambao amepumzika baada ya kustaafu, amepata nafasi ya kusoma mitandao na magazeti mbalimbali na kukuta baadhi ya watu wakimshutumu na kumtukana yeye na familia yake wakimuhusisha na ukwepaji kodi.

“Ni afadhali wanishambulie mimi ila wamuache Rais Magufuli (John Pombe) afanye kazi, ni maneno ya walioshindwa wasinilaumu, aliyewashinda ni Magufuli sasa hawana la kusema. Ni sawa na siasa za maji taka lakini watakuwa wanapoteza muda wao na kufanya kazi bure, kwa kuwa mimi sigombei kitu chochote tena.

“Wanahusisha mpaka na familia yangu, kama mimi mwenyewe sijawahi kuruhusu mtu hata mmoja atoe kontena bila kulipia kodi, siamini kama mke wangu (Mama Salma) au mwanangu Ridhiwani (Mbunge wa Chalinze), wengeweza kufanya hivyo tu na watu wakawasikiliza.

“Wanachonga tuu, wengine wamesema Kikwete hachomoi, kwani nimechomeka nini?” Alihoji na kusababisha watu walioshirikiana naye kufanya usafi katika soko hilo kucheka na kuanza kushangilia.

Alisema nafasi ya urais aliyoaminiwa na Watanzania kwa miaka kumi, ilikua yake na haikuwa na ubia na mkewe wala mtu mwingine yeyote.

Kikwete aliwataka Watanzania wamuunge mkono Rais Magufuli katika jitihada anazofanya za kukabiliana na wakwepa kodi, huku akitoa mfano akisema wakwepa kodi kwa Serikali ni kama inzi na kidonda, hawaondoki bila kufukuzwa na ukiacha kuwafukuza wanarudi.

Aliwakumbusha wananchi kwamba Serikali ina wajibu wa kutumikia wananchi katika mahitaji yao, ambayo utekelezaji wake unahitaji fedha.

“Serikali ina wajibu kwa wananchi, wanataka barabara, shule, hospitali ziwe na dawa na mengine mengi, lakini haya yote yanahitaji fedha na Serikali inapata fedha kutoka katika vyanzo vya kodi,” alisema.

Alisema pia yapo mapato mengine ikiwemo ushuru mbalimbali kama katika kulipia leseni, hati za kusafiria na nyingine, lakini pia Serikali inaweza kuchukua mikopo na misaada.

Hata hivyo alisema Serikali inapaswa kuimarisha ukusanyaji wa mapato hasa ya kodi, ikiwemo kodi ya mapato na ushuru wa forodha na hayo ya mikopo na misaada, yanatakiwa iwe sehemu ndogo ya mapato ya Serikali.

Kikwete alisisitiza yeye wakati wa uongozi wake kazi hiyo ya kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya ya upotevu wa mapato ilifanyika, ndio maana akafanikiwa kuongeza makusanyo ya kodi kutoka Sh bilioni 177 kwa mwezi mpaka Sh bilioni 900.

Pamoja na mafanikio hayo ya uongozi wake, Kikwete alisema bado mahitaji ya Serikali kwa watu wake yameendelea kuwa makubwa, kuliko upatikanaji wa mapato.

“Tunapaswa kuendelea kuboresha mifumo ya kodi, taasisi za mapato na kupata watendaji waadilifu, kwa kuwa kama mifumo na taasisi vikiwa imara, lakini watendaji si waaminifu haisaidii.

“Hajazaliwa mtu anayependa kulipa kodi, ndio maana wanaokwepa kodi wanatumia uzembe wa watendaji na wengine wanatumia rushwa…sasa uzembe na ulaji wa rushwa lazima tupige vita na hiyo ndiyo kazi anayofanya Rais Magufuli ya kupambana na wazembe na wala rushwa,” alisema Kikwete.

Kikwete alisema kazi hiyo anayofanya Dk Magufuli ni kubwa kwa kuwa inahusisha kunyang’anya tonge watu na kusisistiza namna bora ya kumuunga mkono Rais Magufuli, ni kulipa kodi na wakusanyaji wa mapato ya Serikali wawe waaminifu.

“Ukitaka kuongeza mapato bila kuziba mianya ya kuvuja kwa mapato ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu na anachofanya Rais ni kuumbua wote wanaokwepa kodi,” alisema Kikwete.

*Kamati Kuu
Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, alisema hata katika kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho walichokaa juzi, waliamua kumuunga mkono Rais Magufuli na kuwataka wanachama wote wa chama hicho kufanya hivyo.

“Ni pale tu mapato yatakapoongezeka, ndipo wajibu wa Serikali katika kuhudumia wananchi utawezekana , tukimuunga mkono Rais wetu mzuri ataweza na mapato yakiongezeka, maji yatapatikana, mapato yakiongezeka, zahanati na hospitali zetu zitapata dawa za kutosha, mapato yakiongezeka barabara za lami zitajengwa,” alisisitiza.
Kikwete alisema akizungumzia kudhibiti upotevu wa mapato na kuongeza mapato ya Serikali Kuu, hivyo hivyo inapaswa kutekelezwa katika halmashauri.
Alisema katika Serikali Kuu, makusanyo yako nyuma ya asilimia 10 ya lengo, lakini kwa juhudi za Rais Magufuli, hali inavyokwenda lengo hilo litapitwa na Serikali itaanza kuzungumzia makusanyo ya matrilioni kwa mwezi.
Hata hivyo alisema juhudi hizo za Serikali Kuu hazionekani katika halmashauri ambako ni kama hakuna kazi inayofanyika na hata pale kunapokuwa na juhudi za kukusanya mapato, wakati mwingine yanaishia mikononi mwa wajanja. 
*Usafi
Kikwete ambaye alifanya usafi katika soko ikiwemo kufagia, kukusanya na kuzoa taka akiwa na mkewe, huku akikataa kuvaa vifaa vya kuzuia vumbi, aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kufanya usafi.

Alisema uamuzi wa Rais Magufuli wa kutuma maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru kuwataka wananchi wote wafanye usafi ni wa busara na si wa kukurupuka kwa kuwa mwaka huu taifa lilikabiliwa na ugonjwa wa kipindupindu.

Kikwete alisema tangu Mei mwaka huu mlipuko wa ugonjwa huo ulipoanza Dar es Salaam, ulisambaa kwenye mikoa 19 na kuambukiza watu 10, 894 huku watu 109 wakifariki.

“Kipindupindu si rehema ya Mungu ni uchafu na kinasababishwa na kula uchafu na kinyesi huku mwenezaji mkubwa akiwa inzi. Ukijiepusha kula chakula kichafu, utajiepusha na kipindupindu,” alisema Kikwete.


Aliwataka wananchi wasisubiri kukumbushwa, bali wajenge tabia ya usafi na usafi huo uanzie nyumbani na wananchi na viongozi wahakikishe maeneo mengine ikiwemo sokoni, hospitalini na katika vituo vya mabasi kunakuwa safi na kuhakikisha utamaduni wa usafi unakuwa sehemu ya maisha na si kusubiri kukurupushwa.

No comments: